R.I.P Captain Mazula, tumepoteza Rafiki na ndugu wa kweli mwenye kuipenda nchi yake kwa dhati. Mwenyezi Mungu ailaze Roho yake mahali pema peponi
Alipokuwa mwanafunzi pale Tambaza, nakumbuka wanafunzi wengi walijua mara moja kwamba George Mazula aliipenda nchi yetu kwa dhati na alikuwa tayari kufanya chochote kulitumikia taifa letu. Alikuwa jasiri, shupavu, lakini pia mnyenyekevu.
Alichaguliwa na headmaster wetu, Mr. Lila, kuwa head prefect mwaka 1970. Kabla ya hapo mwaka 1969, alichaguliwa kuwa mmoja wa ma prefect wa shule yetu Tambaza High School. Na sisi sote tulijua kwamba alistahili kuwa kiongozi.
Na licha ya madaraka aliyokuwa nayo, alijulikana kuwa ni mtetezi wa wanyonge. Wengi wetu tulisema kwamba angefaa kuwa kiongozi miaka ijayo na tulifikiri kwamba labda angesomea masomo mengine - na si ya kisayansi - ili apate kazi serikalini na kuendelea huko mpaka atakapokuwa kiongozi wa taifa. Alikuwa katika Form V na Form VI Science (1969 - 1970).
Na katika mazungumzo yetu, alisema mara nyingi kwamba anataka kuwa rubani - na atakuwa rubani! Hakuwa na mashaka hata kidogo. Na alifanikiwa.
Alikuwa ni kiongozi. Hata headmaster wetu, Lila, alijua mara moja alipomchagua kuwa prefect mwaka 1969 na head prefect mwaka 1970 kwamba ni kiongozi na anastahili kuwa kiongozi wa wanafunzi wenzake.
Nakumbuka pale H.H. The Aga Khan Hostel, Upanga, kulikuwa na wanafunzi wa Kihindi tulioishi nao walioonyesha kwamba wanatudharau sisi wanafunzi weusi. George Mazula aliwanyosha mara moja mbele ya wanafunzi wengine, na kwa sauti nzito, na walikuwa wanamwogopa sana; si kwa sababu alikuwa anawakandamiza - walimwogopa kwa sababu alikuwa anasema ukweli mbele ya watu.
Alijulikana katika shule yetu kama Msema Ukweli. Hakumwogopa mtu. Lakini kuliko kitu chochote kama prefect pale Tambaza High School, aliheshimiwa na alipendwa sana na wanafunzi wenzake kwa sababu alikuwa ni mtetezi wa wanyonge.
Na angekuwa jeshini, sisi sote tuliomfahamu tungemwona askari shupavu, na General, anayeongoza jeshi letu vitani kuilinda nchi yetu.
A true patriot! A gem! Tangu alipokuwa kijana hadi alipotuondoka.
Ametuacha, lakini bado yuko nasi mioyoni. And the ideals he cherished and upheld will always inspire us. Daima!
Kwaheri, Ndugu Mazula, and rest in peace until we meet again where you are. There's a better place than the world you left behind. Umetutangulia, tutakufwata. As always, tuko nyuma yako.
Rest in peace, Ndugu! Mzalendo halisi!