Buriani Bi. Zainab Sykes, mhifadhi wa hazina ya nyaraka za historia ya kupigania huru wa Tanganyika baada ya kupata taarifa ya msiba wa mama yangu

Buriani Bi. Zainab Sykes, mhifadhi wa hazina ya nyaraka za historia ya kupigania huru wa Tanganyika baada ya kupata taarifa ya msiba wa mama yangu

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
BURIANI BI. ZAINAB SYKES
MUHIFADHI WA HAZINA YA NYARAKA ZA HISTORIA YA KUPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA

Baada ya kupata taarifa ya msiba wa mama yangu Bi. Zainab Sykes baada ya mshtuko kupita niliinamisha kichwa nikarejea utotoni na nikajaribu kukumbuka mama zangu ambao kwa hakika nilikuwa na kumbukumbu zisizo shaka kwa maana ya kuwakumbuka waziwazi kwa sura, vitendo na kwa majina.

Wengi katika hawa walikuwa majirani pale Mtaa wa Kipata nilipozaliwa na wengine wakija nyumbani kwetu na hapo ndipo nilipokuwa nasikia majina yao yakitajwa.

Katika hawa wachache nilikuja kuwajua vizuri nikiwa nina akiili zangu ingawa bado mdogo sijafika hata miaka kumi.

Namkumbuka Mama Nambaya na mwanae Nambaya, dada yangu akinibeba wakati mwingine na kuzunguka na mimi mtaani hadi dukani kona ya Kipata na Swahili nyumbani kwa Mama Kilindi mmoja wa mashoga wa mama yangu.

Nambaya alikuwa mlemavu wa ngozi na alikuwa na kaka yake akiitwa Shabaka.

Nina kumbukumbu ya ajali aliyopata Shabaka akiwa
mdogo na akapoteza jicho moja.

Shabaka hadi anafariki miaka michache iliyopita alibakia kaka yangu na alikuwa na mapenzi makuwa sana na mimi.

Huyu Kilindi wa Mama Kilindi ni dada yangu na yeye pia akinibeba.

Mtoto wa Bi. Kilindi, Bwana Amani, jina la utani ‘’Scuba,’’ nilikuja kumjua baada ya takriban miaka 50 kwa bahati tu katika kukutananae mara nyingi msikitini na siku moja katika mazungumzo nikamuuliza kuhusu wazazi wake.

Nilipata mshtuko wa aina yake nikamueleza udugu uliokuwapo baina ya mama yake na mimi miaka mingi iliyopita.

Machozi yalinidondoka.

Dada yangu Kilindi mwanae Scuba alinifahamisha alikuwa amefariki si miaka mingi iliyopita na siku chache tukiwa mazikoni Makaburi ya Mwinyi Mkuu Scuba alinionyesha upande lilipo kaburi la Bi. Kilindi.

Wajukuu wanne wa dada yangu Bi. Kilindi ni kati ya marafiki zangu na wakienda madrasa au wanatoka au wakiniona msikiti lazima watakuja kunisalimia babu yao.

Mama Kilindi na Mama Nambaya hawa walikuwa majirani na mashoga wakubwa wa mama yangu na huu udugu uliendelea hata pale mama alipofariki na mimi kuondoka Mtaa wa Kipata.

‘’Dada Sikitiko.’’

Hivi ndivyo nilivyokuwa nikisikia mama yangu akimwita huyu Bi. Mkubwa na kwa hakika wakati ule hawa wote ninaowataja walikuwa wasichana hawajazidi miaka 30.

Bi. Sikitiko ni mama yake Kesi Mohamed, maarufu kwa jina la Kesi Mjinga.

Kesi Mjinga alikuwa kijana maarufu Dar es Salaam.

Bi. Sikitiko alikuwa shoga kipenzi cha mama yangu na kutokana na kumsikia hata mama yangu mkubwa Bi. Mwanaisha akimwita Dada Sikitiko nimejua kuwa alikuwa amewazidi umri mama zangu wote.

Kulikuwa na Mwalimu Blandina.

Mwalimu Blandina alikuwa mwalimu Kitchwele Girls School.

Namkumbuka sana Mwalimu Blandina.

Siku moja niko Maktaba ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam nikaona picha yake katika moja ya magazeti ya zamani.

Biti Hassan Machakaomo mwanamke wa Kizulu binti ya Hassan Machakomo.

Biti Hassan hana chembe ya athari ya Uzulu aliishi na kufa akiwa kama Mzaramo.

Huyu Machakaomo aliingia Tanganyika akiwa askari mamluki katika jeshi la Wazulu pamoja na Sykes Mbuwane chini ya Hermann Von Wissman.

