Viongozi wa nchi wanachama wa BRICS ambazo ni kundi la nchi zinazoibukia kiuchumi, wamemaliza mkutano wao kilele wa 15 wa kila mwaka uliofanyika huko Afrika Kusini. Katika mkutano wa safari hii ambao umeanza Agosti 22 na kuendelea hadi Agosti 24, umekuwa ukifuatiliwa zaidi na watu mbalimbali duniani, hasa baada ya kutangazwa kwamba mbali na mada nyingine lakini mada itakayopewa uzito zaidi ni kuhusu kuongeza wanachama wa kundi hili.
Zaidi ya nchi 40 zimetangaza nia ya kujiunga na BRICS yenye wanachama ambao ni pamoja na Brazil, Russia, India, China, na Afrika Kusini. Wakiwa wamechoshwa kabisa na jumuiya za magharibi na pia kama mbadala wa makundi ya kimataifa yanayoongozwa na nchi za magharibi likiwemo kundi la nchi saba (G7), nchi hizi zinatumai kwamba mchakato wa kujiunga na muungano huu hautachukua muda mrrefu hasa ikizingatiwa kwamba ni muungano unaojali zaidi maslahi ya kila upande, tofauti na baadhi ya makundi ambayo yanaweka mbele maslahi ya baadhi za nchi zenye nguvu tu.
Hatua hii imefanya baadhi ya nchi za magharibi kuonekana kuwa na kitumbo joto hivi sasa, wakijua kwamba kadiri BRICS inavyozidi kupanuka ndivyo ushawishi wao utakavyopungua. Ni miaka mingi imepita sasa tangu BRICS iongeze mwanachama wake mpya ambayo ilikuwa ni Afrika Kusini. Mwaka 2010 Afrika Kusini ilianza juhudi zake za kujiunga na kundi hili, ambapo Disemba 24 mwaka huohuo ikawa mwanachama rasmi wa BRICS, baada ya kualikwa rasmi na China kujiunga na kukubaliwa na nchi nyingine wanachama.
Kama wahenga wanavyosema "Ukitaka kwenda haraka, nenda peke yako; ukitaka kwenda mbali, nenda pamoja na wenzako". Nchi nyingi za Afrika zinafahamu kwamba China ambayo ni mwanachama muasisi wa BRICS, hivi sasa inasonga mbele kwa kasi kimaendeleo, jambo hili limefanya hata baadhi ya wataalamu kusema kwamba baada ya miaka kumi au kumi na tano mbele uchumi wa China unaweza kuja kuupiku wa Marekani. Hii inaonesha nguvu na dhamira kubwa ya nchi hii kutaka kupata maendeleo pamoja na nchi nyingine bila kujali ni za bara gani, na ndio maana alitoa wazo hili la kuanzishwa BRICS.
Katika hotuba yake kwenye mkutano wa BRICS rais Xi alisisitiza kwamba nchi wanachama wake daima wanatetea na kutekeleza sera huru za kigeni. Kila mara wanashughulikia masuala makuu ya kimataifa kulingana na faida zake, kutoa maoni ya haki na kuchukua hatua za haki. Na kwamba nchi za BRICS zina makubaliano ya kina na malengo ya pamoja.
Hivyo baada ya kufuatilia kwa makini mwenendo wa muungano huu wa BRICS, bila shaka nchi nyingi zinashawishika kujiunga nao, zikijua kwamba na zenyewe hazitaachwa nyuma bali zitafuatana mguu kwa mguu na waasi wa BRICS katika kuzinyanyua kimaendeleo na kiuchumi.
Sasa hivi inaonekana kuwa shauku ya kujiunga na BRICS imekuwa kubwa, hasa kwa nchi zinazoendelea, na cha kutia moyo ni kwamba rais Xi kwenye hotuba yake alithibitisha mbele ya wajumbe wa mkutano kwamba wakiwa kama nguzo ya BRICS, watachukua hatua kwa moyo wa BRICS ambao ni wa uwazi, wa ushirikishwaji na ushirikiano wa kunufaishana ili kuleta nchi nyingi zaidi katika familia ya BRICS, na kuunganisha hekima na nguvu zao katika kufanya utawala wa kimataifa kuwa wa haki na usawa zaidi.
Kauli hiyo ya rais Xi ilionesha matunda yake kwani kabla ya wajumbe kufunga makabrasha yao na kumaliza mkutano huo, nchi sita zilitangazwa kujiunga na BRICS zikiwemo Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Argentina, Iran na Ethiopia. Baada ya kutolewa tangazo hilo, viongozi na maafisa wa nchi hizo sita walipongeza mwaliko huo na kutarajia kuimarisha ushirikiano.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa zamu wa nchi za BRICS alisema kwamba nia ya kuunga mkono upanuzi wa BRICS imeelezwa na wanachama wake wote. Kwa maana hiyo hivi sasa wanachama wa BRICS wapo kwenye kilele cha kupanua familia hii ya BRICS na kuwa kubwa zaidi.
Ingawa nchi za magharibi hapo awali zilidai kwamba upanuzi huu unapingwa na nchi mbili wanachama za muungano huo ambazo ni Brazil na India, lakini Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alithibitisha kuwa shutuma hizo si za kweli kwani naye pia amesema anaunga mkono kuwafungulia mlango wanachama wapya na "anakaribisha kusonga mbele kwa makubaliano".