Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
BURIANI HASSAN MBASHIR
MWANAMJI MPENZI WA SUNDERLAND NA SIMBA
Hassan Mbashir katika uhai wake alikuwa mtu maarufu Dar es Salaam ile ambayo wengi wetu tulikulia.
Alikuwa mpenzi mkubwa wa Sunderland katika miaka ya 1960 hadi Simba miaka ya 1970.
Nimemkuta Hassan Mbashiri East African Cargo Handling Services (EACHS) akifanya kazi kama dereva wa ‘’staff car,’’ gari ndogo za kubeba mabosi kwani bandarini kulikuwa na kila aina ya madereva.
Kulikuwa na madereva wa crane, hapa namkumbuka marehemu Sarang Sab, mtu wa vituko sijapatapo kuona.
Wala hili Sarang si jina lake hiki ni cheo cha usimamizi wa kazi kwa makuli na hakuna aliyejua jina lake khasa ni nani labda rafiki yake kipenzi marehemu Ali “Yuri Gagarin’’ Ngwena.
Mtu mwingine aliyekuwa na kipaji cha ajabu kujibu maneno ambayo wewe huwezi kufikiria.
In Shaa Allah iko siku panapo majaliwa nitaandika historia za hawa ndugu zangu.
Tuendelee.
Kulikuwa na madereva wa forklift na hapa namkumbuka kaka na rafiki yangu, Athumani Kilambo na Abdulrahman Lukongo wote marehemu, wachezaji wa Yanga na timu ya taifa.
Namkumbuka Kilambo kwa ustaarabu wake na kipaji cha kuzungumza akiingiza maneno ya Kiingereza katika mazungumzo yake kiasi cha kushangaza ukichukulia kuwa hakupatapo kusoma elimu ya sekula hata siku moja.
Lukongo namkumbuka kwa kuvaa.
Alikuwa mchaguaji wa nguo za kupendeza na zikimkaa vyema. Kilambo na Lukongo wawili walikuwa marafiki wakubwa.
Kulikuwa na madereva wa malori. Bandari ilikuwa shirika kubwa sana na la kupendenza khasa katika miaka ile ya 1960 hadi 1970 kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Hassan Mbashir alikuwa dereva wa staff car.
Kama vile namuona katika uniform yake ya Kaunda suti imemkaa vyema na kiatu chake kimepigwa kiwi vizuri sana.
Unaweza ukapotea ukadhani yeye Mbashir ndiye bosi kumbe yeye ndiye anaemwendesha bosi.
Naikumbuka Vespa yake ambayo ilikuwa siku zote ipo katika hali ya kupendeza ikionekana mpya.
Lakini nimeikumbuka Vespa hii ya Mbashir si kwa hili bali kwa jingine.
Kulikuwa na mtu mmoja Cargo anaitwa Churchill sasa ni marehemu.
Jina lake halisi ni Mohamed Waziri.
Lakini kwa jina hili utamaliza mji mzima hutampata, jina lake maarufu lilikuwa Churchill.
Churchill akiipenda sana Yanga na ndiye aliyekuwa fundi mkubwa wa kutengeneza Vespa zote za vijana wa Dar es Salaam akina Hassan Mbashir na marehemu Mwinyiamiri Mwinyimadi mchezaji wa Yanga.
Mwinyiamiri alikuwa Cargo na mtoto wa Mzee Mwinyimadi mtu wa kujiweza enzi zake.
Turudi kwa Churchill.
Hakuna spea ya Vespa ambayo Churchill atakuwa hana.
Chini kunakwenda watu.
Unaweza kuandika kitabu kizima kuhusu Churchill.
Churchill alipatapo kukwaruzana na mtu aliyempa Vespa yake kutengeneza ikabidi waende mahakamani.
Mahakamani likaletwa pipa limejaa spea za Vespa kama ushahidi dhidi ya Churchill.
Hakimu akamuuliza Churchill. ‘’Wewe unasema katika maelezo yako kuwa unafanyakazi Cargo na kazi yako ni kuli sasa hili pipa la spea za Vespa imekuwaje limekutwa uani kwako?’’
Churchill akamjibu Hakimu akamwambia, ‘’Ninapotoka kazini mimi ni fundi wa Vespa.’’
