Buku la Biubwa Amour Zahor limefunua chano hadharani

Buku la Biubwa Amour Zahor limefunua chano hadharani

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
BUKU LA BIUBWA AMOUR ZAHOR LIMEFUNUA CHANO HADHARANI

Jana Zanzibar kulikuwa na mambo matatu makubwa kwa aina yoyote ya kipimo.

Kulikuwa na kongamano la Maalim Seif Foundation, Maadhimisho ya Utawala wa Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Mwinyi kutimiza mwaka na Uzinduzi wa Kitabu, ''Mwanamke Mwanamapinduzi.''

Shughuli hizi zote zimefanyika sehemu moja - Golden Tulip Hotel.

Asubuhi kulikuwa na shughuli mbili zikenda sambaba - Kongamano la Maalim Seif na Maadhiisho ya Utawala wa Rais wa Zanzibar Dr. Husein Mwinyi.

Jioni ndiyo kulikuwa na uzinduzi wa kitabu, ''Mwanamke Mwanamapinduzi,'' kilichoandikwa na Zuhura Yunus.

Mwanzoni mwa kitabu tu Biubwa anaeleza kama utangulizi wa kitabu cha maisha yake kuwa kashiriki katika mapinduzi na mengi aliyofanya yameleta ‘’amani, utulivu na upendo.’’

Maneno mazito yanayohitaji tafakuri.

Niliposoma sentensi hii mwanzo wa kitabu nilijua kuwa hiki si kitabu chepesi.

Hii ikanikumbusha Macbeth ya William Shakespeare anafungua kitabu chake na "The Three Weird Sisters."

Kama hilo halikutosha nyuma ya kitabu katika "blurb" yameandikwa maneno ''mapinduzi matakatifu.''

Asubuhi na mapema, alfajir nikawa nimetambua kuwa haitakuwa rahisi kwangu kufanya pitio la kitabu hiki.

Narudia tena kusema kuwa kama na hili halikutosha kila nilipofungua kurasa kusoma, (na hapa nakiri kuwa hiki ni ''fast book,'' yaani ni kitabu kinachokwenda kasi) nakutana ndani ya kitabu majina ya watu ambao nawafamu kwa karibu na mbali kwa njia moja ama nyingine na wote wamo katika, ''dramatis personae," ya mapinduzi.

Hili ni tatizo kubwa kwangu.
Hii inahitaji makala yake pekee inayojitegemea.

Kitabu hiki kinahitaji kufanyiwa pitio na mtu asiyeijua historia ya Zanzibar, lakini mtu huyo hii leo utamtoa sayari gani?

Nani asiyejua historia ya Zanzibar?

Kitabu hiki kupitia maisha ya Biubwa kimeeleza ubaguzi katika uhalisia wake.

Yawezekana kuwa historia ya Biubwa ni ‘’isolated case,’’ isiyowezekana kujenga hoja madhubuti?

Kitabu kinaeleza yaliyotokea kwenye Uchaguzi wa Juni 1961 na kitu cha kufikirisha sana ni vurugu za mfano wa hizo zimekuwa zikirejea kila uchaguzi Zanzibar nusu karne baada ya mapinduzi.

Wazanzibari bado wanauliwa katika kila uchaguzi.

Lakini Biubwa anasema mapinduzi ambayo yeye ameshiriki yameleta, "amani, utulivu na upendo."

Kitabu hiki ni kamusi ya visa vya kusikitisha vya mapenzi yaliyomkuta binti mdogo wa miaka 18 akihangaika na uzito wa kutafuta faraja mahali pasipo na faraja ila ukame katika mapambano baina ya ASP na Hizbu.

Fikiria Unguja ya miaka hiyo Biubwa msichana wa Kiarabu mtoto mdogo wa miaka 18 tena bado mwanafunzi anawaletea wazee wake mchumba Mzungu.

Maneno ya posa anapeleka nani, nani mpokeaji na tujaalie posa imekubaliwa na mchumba kasilimishwa akdi inafungiwa wapi?

Waingereza wangesema, ''sheer spectacle.''
Vichekesho!

Lakini hata alipotokea kutaka kuolewa na Mzanzibari mwenzake kijana msomi daktari muhitimu wa chuo Cha Makerere, Dr. Hassan Kingwaba, kasoro ikawepo.

Rangi ya Dr. Kingwaba.
Lakini huyu si Muislam?

Kwani Uislam unajali rangi?

Ataolewaje na Mwafrika ilhali yeye ni Mwarabu?

Wengi kwa miaka mingi sana wamemuhukumu Biubwa kwa historia yake katika mapinduzi ya mwaka wa 1964, mapinduzi ambayo yalisababisha baba yake mwanachama wa Hizbu kuuliwa akiwa jela.

Katika kitabu hiki Biubwa kajipa mwenyewe haki ya kusikilizwa kwani mahakama ilimuhukumu bila ya kumpa nafasi ya kujieleza.

Inawezekana labda kwa yeye sasa kujieleza baada ya nusu karne hakimu ataelewa yaliyomfika hadi kufikia pale alipofika akawa amebeba bunduki katika vichochoro vya Stone Town wakati Waarabu ndugu zake wamejifungia majumbani mwao kwa kuogopa kuuliwa na askari wa John Okello.

Screenshot_20211107-090205_Facebook.jpg
 
Back
Top Bottom