Nilikutana na Biti Hassan mimi sasa mtu mzima na ikasadifu kuwa nimeoa mtoto wa shoga yake mama yangu Biti Simba.

Biti Hassan na dada yake hawakuhama Kipata waliishi nyumba ile ile waliyozaliwa na nilipojitambulisha akawa ananiambia, ‘’Mohamed wewe umezaliwa pale mwanangu,’’ huku akionyesha kidole nyumba niliyozaliwa lakini nyumba ile haikuwapo badala yake kuna ghorofa na nyumba ya mbele ya Mama Nambaya halikadhalika ni gorofa.

Kipata ya miaka ya 1950 ilikuwa imetoweka.

Biti Saburi.

Picha inayonijia ya mama huyu ni zile shanga nyingi alizokuwa akivaa mikononi.

Ukivuka Mtaa wa Sikukuu kwenda mbele kulikuwa na Biti Salum.

Nyumba yake inatazamana na Msikiti wa Kipata.

Hawa wote mama zangu na nimeishi katika wakati wao na hawa wote ni katika uzawa wa Mama Sykes.

Wengine nimewadiriki na kuishinao kwa miaka mingi hadi wakatangulia mbele ya haki na wengine nimesikia historia zao.

Nimeinama kwa majonzi baada ya taarifa ya kifo cha Mama Sykes, nimekwenda nyuma safari ndefu ya miaka yapata 60.

Mama Sykes yeye na mumewe Bwana Ally Sykes nyumba yao ilikuwa Kipata chini karibu na New Street.

Nilimuuliza siku moja Mama Sykes kuhusu mama yangu ambae alikufa akiwa katika umri mdogo sana.

Mama Sykes akanambia, ‘’Mama yako alikuwa ule upande wa juu wa Kipata.’’

Nilipokutana na Biti Hassan Machakaomo alinambia kuwa ni miaka mingi hajamuona Mama Sykes lakini Bwana Ally anapita mara kwa mara nyumbani kwake kila anapokuja Gerezani.

Pale tulipokuwa tumesimama tuliweza kuiona nyumba ya Mama Sykes aliyoshi na mumewe Bwana Ally Sykes katika miaka ya 1950 kwa kuwa sasa ni nyumba ya gorofa ndefu ile nyumba yenyewe ya asili sasa haipo.

Hii nyumba imebeba historia kubwa ya mapambano ya Mwafrika dhidi ya ukoloni.

Hii nyumba ndiyo akiishi Kleist Sykes kuanzia miaka ya mwanzoni 1900 na Mama Sykes aliishi hapo toka alipoolewa na Bwana Ally miaka ya mwanzoni 1950.

Hii ndiyo ilikuwa nyumba ya familia ya Sykes ingawa baadae zilijengwa nyumba kadhaa katika mitaa ya jirani New Street (Lumumba Avenue), Kirk Street (Lindi Street) na Stanley Street (Aggrey).

Hii mitaa yote hivi sasa imebadilishwa majina na kupewa majina ya wazalendo wana Dar es Salaam waliopigania uhuru wa Tanganyika.

Mama Sykes ni mmoja wa akina mama waliomfahamu Julius Nyerere siku za mwanzo alipofika Dar es Salaam.

Mama Sykes amenihadithia visa viwili muhimu sana katika historia ya harakati za kudai uhuru.

Kisa cha kwanza ni siku nyumba yake pale Mtaa wa Kipata ilipovamiwa na askari wakitafuta mashine iliyokuwa ikitumika katika kudurufu makaratasi ya ‘’uchochezi,’’ ambayo Special Branch walikuwa na taarifa kuwa kazi ile akifanya Ally Sykes na hiyo mashine iko nyumbani kwake.

Mama Sykes akiwa ndani mlango ulibishwa hodi na alipokwenda kuachugulia nje (kwani milango yote ilikuwa ikifungwa wakati Ally Sykes akichapa yale makaratasi), Mama Sykes akamuona Amri Kweyamba kachero wa Special Branch amesimama na askari anasubiri kufunguliwa mlango.

Haraka alirudi ndani kumpa taarifa mumewe kuwa kuna askari nje.

Ilimchukua Bwana Ally muda mfupi sana kukusanya yale makaratasi na wino kutumbukiza chooni uani na mashine kurushwa ua kwa ua na ikapotelea kusikojulikana.

Alipofunguliwa mlango Amri Kweyamba hakukuta kitu ndani ila Ally Sykes na mkewe wanamtazama.

Kisa cha pili alichonihadithia ni siku Nyerere alipokwenda nyumbani kwake kutoa taarifa ya kuisajili TANU.

