Casablanca papers

Kudo

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2017
Posts
1,821
Reaction score
6,119
RIWAYA; . CASABLANCA PAPERS....
NA; BAHATI MWAMBA...


Sehemu ya kwanza...

Alikuwa ni mmoja wa watu maarufu sana ndani ya jiji la Dodoma, umaarufu wake haukumkuta kwa bahati mbaya bali ni kwa sababu ya umahiri wake wa kuchoma nyama kwenye minada maarufu ya mji wa Dodoma. Hakuwa ameishi Dodoma kwa muda mrefu, miaka mitatu ilitosha kumpa umaarufu huo ambao hata wenyeji hawakuwahi kuwa nao.

Alikuwa ni hodari wa kutembelea minada ya kuuza mbuzi nae akawa mchuuzi mzuri mwenye kuzingatia afya ya mifugo kabla ya kuwanunua. Wakati wengine wakinunua wanyama kwa lengo la kupata faida kubwa, yeye alikuwa akinunua kwa kutaka kupata wateja watakaoridhika na ladha ya nyama atakayowachomea, mnyama aliyekonda halikuwahi kuwa chaguo lake na badala yake alihakikisha anachukua Mbuzi au Kondoo aliyenawiri na mwenye afya nzuri, hiyo ikawa njia ya kwanza iliyomletea wateja wengi kwenye jiko lake na aliuza wanyama wengi waliochinjwa kwa siku moja.

Njia ya pili iliyompa umaarufu ni ya kuhakikisha anahudhuria kila mnada bila kujali ukubwa au udogo wake, mbali na kununua kwenye hiyo minada pia aliweka jiko lake na kuuza kulingana na uchangamfu wa mnada wenyewe, kwa njia hiyo akawa ni mtu anaefahamika sana angalau na robo tatu ya watu waliokuwa wakihudhuria minadani.

Njia nyingine iliyomweka karibu na watu ni kwa kutumia uso wake, muda wote alihakikisha tabasamu halikauki usoni mwake, maneno ya utani na ucheshi yalimtoka na kuwaacha watu wakiyafurahia, umbo lake la kimo cha askari polisi na wajihi wa kutuna misuli ulikuwa ni kivutio kingine kwa wanawake waliokuwa wakipenda kumchangia jikoni kwake, wanawake wenye mahusiano waliwashinikiza mabwana zao kununua nyama choma kwake ili wapate nafasi ya kumuona kwa ukaribu, wale ambao hawakuwa kwenye mahusiano walijisogeza angalau wapate kusikia neno tamu zaidi ya ucheshi wake, walinunua huku wakiyageuza macho yao kwa namna ya kumuita kwa ishara ya ukaribisho kwenye nafsi zao,

Aliwaona na alielewa lakini kamwe hakuwahi kuthubutu kutafuta mahali pa kuangukia na kuzika hisia zake, alijiepusha, lakini haikuwa bahati mbaya bali alijiepusha makusudi huku akizihesabu siku kwa namna aliyojua yeye.Siku moja akiwa maeneo ya Msalato kilomita kumi na mbili kutoka Dodoma mjini, kwenye jiko lake alitembelewa na mwanamke mmoja ambae mara kwa mara alikuwa akimuona sehemu mbalimbali za jiji, mara zote alizowahi kumuona aliishia kumweka kwenye hesabu ya watu ambao walikuwa na upungufu wa akili.

Mwanamama huyo mara zote alionekana kuwa msafi na asiyekaukiwa tabasamu, lakini mavazi yake yalimtambulisha tatizo alilokuwa nalo na kila mmoja alikubali alikuwa ni mgonjwa wa akili licha ya kujipenda kwa usafi lakini mavazi aliyojipigilia pamoja na miondoko yake viliishia kumshushia hadhi ya umaridadi wake. Hakumtilia maana, akaendelea na hekaheka za kuwahudumia wateja wake huku akiwaroga na ucheshi wake.

