JK kaomboleza pia...
JK amlilia Amina Chifupa
Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete, ameeleza kupokea kwa mshituko mkubwa taarifa ya kifo mbunge wa CCM Viti Maalum, Amina Chifupa.
Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari, ilisema kifo hicho kimetokea wakati usiotarajiwa, huku akihitajika, lakini vivyo hivyo alikuwa ameanza kuvuma kisiasa.
"Wengi tutamkubuka marehemu Amina Chifupa kwa mchango wake muhimu alioutoa bungeni na katika jamii hasa mongoni mwa vijana.
"Alikuwa hodari katika kujkenga hoja na kutetea maslahi ya vijana wenzake na taifa kwa ujumla. Alikuwa kijana msema kweli na jasiri katika kutoa maoni yake kwa jambo analoliona," alisema Rais Kikwete.
Huku akinukuu misemo mbalimbali ya kijamii, Rais Kikwete alieleza kusikitishwa kwake na kifo cha mbunge huyo katika umri wa ujana wake.
"Kwa hakika kifo chake kinawagusa na kuwasikitisha watu wengi nchini. Wabunge wamempoteza mbunge mwenzao kipenzi, CCM wamempoteza nyota yao.
"Familia yake imempoteza nyota yao. Familia yake imempoteza mtoto na ndugu wa karibu. Mwanawe amempoteza mama.
"Mzazi mwenzake amempoteza mzazi mwenziwe wa kusaidiana naye kulea mtoto wao mdogo. Jamii imempoteza mwana jamii mwema, mkarimu na mwenye moyo wa huruma," alisema Rais Kikwete.
Aliwahakikishia jamaa za karibu wa marehemu, huzuni hiyo haikuwa peke yao, bali ni ya wote wanaoguswa na kifo hicho, huku akisisitiza ni "Mapenzi ya Mungu."
Katika hatua nyingine, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), umetoa rambirambi kutokana na kifo hicho cha Amina.
Rambirambi za UVCCM zilizotolewa katika taarifa iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa Taifa, John Nchimbi, zilisema hawataweza kumsahau kutokana na uwakilishi wake hasa wa kutetea maslahi ya vijana nchini wakati wote.
"Amina alikuwa ni mchapakazi hodari, mkweli na ambaye siku zote alitetea masuala ya vijana, sifa ambayo ilimfanya apendwe na wengi," ilisema taarifa hiyo.
Nchimbi katika taarifa yake, alibainisha kwamba wakati wote wataendelea kukumbuka kwa utashi aliokuwa nao katika utumishi wa uwakilishi wa jamii katika chombo hicho cha kutunga sheria.
"Tunaungana na wabunge, familia, ndugu na jamaa za Amina Chifupa, kuomboleza kifo chake na tunamwomba Mwenyezi Mungu awape uvumilivu, nguvu na afya katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo," ilihitimisha taarifa hiyo.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema chama hicho na yeye binafsi wameshitushwa na kifo cha Amina.
Walimsifu marehemu kama mtetezi wa jamii ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo Watanzania wamempoteza kiongozi shupavu.
"CUF - tunatoa pole kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete, Spika Samuel Sitta, wabunge, ndugu na jamaa wa marehemu na tunaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, ilisema taarifa ya CUF, iliyotiwa saini na msemaji Mbaralah Maharagande.
Naye Mwadini Hassan, anaripoti kutoka Dodoma kuwa, Chama cha Mapinduzi kimesema kimepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Mbunge wa Viti Maalum, Amina Chifupa, na kusema namna ya kumuenzi ni kutetea na kuyasimamia yote aliyokuwa akiyatetea.
Kauli hiyo ya CCM ilitolewa hapa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, makao makuu ya chama.
Alisema, marehemu Amina alikuwa kiongozi imara katika kutetea hoja, na hasa kupambana na dawa za kulevya, ambapo alidiriki kueleza hadharani kuwa "hata kama ni mumewe au yeye mwenyewe anajihusisha na biashara ya dawa hizo, watajwe ili wafikishwe katika vyombo vya sheria."
Makamba alisema, Amina alichukia biashara ya dawa za kulevya, ambayo imekuwa chanzo cha kuwaharibu vijana wengi nchini, ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa.
Makamba alitaja eneo jingine ambalo marehemu alilisimamia imara kulitetea, ni la watoto wa mitaani na wanaoishi katika maisha magumu, ambapo licha ya yeye kujitolea kwa hali na mali kupambana na tatizo hilo, alikuwa mara kwa mara akiitaka serikali kuchukua hatua madhubuti kuwasaidia kwa kuwapatia makazi ili waondokane na hali zao.
Marehemu Amina alisema Makamba, aliwahi kulia alipowatembelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hali ambayo ilionyesha alikuwa akiumizwa na hali hiyo na aliahidi kujitahidi kuwasaidia.
"Namna nzuri ya kumuezi, ni kuyaendeleza aliyokuwa akiyasimamia na kuyatetea, na hasa kwa Umoja wa Vijana ambao alikuwa akiuwakilisha bungeni," alisema.
Source: UHURU
Hilo jina ni sahihi kwa mwenye cheo hicho? au wamekosea?