Busara itumike kukomesha mauaji haya ya wakulima, wafugaji

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
Kuna taarifa kuwa hali ya amani na utulivu katika baadhi ya maeneo ya vijiji vya Mvomero ni mbaya. Watu wanashambuliana, wanaumizana na kuuana kinyama. Mifugo pia inauawa. Nyumba zinachomwa moto na mashamba yanateketezwa.

Inaelezwa kuwa yote ni matokeo ya mgogoro uliofukuta kwa siku kadhaa baina ya wakulima na wafugaji kuhusiana na maeneo ya malisho na kilimo kabla ya kufikia hatua hiyo inayotajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kuonekana katika maeneo ya wilaya hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa hadi kufikia jana, watu sita walishapoteza maisha yao kutokana na mapigano hayo, 36 kujeruhiwa vibaya huku baadhi yao wakikimbiziwa hospitalini, wakiwamo waliolazwa katika Hospitali ya Misheni ya Bwagala iliyopo Turiani wilayani humo. Watu 30 pia wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusiana na vurugu hizo.

Hizi ni habari mbaya sana. Na wala hakuna maelezo ya kutosha kuelezea kiwango cha huzuni ambacho sisi na Watanzania wengine tumekuwa nacho kila mara tunaposhuhudia Watanzania wenzetu wakiuana kwa sababu ya migogoro ya aina hii; ambayo mara nyingi husambaa zaidi na kumwaga damu za watu wengi zaidi pindi hatua za haraka zisipochukuliwa.

Si nia yetu kutaka kuingia kiundani kwa sasa na kujua ni kundi gani lenye makosa kati ya wakulima na wafugaji. Bali, tunalaani vurugu na mauaji haya kwa nguvu zote. Hayastahili kuvumiliwa hata kidogo katika ardhi ya nchi hii ambayo tunu yake kubwa ni hali ya amani na utulivu.

Hakika, kila binadamu ana haki ya kuishi. Na kila Mtanzania anapaswa kuhakikishiwa haki hii ya msingi iliyoainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa misingi hiyo, haitazamiwi, na wala haikubaliki hata kidogo kuona kuwa taifa linapoteza raia wake kwa sababu ya visa vya kuuana wenyewe kwa wenyewe, huku chanzo kikiwa ni kugombea ustawi wa mazao na mifugo yao.

Tunakumbwa na huzuni kwa kiasi kikubwa kuona kuwa baadhi ya Watanzania wakiweka ubinadamu nyuma na kutanguliza mbele mazao yao kama mpunga na mifugo yao kama ng'ombe na mbuzi.

Tunalaani mauaji haya kwa kila hali kutokana na ukweli kuwa uhai wa mtu hauna kitu cha kuulinganisha. Kwa namna yoyote ile, thamani ya mwanadamu ni kubwa kuliko mpunga na ng'ombe na hivyo, hakuna anayestahili kuuawa ili kulinda vitu hivyo.

Tunatambua kuwa vipo vyombo vya kushughulikia matatizo haya. Tunajua vilevile kuwa ni Serikali pekee, kwa kushirikiana na wahusika ambao ni wakulima na wafugaji, ndiyo inayoweza kubaini kwa uhakika ni wapi pamekosewa, na nini cha kufanya ili kurejesha hali ya amani na utulivu katika maeneo hayo.

NIPASHE tunajua kuwa baadhi ya viongozi wa serikali wamepiga kambi katika eneo la tukio, wakijaribu kuzungumza na pande zote ili hatimaye kurejesha hali ya utulivu iliyokuwapo awali.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro alishafika katika eneo la maafa, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro na Waziri wa huko. Tunajua vilevile kuwa Jeshi la Polisi pia limebakiza askari wake wengi huko kwa nia ya kudhibiti vurugu na mauaji hayo.

Hata hivyo, wakati tukiunga mkono kwa dhati juu ya hatua hizo za awali katika kumaliza tatizo hilo, tunadhani kwamba sasa kuna kila sababu ya kutanguliza busara zaidi ili kukomesha vitendo vyovyote vile vya kuhasimiana miongoni mwa makundi ya wakulima na wafugaji.

Tunaamini kwamba miongoni mwa hatua za awali katika kuwahakikishia amani wananchi wa maneo hayo ni kufanya mazungumzo na viongozi wa pande zote mbili. Kwa kufanya hivyo, walau suluhu ya haraka katika kipindi hiki itapatikana; hivyo kutoa nafasi kubwa zaidi kwa mamlaka zinzohusiana na ardhi, kilimo, mifugo na vyombo vya usalama kuendelea kusaka suluhu ya kudumu.

Jambo kubwa hapa ni kuhakikisha kwamba viongozi wote, kuanzia ngazi ya vijiji hadi taifa wanatekeleza wajibu wao wa kutumia busara zao katika kuzuia matukio kama hayo.

Uanzishwe utaratibu mzuri wa kuzuia mapema matukio kama hayo kwa kushughulikia malalamiko ya wananchi wa pande zote mapema na siyo kusubiri kukua kwa migogoro hii hadi kufikia hatua ya watu kuuana.

Wakulima na wafugaji wanapaswa pia kuelimishwa kila uchao, pasi na kuchoka, kuwa amani na utulivu ndiyo msingi wa maendeleo yao.

Kamwe wasiruhusu migogoro yao kumalizwa kwa mapigano na kuharibiana mali kwani athari za vitendo hivyo ni kubwa na mbaya zaidi kwao na kwa taifa.

Mifugo huuawa, mazao huharibiwa, elimu hudorora na biashara za kila aina husimama katika maeneo yenye migogoro na wao ni mashahidi wazuri kwani katika siku chache hizi, wamejionea namna hofu ilivyotanda miongoni mwao. Kuna taarifa kuwa baadhi yao walikimbilia msituni ili kujiepusha na vurugu hizo.

Shime, busara itumike kuhakikisha kuwa maridhiano baina ya wakulima na wafugaji yanafikiwa na mwishowe kukomesha mauaji haya yasiyovumilika.




CHANZO: NIPASHE

 
Migogoro itaisha pale land use itakapotekelezwa, ,mara nyingi utasikia wanagawa viwanja vya makazi si mashamba au maeneo ya ufugaji, bila muongozo wa kisheria busara haitotosha, nitafurahi nikisikia serikali imepima mashamba imeweka miundombinu na kuyagawa kama wanavyogawa viwanja, the same kwa ufugaji
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…