Buriani Maulid ''Chubby'' Tosiri

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
Picha hii na marehemu Maulid ''Chubby'' Tosiri tumepiga nyumbani kwake Magomeni Mikumi tarehe 22 October 2015 baada ya kupata taarifa kuwa hali yake haikuwa njema nami nikenda kumjulia hali .

Hili jina la Chubby, Maulid alilipata shule ya Mnazi Mmoja katika miaka ya 1960 mwanzoni wakati mwanamuziki maarufu wa mtindo wa Twist alipotoa nyimbo ambayo ilikuja kuwa maarufu sana, ''Let’s Twist Again,''

Mwalimu aliuliza darasani nani anaweza kutuimbia nyimbo?

Maulidi akanyoosha kidole mwalimu akamwambia aimbe na Chubby akaimba, ''Let’sTwist Again.''

Kuanzia siku hiyo Maulid akawa Chubby na jina hili likavuma kushinda jina lake kama ilivyo kawaida ya ''nick names.''

Msiba wa rafiki yangu Maulid umenikuta niko nje ya Dar es Salaam.

Maulid alikuwa Everton Footbal Club had Saigon na akicheza half back 6.

Mchezaji mstaarabu na ''slow.''

Wala usimuogope kwa ukubwa wa umbo lake ukadhani kuwa atakuzoe wewe na mpira.
Hana haraka katika uchezaji wake.

Namkumbuka sana Chubby kwani mimi na yeye tukiazimana viatu vya mpira.

Nilikuwa na kiatu changu Gola hivi vilitangulia Addidas kwa kuwa vikitengenezwa Uingereza na Tanganyika ilikuwa koloni la Waingereza.

Chubby miguu yake ilikuwa midogo ingawa alikuwa na jimwili la Kimanyema kubwa kwa hiyo haikuwa tabu kwake kuingia katika viatu vyangu.

Hii ilikuwa 1965 tu wadogo sana wastani wa umri wetu miaka 13/14.

Nakumbuka siku zilipotoka fedha mpya mwaka wa 1966 nilikuwa natoka shule Kinondoni Primary School nikakutana na Chubby nyuma ya kituo cha petroli cha AK Nanji na mbele yetu ni Soko la Karikaoo lile la zamani.

Basi nikawa namuonyesha noti mpya za Bank of Tanzania nilizokuwanazo na ‘’coins,’’ na yeye akawa ''really fascinated.''

Maulid tukaja kuwa pamoja East African Cargo Handling Services (EACHS) na mabadiliko yote yaliyotokea kuvunjika kwa jumuia mwaka wa 1977 na yote yaliyotufika hadi sote tukastaafu.

Chubby alikuwa na rafiki yake Twala wakipendana sana na Twala alicheza Centre Half Everton lakini ni miaka mingi Twala sijamuona.

Wengi kama Spencer watu wa zamani sana watamkumbuka. Nilipokuwa Tanga Chubby alikuja kikazi na akafika ofisini kwangu kunisalimu ni siku nyingi tulikuwa hatujaonana basi nikamchukua kwenye chai ya kabab na nylon.

Nylon ni viazi vya kukaanga havimenywi vinakaangwa hivyo hivyo na kwa kweli ni kitafunio kizuri sana kwa chai na kwa kawaida huliwa na kabab na chatney na pilipili na ndimu pembeni.

Nikipenda sana kuwachukua jamaa wakija Tanga kwenye hoteli hii ya mzee wa Kihindi Muismailia, Shamshudin ambayo ‘’speciality,’’ yake ilikuwa nylon.

Chubby alinisaidia sana kunipa historia ya baba yake na Nyerere wakati wa kuunda TANU na kudai uhuru wa Tanganyika wakati naandika kitabu cha Abdul Sykes.

Alinipatia picha za baba yake na Nyerere za wakati ule na nyingine ambazo baba yake alikuwanazo.
Allah amsamehe madhambi yake na amtie peponi ndugu yetu Maulid Tosiri.

Katika picha Chubby wa pili kushoto kavaa blazer na Mzee Tosiri huyo katikati kavaa koti na Panama Hat.

 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…