Bunge la katiba ni mchezo wa namba

IslamTZ

JF-Expert Member
Joined
Nov 22, 2010
Posts
309
Reaction score
182
WAKATI tukijiandaa kwa Bunge maalumu litakaloanza wiki ijayo, Nigeria wameandaa mjadala wa kitaifa utakaofanyika baadaye mwaka huu kutafuta mwelekeo mpya mmoja wa kitaifa katika mambo muhimu.

Bunge hilo maalumu linakuja baada ya Rais Jakaya Kikwete kutimiza jukumu lake la kisheria la kuteua wajumbe 201 watakaoungana na wabunge wote na wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kuunda Bunge hilo la wajumbe 640 litakalotimiza shughuli hiyo muhimu kwa mstakabali wa Taifa.

Kule Nigeria, mdahalo wa kitaifa unalenga kutibu vidonda vya taifa hilo lenye mivutano na migawanyiko ya kidini, kabila, kisiasa na kiuchumi, mdahalo ambao baadhi ya Watanzania wamekuwa wakisema ndio ungetangulia kabla ya zoezi la uandishi wa Katiba mpya.

Nilivutwa na taarifa katika tovuti ya Nigerian Watch kwa hatua ya Umoja wa Dini za Asili wa Nigeria kutishia kuitisha maandamano kupinga kutojumuishwa kwa wawakilishi wa dini hizo katika mdahalo huo ambao watu sita kutoka katika dini mbili za kiislamu na kikristo ni miongoni mwa wajumbe 492.

Msemaji wa dini za asili, Ozo Ozormba Okonkwo, anasema kitendo cha serikali kuzipa nafasi dini ngeni huku dini za asili zikitengwa hakikubaliki.

"Kwa sababu hatupigi kelele au hatujiingizi kwenye siasa haina maana kuwa dini zetu hazipo au hazina maana. Sala zetu zimeisaidia Nigeria kufikia hapa ilipo", alisema Okonkwo.

Kabla ya ujio wa wakoloni waafrika walikuwa na mifumo ya kiutawala, mila, jadi, utamaduni, utawala wa kijadi vilivyowaunganisha na kuwa wamoja. Waafrika wamesambaratika kutokana na nguvu za wageni walioleta mifumo yao ya maisha, iliyoonekana ‘bora zaidi', ingawa baadhi ya mila zilizobagua baadhi ya watu kwa ujinga ziliongeza kasi ya mparaganyiko.

Bunge la Katiba litakuwa kielelezo cha mparaganyiko wetu, ambapo tutaona mitazamo mikali, inayokinzana, itakayoacha ukijiuliza je, hili ni Taifa moja? Ama kweli sisi tunajenga Taifa moja? Kutakuwa na hoja ngumu za kidini na za kisiasa, baadhi tayari tunazijua na nyingine tutazisikia hukohuko. Na kama alivyoonya Rais Kikwete, akihutubia viongozi wa vyama vya siasa Februari 7, Katiba inaweza isipatikane.

Shida ya Watanzania ni kwamba wamefikia hatua ya kuchukiana na kutakiana mabaya kwa sababu ya tofauti za kidini na kisiasa, na kufuata falsafa ya Mao Tse Tung, ambayo hata Rais Kikwete aliinukuu: "Tutaunga mkono kila ambacho adui anapinga na kupinga kila ambacho adui anaunga mkono". Kwa hiyo basi, tutaishia kupinga hoja kwa sababu itamnufaisha adui (ambaye kiuhalisia ni ndugu yako Mtanzania) hata kama wewe hupati hasara yoyote hoja hiyo ikipita.

Na tayari hoja za kuonyesha jinsi utaifa wa Tanzania ulivyosagika zimenza kusikika baada tu ya majina ya wabunge wateule kutangazwa. Kuna mtu aliandika katika ukurasa wa mtandao fulani, "Orodha haiko sawa upande wa bara ..haiwezekani wakristo wawe asilimia 90%, hapa waislamu wasitarajie jipya la manufaa . Tusubiri kura ya maoni , kama hamna mahakama ya kadhi bora isipite".

Mwingine akaandika "Dah kweli hapa hakuna katiba mpya, yaani ni masheikh na ma-CCM yamejaaa. Ndiyo naanza kuwaelewa waliokuwa wanapinga Rais kuteua majina", akiungwa mkono na mwingine aliyeandika "maprofesa wa madrasa wanawaza ubwabwa tu hawana jipya..." na mwingine akaongeza "… ukiangalia hayo majina wamejaa wakina Abdala, Ahmadi, Moh'd, Yusuf, Asha....hapa kuna makusudi imefanyika kwa mkakati maalumu".

Tukirudi katika uteuzi wa Rais, je, Watanzania tumekumbuka kujumuisha katika Bunge hili makundi madogo (kama ya dini za asili kule Nigeria) ambayo huenda kusahauliwa kwao ni kwa ajili ya uchache au udhaifu wao? Nimesoma gazeti likinukuu viongozi wa Chama cha Viziwi (CHAVITA) wakilalamika.

Je, mchakato wa uteuzi huu umefanyika kiweledi na kuzingatia maslahi ya Taifa – kuanzia katika kupendekeza majina hadi katika kuyachuja? Na tatu, Serikali ya CCM ambayo Mwenyekiti wake ndiye mamlaka ya uteuzi, haikutumia nafasi hii kujinufaisha kwa kuhandisi mapendekezo ya watu fulani ili awateue?

