Kifo cha Amina ni kurogwa, kisukari-Chifupa
*Asema alichanganyikiwa na kutaja majina ya viongozi
*Adai alimtokea bibi yake ndotoni siku ya 3 ya maziko
Beatrice Moses na Gladness Mboma
BABA mzazi wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, marehemu Amina Chifupa, Bw. Hamisi Chifupa, amesema kifo cha bintiye kilichangiwa na magonjwa ya 'kiswahili' na kisukari.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO, Bw. Chifupa alisema hali ya mtoto wake ilianza kuwa mbaya kiasi cha kufikia kutaja majina ya baadhi ya viongozi wa Serikali kwa maneno makali.
Akifafanua, alisema hali hiyo ilianza Mei 6 mwaka huu, baada ya mtoto wake kuahirisha ziara ya Mtwara ghafla akiwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu J.K. Nyerere, Dar es Salaam. Magonjwa ya 'kiswahili' yanamaanisha kurogwa.
"Mimi na mdogo wake ndio tulimsindikiza hadi uwanja wa ndege ambako alikutana na Waziri Mwandosya (Profesa Mark) wakasalimiana, kisha akaanza maandalizi ya kupanda ndege, lakini ghafla alimwita mhudumu na kuahirisha safari, tukatoka na kurejea nyumbani Mikocheni," alisema Bw. Chifupa.
Alisema baada ya kurejea nyumbani, hali ya bintiye ilibadilika ambapo alianza kutaja majina ya viongozi wa Serikali kwamba ndio waliomsababishia kuugua kwake, hapo ndipo familia ikaanza kuhisi kuwa alikuwa na tatizo kubwa hivyo wakamwita daktari.
"Baada ya hapo hali haikuwa nzuri, tulijua hayo yalikuwa mambo ya 'kiswahili', ndipo tulipoamua kumtibia pia 'kiswahili', Amina alikuwa hali katika kipindi chake chote cha kuugua," alisema Bw. Chifupa.
Hata hivyo, maelezo ya baba huyo yalionekana kuwachanganya waandishi wengi waliokuwa wakimsikiliza kwenye mkutano huo, baada ya yeye kukiri, kwamba alikataa mtoto wake kutibiwa nje ya nchi, kwa madai kuwa ana ugonjwa wa 'kiswahili', lakini pia alisema alipopelekwa hospitalini na kupimwa, alibainika kuwa na kisukari kilichofikia 400 na homa kali.
Alisema kisukari kiligundulika wenye hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, baada ya kuahidiwa ulinzi mkali, kwa kuwa baadhi ya magazeti nayo yalikuwa yakiwachangaya sana, ingawa baadhi yalikuwa yakiwasaidia.
"Baada ya kueleza, vipimo vingi vilifanyika na kugundulika vilikuwa vizuri, lakini sukari ilikuwa haishuki na homa ambayo ilitutia shaka sana, kwa kuwa kila ikipimwa, ilikuwa pale pale au kupanda," alisema Bw. Chifupa.
Alisema wakati Amina akiwa hospitalini hapo, alikuwa akizungumza maneno ya ajabu na mazito yakiashiria kifo chake, hatimaye alifariki dunia Juni 26 mwaka huu saa 2.45 usiku, wakati akipata matibabu ya Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Brigedia Jenerali Salim, madakatari wengine na wauguzi.
Katika hali ya kushangaza, Bw. Chifupa alisema siku tatu baada ya maziko, Amina alituma salamu zake kwa ndoto kupitia kwa bibi yake mdogo aitwaye Tulaonana Mnyalape, ambaye alimhoji yupo wapi.
"Kwa kuwa alikuwa akimtafuta, naye akasema kuwa kwa sasa yuko kwa Mungu na hakutaka kwenda huko mapema ila binadamu ndio waliompeleka huko, ilhali wakati wake ulikuwa bado, pia alimweleza bibi yake mzaa mama, kuwa amekwenda kijijini hapo kuishi naye," alisema.
Bw. Chifupa aliwataka ndugu jamaa na marafiki wa Amina, kuacha kuhuzunika kwa kuwa tayari imebainika kuwa hajafanywa msukule wala ndondocha.
Alisema anawashukuru viongozi wote walioguswa na msiba huo, kwa kuwa inawezekana wapo ambao alisema wamefurahia sana hasa wanaojihusisha na dawa za kulevya au ambao walikuwa wakichukia jinsi Amina alivyokuwa akichipukia haraka kisiasa.
Bw. Chifupa alisema familia yake inatambua kuwa watu wengi wamekihusisha kifo cha binti yao na dawa za kulevya na kama ni kweli, basi wanaona vita hiyo haijamalizika na badala yake imetiwa petroli.
"Ombi letu kwa Serikali, ikiwa yupo kiongozi au mwananchi ametajwa katika vita hii, awekwe bayana hata akiwa ni mmoja wa wanafamilia yetu atajwe au akiwa ni mbunge au mjumbe wa NEC atajwe tu," alisema Mzee Chifupa.
Alisema Serikali isiwe na kigugumizi kwa hilo, kama viongozi au wahusika wanaharibu Taifa wasiachwe na fununu zenye ukweli zisizo majungu zifanyiwe kazi, kama wanaotajwa moja kwa moja kuwa wanauza unga wakamatwe.
Bw. Chifupa alisema watamuenzi Amina kwa kuwa amekufa Siku ya Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya duniani, ambapo familia yao imeanzisha Mfuko unaoitwa Amina Foundation ambao utatumika kuendeleza aliyoyaacha, ikiwa ni pamoja na gari lake ambalo litatumika kwa ajili ya Mfuko huo.
Alisema hata kama kuna ahadi aliyoitoa ya msaada kwa watu au taasisi lakini akakosa nafasi ya kuitekeleza, basi Mfuko huo utafanya hivyo.