Rais Bush wa Marekani kukaa Tanzania siku nne ziara ya Afrika
*Kutembelea Arusha, Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu
Rais George Bush anatarajiwa kukaa kwa siku nne nchini Tanzania kati siku saba za ziara yake kutembelea Bara la Afrika.
Akizungumza katika kikao cha wahariri kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jana, Msemaji wa ubalozi wa Marekani nchini, Jeffery Salaiz alisema katika ziara hiyo Rais Bush atatembelea mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.
Alisema kwamba ziara hiyo ina malengo makuu matatu, ambapo kwa pamoja yanadhihirisha nia ya Marekani kuijali Afrika.
Wakati wa ziara hiyo, Bush atakagua baadhi ya miradi mbalimbali ambayo serikali chini ya uongozi wake imekuwa inasimamia na kufadhili kwa karibu.
Alitaja miradhi hiyo kuwa ni ya Ukimwi na Malaria ambayo kwa sehemu kubwa imesaidia idadi ya wagonjwa na vifo vitokanavyo na malaria katika Visiwa vya Pemba.
Rais Bush anatarajiwa kuanza ziara ya kutembelea nchi tano za Afrika kuanzia Februari 15 hadi 21. Nchi hizo ni Benin, Tanzania, Rwanda, Ghana and Liberia.
Marekani ni moja ya nchi ambazo ni wafadhili wakubwa kwa Tanzania, ikiwa imetoa Sh700 bilioni kwa mwaka huu. Kuanzia mwaka 2003 Marekani imetoa zaidi ya Sh700 bilioni kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya Ukimwi.
Katika mradi wake wa kupambana na malaria, Marekani imekwishatoa zaidi ya Sh77 bilioni.
Ziara ya Bush inatarajia kujenga uhusiano mzuri kati ya nchi hizi mbili na kuitangaza Tanzania duniani kwa kuwa waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa wanatarajiwa kuaambatana naye.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Marekani kukaa Tanzania kwa siku nne kwani mara ya mwisho Rais wa nchi hiyo, Bill Clinton alipotembelea nchini mwaka 2003 alikaa nchini kwa masaa matatu tu.