Katika mchakato wa namna hii, ni rahisi kusema makundi yamewakilishwa – maana tunaona majina yanayonasibishwa na taasisi za kiraia, wakulima, wavuvi, wasomi, wafanyakazi, lakini picha hii ya juu juu ya uwakilishi ‘mpana' inaweza kuwa imeficha uongo kwa sababu huu ni uwakilishi unaotokana na taasisi za makundi hayo. Uzoefu unaonyesha mara nyingi hutokea taasisi hizo kuendeshwa na wasomi waishio mijini, wasiojua changamoto za kundi husika kiundani na matokeo yake unakuwa na Bunge la Katiba la kimjini na kisomi (elites).

Kadhalika, katika mijadala mbalimbali, baadhi ya wanaharakati mbalimbali wameonyesha wasiwasi kuwa wengi kati ya walioteuliwa na Rais ni aidha wanachama wa CCM au washabiki au watu wenye milengo ya CCM au wana fadhila za kuilipa CCM. Sina uhakika wa ukweli wa madai hayo, ingawa binafsi naamini Rais angeweza kupunguza malalamiko ya namna hii kama angeteua watu wanaoakisi zaidi sifa za kundi husika.

Hoja hii inanipeleka kwa Kingunge Ngombale Mwiru na wanasiasa wengine waliopo katika kundi kwa mfano la taasisi za kiraia. Hakuna mtu makini atakayebisha kuwa Kingunge ni mmoja kati ya watu makini sana ambao wanaweza kusaidia mijadala kwa elimu, uzoefu na busara zao. Lakini watu wengi wameuliza anawakilisha taasisi gani ya kiraia, swali lililozaa majibu mengi, ikiwemo kauli za utani kwamba eti Ngombale ni taasisi inayojitegemea na kuthibitisha hilo angalia jina lake NGOmbale – lina NGO.

Utani pembeni, wote tunamjua Kingunge kama mwanasiasa wa muda mrefu, na kama yuko katika taasisi za kiraia aidha ameingia baadaye (huenda baada ya kustaafu) au kama alikuwapo basi, ilikuwa ziada, baada ya siasa. Je, Rais ameshindwa kabisa kupata watu miongoni mwa waliopendekezwa ambao wamekuwa katika taasisi za kiraia sehemu kubwa ya maisha yao, na hivyo kuwa na uwezekano wa uelewa mkubwa zaidi wa ajenda za taasisi za kiraia?

Rais angeteua watu ambao jamii inawajua kuwa ni wanaharakati wa taasisi za kiraia, (kadhalika katika makundi mengine) hata kama wangekuwa wenye mitazamo ya CCM, angeepusha lawama nyingi, kuliko sasa ambapo aliowateua sio tu, uana harakati wao katika taasisi hizi unatia shaka, lakini U-CCM wao upo, si jambo la kuuliza.

Uteuzi wa Kingunge ni kielelezo tu cha tatizo. Ukweli ni kuwa kuna wateuliwa kadhaa ambao huenda si wawakilishi sahihi sana wa makundi wanayowakilisha, ukilinganisha na wengine walioachwa ambao bahati mbaya hatuwajui na huenda hatutawajua milele.

Katika hali hii, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alikuwa na haki ya kulalamika aliposema: "Tunashangaa kuona watu walioteuliwa wengi ni wanasiasa. Tulitarajia wengetoka nje ya vyama vya siasa, lakini ndiyo Rais kaamua."

Nionavyo, labda tulikosea tangu mwanzo pale sheria ilipompa madaraka Rais kuteua wajumbe miongoni mwa waliopendekezwa, bila vigezo vilivyowazi na huenda hata bila kulazimika kuweka hadharani majina yote ya waliopendekezwa na huenda hata bila kulazimika kueleza kwa nini amemteua huyu na kwa nini hakumteua yule? Sheria ile ilitoa njia ya kufisidi kisiasa. Sheria nzuri katika siasa za ushindani haipaswi kutoa nafasi kwa mamlaka kufisidi kirahisi namna hii, bila kuvunja sheria. Katika mapendekezo, Rais atashindwaje kupata vitaasisi vya kumpendekezea anaowataka ili waingie?

Hata hivyo, Watanzania tujue kuwa Bunge la Katiba ni mchezo wa namba na hivyo labda ili Katiba ipatikane, Rais kwa busara zake akaamua tu badala ya kupoteza fedha nyingi na kuishia katika mkwamo kwa kila kundi kukosa wingi, ni bora tu atengeneze wingi ili mambo yaende.

Labda pia Rais aliamua kuhakikisha uwiano wa nguvu wa vyama uliokuwapo tayari bungeni haubadiliki ili chama kikubwa kiendelee kuwa na faida dhidi ya wengine. Ni mchezo wa namba.

Hata hivyo, natumai mchezo huu wa namba hautotumika kupindua matakwa ya wengi hususan katika hoja nyeti ya mfumo wa Muungano kwani hiyo ni sawa na kuahirisha matatizo.

Nawashauri Watanzania tusahau yaliyopita tugange yajayo kwani sijawahi kusikia Rais akibadili msimamo kwa mambo kama haya ya uteuzi. Tuombee tu kuwa wajumbe walioteuliwa, watatuwakilisha vizuri, watatoa hoja na si vioja.

Source: Raia mwema
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…