Mwanamke huyo ambae kwa kumkadiria umri wake usingelizidi miaka thelathini na tano, aliendelea kusimama pembeni ya wateja wengine huku akimtazama mchomaji kwa namna ya ajabu ambayo hakuna mtu aliielewa. Baadhi ya wateja walihisi ananjaa na anahitaji chakula au ametamani nyama iliyokuwa ikikaushwa na moto wa mkaa, mmoja akapaza sauti na kumpa ofa ya nusu kilo huku akimtaka atafute pahali tulivu wakati ofa yake ikishughulikiwa.

Akakubali na kushukuru kwa namna ambayo kila mmoja alijua kweli alikuwa na matatizo kichwani mwake, licha ya kushukuru lakini haikuwa sababu ya yeye kuondoka kando ya jiko kama alivyoombwa na msamaria mwema badala yake aliendelea kusimama na macho yake akiyageuza kama mtu aliyekaribu kukata roho, alifanya hivyo kila alipokutanisha macho yake na mchoma nyama. Watu wengine hawakuelewa wala hawakuwa wakiyaona macho yake hayo kwenda kwa mchoma nyama, lakini mchomaji yeye alianza kuvutiwa na mtindo huo wa kutazamwa na akaanza kuuzingatia na kila mara akawa akiyatupa macho yake kwa mtazamaji ambae nae aliendelea na mchezo wake bila kukoma.

“Nyama yangu tayari?” Mtazamaji alimuuliza mchoma nyama huku akijichekesha, lakini hakuwa akimtazama usoni kama wakati ambao alikuwa kimya.
“Bado kidogo... Dakika sita hivi..” Mchomaji alijibu huku mikono yake ikifanya kazi ya kugeuza mapande ya nyama juu ya jiko la chuma.

“Mwewe unalala sana bwana. Amka!” Alisema kwa sauti ya dhihaka hadi wateja wengine walijikuta wakicheka, mchoma nyama nae alicheka huku jambo fulani likipita kichwani na kumfanya amtazame mwanamke yule mwenye upungufu wa akili, akakutana na macho yakizungushwa kwa mtindo usio wa kawaida.
“Niamke?” Mchomaji alimuuliza huku akicheka ili watu wasielewe alichokuwa ameelewa kutoka kwa mtu mwenye upungufu wa akili.

“MWEWE, amka!” Mwanamke alisema huku akiangusha tabasamu lakini tabasamu lake wakati huu halikupokelewa na mchoma nyama, badala yake aliona ishara ya kuitwa pembeni na mchoma nyama akiwa na bahasha iliyofungwa nyama ndani yake. Mchoma nyama alikuwa ameelewa bila kueleweshwa, neno Mwewe lilimaanisha alichokisikia na hakuwa na chembe ya shaka juu ya yule mwanamke ambae tangu afike Dodoma amekuwa akimuona sehemu mbalimbali za mji, bahati mbaya nyakati zote hizo hakuwahi kujiuliza swali ambalo wakati huo tayari alikuwa ameshajiuliza na alikuwa na jibu lake; mwanamke yule alifikaje kwenye mitaa mbalimbali ya jiji?

“11:39 pm Uvundo lodge.” Mwanamke alimwambia huku mikono yake ikipokea nyama iliyofungwa kwenye kifungashio, akaondoka zake bila kusubiri jibu au swali kutoka kwa Honda Makubi ambae alikuwa ni mchoma nyama maarufu jijini Dodoma kiasi cha kuaminiwa na kualikwa kwenye baadhi ya matukio makubwa yaliyohusisha ulaji nyama kavu, kila pahali alifika isipokuwa Ikulu.

Baada ya kupewa ujumbe huo ni kama akili yake haikuwa sawa, akasahau kuweka tabasamu lake la mitego kwa wateja wake, akawa hamjibu kila mteja aliyejaribu kumchangamkia, wapo waliomuuliza kulikoni na wapo ambao waliamua kukaa kimya kwa kudhani siku hiyo kwake haikwenda kumalizika salama, walikuwa sahihi.