Hakimu akatoa hukumu kuwa Churchill hana kosa na pipa lake la spea arudishiwe mara moja.
Hawa wote niliowataja wametangulia mbele ya haki mmoja baada ya mwingine na kwangu mimi walikuwa ni kaka zangu na Dar es Salaam ile sote tukijuana na kupendana sana.
Hassan Mbashiri katika kundi hili alijipambanua kwangu kwa namna ya kipekee.
Mbashir alikuwa mtu shujaa sana.
Zamani katika miaka ya 1970 mjini, Independence Avenue karibu na Maggot, ‘’night club,’’ maarufu miaka ile, kulikuwa na kibanda kinauza hamburger, wenyewe tukiita burger.
Siku hiyo imetokea nilikuwa mitaa ile na nikaenda pale nikikusudia kula humburger na cocacola.
Nikamkuta Mbashiri ameegesha Vespa yake pembeni kavaa msuli wa rangirangi za kuvutia na shati zuri la mikono mirefu.
Kwa ule msuli ulivyokaa kiunoni utasema katoka barazani nyumbani kwake Ilala anavuka barabara anakwenda dukani kwa Mpemba kununua kitu.
Ukimtazama hupati shida kujua kuwa huyu ni Mswahili na mtoto wa Kidaresalama kindakindaki na msuli ni kivazi chake rasmi kama vile wengine wanavyovaa suruali.
Hakika alikuwa kapendeza sana.
Fikiria katoka na msuli kutoka Ilala tena kapanda Vespa yake kaja hadi mjini, Uzunguni.
Mbashir ile kunitia machoni tu akanipokea kwa bashasha, ‘’Oh mdogo wangu Mohamed Asalaam Aleikum karibu karibu,’’ hata sijajibu salam kamgeukia muuza burger anampa oda, ‘’Mfanyie mdogo wangu burger mpe na soda aitakayo.’’
Nikamshukuru na tukawa tuko pale tunakula burger zetu tukishushia na soda huku tunazungumza hili na lile na mara chache anatupiana maneno ya unazi wa Simba na Yanga na madereva taxi waliokuwa na kituo chao pale jirani.
Kwa hali ya kawaida usingetegemea yeye kuninunulia mimi chochote kwa ile fikra ya wengi kuwa mimi ni afisa nina hela.
Mbashiri hakuwa ananiangalia mimi kwa jicho na fikra hiyo.
Mbashir alikuwa ananitazama mimi kama mdogo wake na ndugu yake, mambo ya cheo changu kazini yalikuwa mbali sana katika fikra yake.
Ukapita muda nikawa simuoni Mbashiri bandarini.
Siku moja tukakutana mpirani Uwanja wa Taifa nikamuuliza imekuwaje hatuonani.
Mbashir akaniambia kuwa ameacha kazi saa 24 ameondoka. Nikataka kujua sababu.
Mbashir akanieleza.
Kwa wale wanaomjua naamini hivi wasomapo ni kama wanamuona na kusikia ile sauti yake kubwa na kuzungumza kwake kwa vishindo.
‘’Yule jamaa yako hana adabu anataka kunivunjia heshima yangu.
Yeye kaja kuvaa suti hapa bandarini mimi nimevaa suti bado mtoto baba yangu akinipeleka kwa Jimpota fundi wa suti maarufu Dar es Salaam anishonee suti.
Nimestahamili mwisho nimeshindwa.
Siku hiyo nikamkabili uso kwa macho tukatoleana maneno nipe nikupe.
Ananitishia kazi. Nikamwambia, ‘’Mradi unaona leo nakufokea basi jua mimi kazi sina haja nayo.
Watu walijazana kibao nje ya ofisi ya bosi wetu wanashuhudia.
Baada ya kumaliza risala yangu nikamkabidhi funguo za gari nikachukua Vespa yangu nikaondoka kurudi nyumbani.’’
Huyu ndiye Hassan Mbashir rafiki na kaka yangu.
Mbashir ananikumbusha marehemu Jahazi bin Ali kwani wamefanana kwa mengi kuanzia maumbo yao hadi hulka na yeye pia Jahazi alikuwa mpenzi wa Simba na alikuwa Cargo.
Allah awaghufirie ndugu zetu tuliowakumbuka dhambi zao na awaweke mahali pema peponi.
Amin.