Hii ilikuwa baada ya TANU kuasisiwa katika mkutano wa mwaka wa TAA tarehe 7 Julai 1954.

Hii ndiyo siku ilipoundwa TANU.

Abdul na Ally Sykes na Julius Nyerere walikuwa wamekubaliana kuwa Nyerere akitoka kwa Msajili kuisajili TANU wakutane nyumbani kwa Ally Sykes Mtaa wa Kipata.

Mama Sykes anasema Nyerere alipofika alikuwa kalowa sana akaeleza kuwa Msajili amekataa kuisajili TANU kwa kuwa haina kitabu cha rejesta kinachoonyesha majina ya wanachama.

Abdul Sykes palepale aliagiza Mzee Said Chamwenyewe atafutwe ili ampe maelekezo ya kwenda Rufiji na rejesta na kadi za TANU kutafuta wanachama wa mwanzo wa TANU.

Katika orodha ya mama zangu niliowadiriki hadi leo Mama Sykes naamini ni mmoja katika kundi la mwisho katika huu uzawa wa akina mama walioshuhudia harakati za uhuru.

Waliobaki kwa ufahamu wangu ni akina mama wanne – Mama Ali aliyekuwa mke wa Aziz Ali baba yake Dossa Aziz, Bi. Maunda Plantan, Bi. Flora Mgone na Mama Maria Nyerere.

Akina mama hawa wameona kila kitu katika historia ya uhuru kwa macho yao.

Laiti akina mama mama hawa wangelinyanyua kalamu na kuandika yale waliyoshuhudia miaka ya 1950 wakati baba zetu hapa Dar es Salaam wanaanza harakati za TANU kudai uhuru wangetuachia hazina kubwa ya historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika isiyo na kifani.

Hata hivyo mama zetu hawa wamezungumza kwa kiasi chao na tumeyajua mengi kutoka kwenye vinywa vyao.

Mama Sykes ndiye aliyehifadhi nyaraka za familia ambazo mimi nashukuru kuwa nyingi nimezisoma wakati natafiti kitabu cha maisha ya Abdul Sykes.

Nyaraka hizi naamini ndiyo nyaraka pekee zilizobakia mikononi mwa watu binafsi zinazoeleza historia ya kudai uhuru wa nchi yetu na kwa njia ya pekee nyaraka hizi zinaeleza pia historia ya Julius Nyerere na uhusiano wake na ukoo huu katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Itapendeza sana sasa kwa familia hii kufikiria kwa heshima ya mama yetu huyu angalau kuwa na maktaba ndogo itakayohifadhi kumbukumbu hii na ile hazina kubwa ya picha iliyopo inayofungamana na historia ya Tanganyika na historia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwenyezi Mungu tunakuomba mfanyie wepesi mama yetu katika safari yake hii.

Amin.

1613024283000.png
 
Kessy Mjinga, nafikiri kati ya watoto wake yupo mmoja anaitwa Yusuph pamoja na dada zake.
 
Innalillah

Kinachiniskitisha ni kukosekana mtu wa kuwahoji na kuandika mengi yasiyo kwenye vitabu

Jitu linapata fursa ya kuonana na kumhoji Mama Maria Nyerere linamuuliza mambo ya Kasi sijui ya awamu ya Tano sijui Uchumi wa Kati… Kizazi cha Kina Mama Maria kikipotea tujiandae na historia ya Kina Ndalichako
 
Asante kwa ujumbe mzito kweli kama wanavyosema Waingereza it is the end of an era. Maneno yako ni ya mitaani, sote tumekulia mitaani, majirani wote ni mama "zetu", naomba usiyakuze mno ingawa ni muhimu. Aidha, nakuomba usiwe mnyooonge, umedhoofu kana kwamba ni mwisho wa dunia. Kuna mama zako wanne umewataja kwa majina bado wapo hai, si uwafuate? Leo umemtaja Mama Maria Nyerere kwa mara ya kwanza kabisa, kimekugusa nini?
 
Asante kwa ujumbe mzito kweli kama wanavyosema Waingereza it is the end of an era. Maneno yako ni ya mitaani, sote tumekulia mitaani, majirani wote ni mama "zetu", naomba usiyakuze mno ingawa ni muhimu. Aidha, nakuomba usiwe mnyooonge, umedhoofu kana kwamba ni mwisho wa dunia. Kuna mama zako wanne umewataja kwa majina bado wapo hai, si uwafuate? Leo umemtaja Mama Maria Nyerere kwa mara ya kwanza kabisa, kimekugusa nini?
LGF,
Maneno yangu si ya mitaani wala sijayakuza kama unavyodhani.

Nimeandika kama ninavyokumbuka nikiwa na umri wa mtoto mdogo.

Nikufahamishe vilevile kuwa nilikuwa na wake zangu pia.

Unasema na wewe umekulia mjini inawezekana lakini utamaduni uliokulia wewe tofauti na wangu kwa mbali sana.

Ndiyo nimekuongezea kuwa nilikuwa na wake zangu pia - Biti Rajabu na Biti Mwakaruzo.

Hawa ni mama wa mama zangu kwa utamaduni wetu hawa sasa mimi kama mjukuu ni mume wao.

Naamini umeelewa.

Si kweli kuwa ndiyo leo namtaja Mama Maria kwa mara ya kwanza.

Mama Maria huwa namtaja kila nihadithiapo historia ya TANU na bibi zangu kama Mama Sakina, Mama Daisy, Hawa bint Maftah, Tatu bint Mzee na Bi. Titi Mohamed kwa kuwataja wachache.

Hawa ndiyo akina mama wanachama wa mwanzo wa TANU waliompokea Mama Maria Dar es Salaam.

Kuna kisa nimemtaja Mama Maria kipo hapa jamvini.

Ni mkasa kuhusu Mwalimu ilipodhaniwa kalishwa sumu kwenye chakula nyumbani kwa Abdul Sykes.

Katika mkasa huu Bi. Nyang'ombe Mugaya, mama yake Nyerere alikuwapo.

Kuna historia ya duka la mafuta ya taa ambalo Mama Maria alifungua Mtaa wa Mkunguni na Livingstone jirani na nyumba ya Mama Sakina.

Duka hili baadae Mama Maria akalihamishia nyumbani kwa Ali Msham ilipokuwa tawi la TANU la kwanza Mtaa wa Jaribu, Magomeni Mapipa.

Ukiwa unataka kusoma historia hizi za Mama Maria katika harakati nifahamishe In Shaa Allah nitaviweka hapa upya.

Unaniomba nisiwe mnyonge.

Waislam sheria yetu msiba ni siku tatu baada ya hapo maisha yanaendelea.

Ndipo nimekueleza kuwa lau kama na wewe ni mwanamji kama mimi tofauti baina yetu ni sawa na mbingu na ardhi.

Hakuna popote tutakaposhabihiana.
Nakupa pa kuanzia.

Soma bandiko lako lililopita angalia lugha yako.

Na hii ni changamoto nawapa wasomaji wengine watusome na kwengine.

Hawa bila shaka watakuwa na neno la kusema.
 
Maalim Said sisi tulio wengi tunakufaidi sana tusomapo simulizi zako zilizojaa hazina ya historia. Hao pimbi wachache Wala usihangaike kuwajibu
 
Innalillah

Kinachiniskitisha ni kukosekana mtu wa kuwahoji na kuandika mengi yasiyo kwenye vitabu

Jitu linapata fursa ya kuonana na kumhoji Mama Maria Nyerere linamuuliza mambo ya Kasi sijui ya awamu ya Tano sijui Uchumi wa Kati… Kizazi cha Kina Mama Maria kikipotea tujiandae na historia ya Kina Ndalichako
Teuzi kaka teuziiiiiiiiiiiiii zinawatoa watu ufahamu
 
Naomba ugusie kidogo na ile nyumba ambayo TANU iliundwa pale Mwananyamala A kwa Mwinjuma
 
Naomba ugusie kidogo na ile nyumba ambayo TANU iliundwa pale Mwananyamala A kwa Mwinjuma
Nyiluka,
Kama kuna nyumba ndani yake TANU iliundwa basi nyumba hiyo itakuwa ni nyumba ya Abdul Sykes iliyokuwa Mtaa wa Stanley na Aggrey Street.

Sijui ilikuwa je kikawekwa kibao kuwa TANU iliasisiwa nyumbani kwa Mzee Mwinjuma Mwinyikambi.

Katika nyumba hii ndipo Nyerere alipelekwa na JosephKasela Bantu kujulishwa kwa Abdul Sykes mwaka wa 1952.

Nyerere alipoacha kazi mwaka wa 1955 alikwenda kuishi nyumba hii na Abdul Sykes.
Mikutano yote ya TANU ilikuwa ikifanyika nyumbani kwa Abdul Sykes.

Bahati mbaya Abdul Sykes kafutwa katika historia ya TANU kama ilivyoandikwa na Chuo Cha CCM Kivukoni na nyumba ambayo Nyerere hakuwahi kuishi wala kulala ndiyo yenye kibao kuwa TANU humo ndimo ilipoasisiwa.

1615063974866.png
 
Back
Top Bottom