Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
BURIANI ASAYYID SHARIF HUSSEIN AHMAD BADAWIY
Shariff Hussein Badawiy kaacha athari kubwa sana Dar es Salaam katika usomeshaji wa Qur'an Msikiti wa Badawiy (sasa Rawdha) hadi pale alipofukuzwa Tanganyika mwaka wa 1963 yeye na mdogo wake Mwinyibaba.
Masjid Badawiy ilisifika sana kwa kutoa wasomaji bingwa wa tajwid.
Nilibahatika siku moja kuzungumza na Shariff Hussein jirani ya msikiti wa Ibadh nilipomkuta kasimama nje na mtu mmoja.
Huyu bwana alikuwa rafiki yangu Sheikh Mtangala maarufu kwa jina la Kawawa.
Nilikwenda pale kumwamkia kisha nishike hamasini zangu lakini Sheikh Mtangala aliyekuwa anazungumzanae akanizuia nisiondoke ili nisikilize mazungumzo yao.
Nilibakia. Nilifaidika sana siku ile kwani nilimsikia mwenyewe akieleza mengi aliyoona wakati ule na pigo alilopata kwa kufukuzwa Tanganyika.
Msikiti wa Badawiy palikuwa na moja ya darsa kubwa mjini Dar es Salaam ambako Mufti Sheikh Hassan bin Ameir alikokuwa akisomesha tafsir ya Qur'an.
Darsa hii ilikuwa inajaza msikiti na wanafunzi wake walikuwa masheikh wakubwa wa nyakati zile.
August Nimtz aliyeandika kitabu maarufu, ''Islam and Politics in East Africa The Sufi Order in Tanzania'' (1980) ameitaja hii madrasa katika kitabu chake.
Mwanafunzi wa mwisho naamini kufariki katika kundi hili la masheikh wa wakati ule ni Shariff Adnan ambae alibaki pale msikitini kama Imam Mkuu hadi kifo chake miaka michache iliyopita.
Nimepata kumpiga picha Shariff Hussein Lamu na Dar es Salaam baada ya yeye kurejea.
In Shaa Allah nitaziweka hapa baadhi kwani picha inasema maneno elfu moja.
Shariff Hussein baada ya kurejea Tanzania katika miaka ya 1980 alifungua madrasa Lushoto na akaanza kusomesha upya.
Allah amfanyie wepesi safari yake.
Angalia picha: