Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
(1929 - 2024)
Hiyo taazia hapo chini niliandika majuma machache yaliyopita nilipopokea taarifa kuwa Sultan Jamshid kafariki.
Haukupita muda nikapokea taarifa kuwa si kweli yu hai.
Nilijisikia vibaya sana.
Ninachokumbuka ni kupokea ujumbe kutoka kwa rafiki yangu akiniambia nilifanya haraka kuandika.
Sikuwa na la kusema.
Nilibakia kimya.
Niliandika taazia wakati Sultan Jamshid yu hai.
Taazia niliyoiandika ni hiyo hapo chini:
Jana usiku ndugu yangu kaniletea ujumbe mfupi kuwa Sultan Seyyid Jamshid, Sultani wa mwisho wa Zanzibar kafariki.
Asubuhi ndugu yangu huyu akanipigia simu tukazungumza mawili matatu akanifahamisha kuwa yeye hakupata kuonana na Jamshid ila alizungumzanae mara moja kwa simu Jamshid alipokuwa anaishi Portsmouth.
Sasa nikawa najiuliza nini naweza kuandika kuhusu Sultan Jamshid.
Jamshid kaandikwa sana kiasi nimekumbuka maneno ya marehemu Bibi Titi Mohamed aliponiambia, "Bwana Mohamed kipi utakachoandika wewe kuhusu mimi ambacho bado hakijaandikwa?"
Kipi ninachoweza mimi hii leo kuandika kuhusu Sultan Jamshid ambacho bado hakijaandikwa?
Kipo cha kuandika kuhusu Sultan Jamshid bin Abdulla bin Khalifa ambacho bado hakijaandikwa.
Jamshid kaondoka Zanzibar baada ya mapinduzi nafsi yake ikiwa imesalimika.
Jamshid anakwenda kwa Mola wake vidole vyake vikiwa safi havichuruziki damu.
Hakuna Mzanzibari anaeweza kusimama akasema Sultani ameniulia ndugu yangu au Sultani kanidhulumu haki yangu hii au ile.
Jamshid kaondoka Zanzibar hakuacha jela za mateso.
Jamshid hakuacha jela za mateso kwa kuwa hakurithi jela ya mateso.
Jamshid hakupata kukalia kiti cha enzi kilicholowa damu.
Hakika lipo la kuandika na la kusema kuhusu Jamshid.
Nimeingia Maktaba.
Natalii farahasha ya kitabu cha Harith Ghassany, "Kwaheri Uhuru Kwaheri Ukoloni."
Nataka nijikumbushe.
Najikumbusha kwa kuwa nilikuwa msaidizi wa Dr. Ghassany wakati wa utafiti wa kitabu hiki chake.
Nasoma yaliyomfika Jamshid halikadhalika nayasoma yale waliyopitia Wazanzibari waliokuwa nje ya Zanzibar mapinduzi yalipotokea.
Nayasoma na kuona kama vile ndiyo kwanza hayo nisomayo nayasikia leo.
Sultan Jamshid kapewa hifadhi Dar es Salaam yeye na familia yake na baadhi ya watu.
Wako wamejibanza kwenye nyumba mbili jumla yao watu 43.
Serikali ya Tanganyika inafanya mawasiliano na Waingereza kuhusu Sultan Jamshid.
Jamshid Sultan wa Zanzibar ni mtu masikini kwani hana fedha nje ya Zanzibar hata senti moja.
Sultan hana nauli ya kumfikisha Uingereza.
Nimetosheka.
Navuta kitabu kingine ninachokumbuka kuna habari za Sultan Jamshid.
Hili ni buku la mapicha kutoka matoleo ya gazeti maarufu DRUM lililokuwa likimilikiwa na Jim Bailey kutoka Johannesburg, Afrika Kusini.
Nilisaidia kuhariri na kuchapwa kwa kitabu hiki.
Katika kitabu hiki kuna makala ya Jamshid akiwa na watu wapatao 500 wananchi wa kawaida wanaingia porini kuwinda nguruwe.
Sultan Jamshid anaingia porini kwenye msitu mzito bila ulinzi wowote kuwinda pamoja na wawindaji wenzake wamemzunguka wamebeba mikuki.
Hakika yako mengi ya kusema kuhusu Jamshid.
Sura inayofuatia katika DRUM ni kuhusu mapinduzi chenye kichwa cha habari, "Bloodshed on the Spice Isle."
Nahitimisha safari yangu Maktaba kwa kitabu muhimu sana katika historia ya masultani: "Omani Sultans in Zanzibar," kilichoandikwa na Ahmed Hamoud Al Maamiry.
Mwanzo wa kitabu mwandishi anasikitika kuhusu damu iliyomwagika katika mapinduzi.
Siku zote historia ya mapinduzi itakuacha na majonzi.
Mwenyezi Mungu amfanyie wepesi hisabu yake ndugu yetu Sultan Jamshid bin Abdulla bin Khalifa.