Baada ya ujumbe kutoka kwa mwanamke kichaa mawazo yake hayakuwa kwenye biashara tena bali kwenye ujumbe. AMKA! MWEWE.. Maneno aliyoyaelewa vema na alijua alitakiwa kufanya nini endapo angelikutana na ujumbe wa namna hiyo kwenye maisha yake, ujumbe ambao hakuwahi kujua ataupokea lini na wapi kabla ya siku hiyo.

Saa moja baadae aliamua kuikabidhi kazi yake kwa msaidizi wake wa karibu ambae walijuana kwenye harakati zake za uchuuzi wa wanyama, Honda Makubi akatoweka Msalato na kuelekea alipokuwa ameweka makazi yake maeneo ya Nkuhungu, huko alijifungia ndani na hakutoka watu wakimuona, alitoka saa tano kamili usiku akiwa na begi lake mgongoni, begi ambalo lilikuwa na nguo chache na pea moja ya viatu.

Saa tano na dakika thelathini na saba alikuwa nje ya mlango wa kuingilia Uvundo lodge, akausukuma mlango na kuishia mapokezi.
“Nitapata chumba? Naitwa Kiraka.” Alisema huku akimtazama mhudumu usoni, mhudumu nae akakwepesha macho yake na kutazama ukutani ambapo aliiona saa iliyomsomea ni dakika moja kabla ya kufika saa tano na dakika thelathini na tisa.

“Mwenyeji wako alishalipia chumba chako, funguo hii hapa..” Mhudumu alimwambia huku akimpa ufunguo wa chumba namba 14, akapokea na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba alichoelekezwa na mhudumu, akatumbukiza ufunguo kwenye tundu la kitasa na kufyatua loki zake, mlango ukawa wazi na akajitosa ndani bila wasiwasi wowote.

Akalivua begi lake na kulitupa kitandani, macho yake akayazungusha kila pembe na kuridhishwa na usalama uliokuwepo, hakuona chochote mbali na kitanda kilichotandiwa mashuka ya rangi ya bluu. Chumba kilikuwa na choo kwa ndani hivyo hakuridhika na ukaguzi wake wa mahali pa kulala, akapiga hatua hadi alipoufikia mlango wa maliwato, akashika kitasa na mkono wake ukataleza. Akasimama akikitazama kitasa huku akachezesha vidole vyake ambavyo viligusa utelezi kwenye kitasa cha mlango, akarudia tena kukishika lakini wakati huu alikishika kwa nguvu zaidi ili asiteleze, akafanikiwa kuusukuma mlango na kuingia. Kitu cha kwanza alichokiona ni sabuni iliyokuwa juu ya sinki la choo na ilikuwa ni kipande kikubwa tofauti na vipande

Vinavyowekwa kwenye nyumba za kulala wageni, mbali na kipande hicho hakuna kingine alichokiona zaidi ya kandambili za rangi mbili tofauti, hakushangazwa na hilo kwa kuwa ilikuwa ni utaratibu wa nyumba nyingi za wageni kuweka ndala za rangi mbili tofauti au za mguu mmoja wakiwa na lengo walilojua wao.

Akakata shauri arejee chumbani lakini kabla hajaufikia mlango akakumbuka kunawa mkono wake uliokuwa umegusa utelezi ambao alihisi ni wa sababuni na alibashiri pengine uliachwa na mhudumu au mtu aliyetumia chumba muda mfupi kabla yeye hajaingia.

Alinawa vizuri mikono yake kwa sabuni aliyoichukua kwenye sinki, alipohakikisha mikono yake imetakata alitaka kugeuka na kuondoka lakini alisita baada ya kukumbuka kama aliona kitu kwenye kipande cha sabuni wakati akiipitisha kwenye viganja vyake, akaikota tena na kuitazama kwa ukaribu zaidi na alikubaliana na kumbukumbu zake, kipande kilikuwa kimeunganishwa baada ya kukatwa katikati. Akakivunja kufuatisha ufa aliuona, macho yake yakakutana na kifundo cha kipande cha gazeti, akakitoa na kukishika kwenye mkono wake mwingine huku akikichunguza kwa umakini mkubwa.

