Kumekuwa na video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, hususan Instagram, ikimuonesha Mkuu wa Kitengo cha Habari wa CHADEMA, Brenda Rupia, akitoa kauli ambazo zimefasiriwa kuwa chama hicho kina ajenda ya kufanya vurugu.
Katika chapisho hilo, mwandishi amedai kuwa:"Huyu ni msemaji wa CHADEMA. Inashangaza kuona binti mdogo kama huyu akiunga mkono ajenda za uvunjifu wa amani na kukaa mbele ya kamera akisema kuwa chama chao kinapanga kufanya fujo."
Aidha, chapisho hilo limeendelea kudai kuwa:"Bila shaka taarifa aliyoisoma iliandaliwa na Heche, na yeye akakabidhiwa tu ili aisome. Hata hivyo, ukweli ni kwamba Watanzania hawahitaji fujo; hawahitaji kuona miundombinu wanayoitumia kila siku ikiharibiwa wala mali zao zikiibiwa. Wanachohitaji ni amani, utulivu na maendeleo."
Je ni upi uhalisia wa chapisho hilo linalosambaa kwa kasi zaidi kwenye mitandao ya kijamii ?
Your browser is not able to display this video.
Tunachokijua
Madai
Ipo video inayosambazwa mtandaoni ikimuonesha Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, akisema wao kama chama ajenda yao ni kufanya vurugu.
Je, ni upi uhalisia?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck umejiridhisha kuwa video hiyo imepotoshwa uhalisia wake kwa kuondoa baadhi ya vipande hatimaye kutengeneza ujumbe ambao ni tofauti na uliotolewa na Rupia.
Katika video halisi akizungumza na waandishi wa habari Juni 16, 2026 Brenda Rupia alisisitiza kuwa chama chao hakina nia yoyote ya kufanya vurugu bali ajenda yao kuu inabaki kuwa amani kupitia uzinduzi wa operesheni ya "Katiba Mpya" na "Free Tundu Lissu" inayotarajiwa kuanza Juni 18.
"Nilifanya press wiki mbili nafikiri zilizopita, na nikazungumza kuhusu jeshi la polisi ambalo lilichukua vifaa vya uenezi kutoka kwa ndugu Mbyela ambaye ndiye muuzaji mkuu wa vifaa vya uenezi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo. Na walichukua track suti nyingi, walichukua kombati nyingi lakini walichukua skafu zetu na na na viremba vingi.
Tunafahamu nia yenu ovu ya kutaka kutumia hizo yunifomu za Chadema, na mkawavisha mnaowajua nyinyi kwa madhumuni ambayo mnayajua nyinyi ili kuleta taswira kama chama cha Demokrasia na Maendeleo ndicho ambacho kinaenda kufanya vurugu siku ambayo mmeipanga nyinyi. Lakini sisi kama chama ajenda yetu ni katiba mpya, Free Tundu Lissu. Na hatutasimama kama nilivyotangaza hii operesheni ndugu wananchi naomba iwe ndio stori na ajenda yetu ya chama.
Hatuna hatuna nia ovu na nchi hii. Hatuna nia ovu ya kufanya vurugu kwenye nchi hii. Hii nchi ni yetu sote na lengo la kuitisha hii press conference ingawa limekuwa ni fupi, lakini imekuwa lengo kuu ni kutangaza operesheni katiba mpya operesheni Free Tundu Lissu ambayo itaanza tarehe 18 June." - Rupia alisema