“Ujumbe!” Aliwaza huku akiondoa kipande cha gazeti ambacho kilikuwa kimeloweshwa na unyevunyevu wa sababuni, alisaliwa na kipande cha karatasi nyeupe ambayo ilikuwa na maandishi ya wino wa kalamu ya mkaa.
‘KINYONGA AAMSHWE..KUNAFUKUTA.. OFISI NAMBA 9 MAKUTANO YA MWISHO.’ Ujumbe ulisomeka hivyo na aliuelewa. Hakuwa na shida ya ziada na kipande cha karatasi chenye ujumbe mzito kwake, akakitupa kwenye tundu la sinki na kuruhusu maji yakisombe kukiingiza kwenye njia ya shimo la takatumbo, alipohakikisha karatasi imesombwa na maji aliamua kutoka na kuelekea chumbani, akalitwaa begi lake na kuliweka mgongoni kisha akatoka na kukifunga chumba, akaenda hadi mapokezi na kukabidhi funguo huku akidanganya atarejea muda mfupi baadae kwa kuwa alikuwa hajala na alitaka kutafuta chakula huko nje. Ukweli ni kwamba huo ulikuwa ni muda wake wa mwisho kuwepo Dodoma na machweo yasingelimkuta akiwa kwenye ardhi hiyo aliyoikalia kwa zaidi ya miaka mitatu, safari yake ilikuwa ni jijini Dar es laam lakini kabla ya kufika huko alitaka kupitia Bagamoyo akiitumia njia ya Msata.
* * **
Saa nne na nusu ahsubuhi ilimkuta akiwa kwenye ardhi ya Bagamoyo na sehemu aliyochagua kuweka kituo chake cha mwisho ndani ya mji huo ni mita mia mbili, mashariki mwa soko kuu la mji huo wenye bahati ya kutembelewa na wageni wa kila aina, iwe ahsubuhi, mchana,jioni au usiku. Wageni wasiochoka kufurahia vivutio mbalimbali vya utalii. Kwenye moja ya mifuko iliyokuwa kwenye begi lake alikuwa ametoa kipande cha sarafu ya kale, kipande hicho kilikuwa na ukubwa wa nusu duara. Alipokuwa amesimama pembeni yake kulikuwa na vibanda vya wajasiliamali wadogo waliokuwa wakiuza maandazi na vitumbua, alitembea taratibu akiwa amekilenga kibanda kimoja kati ya vibanda sita vilivyokuwa vimejipanga kwa kufuatana.

“Karibu.” Alipokelewa na sauti ya bashasha kutoka kwa mwanamke wa Pwani aliyekuwa amejisitiri kwa hijabu lilolomfunika sehemu kubwa ya mwili wake, akapokea ukaribisho huo kwa kutupa tabasamu laini pasipo na kuongeza neno lingine, mkono wake mmoja ulizama kwenye mfuko wake wa suruali na kutoka na noti ya shilingi elfu mbili, akampa muuzaji.

“Naomba vitumbua sita..chenji baki nayo..” Alisema.
“Ahsante sana, hakika Mungu akuongezee zaidi kwenye kipato chako.” Mwanamke alishukuru kwa kupiga magoti, lilikuwa ni jambo la kuvutia kuona bado wapo wanawake wenye heshima ya kupiga magoti wakipewa kitu, Dunia ya sasa imewakimbiza wanawake wa namna hiyo.
“Amin..” Alijibu huku akimtazama kijana mdogo wa umri wa kupata miaka kumi kasoro hivi, alimchangamkia.
“Huyu kijana ni wako?” Alimuuliza yule mwanamke ambae wakati huo alikuwa akihesabu vitumbua na kuvifunga kwenye gazeti.

“Ni mwanangu...” Alijibiwa.
“Anasoma?” Aliuliza tena huku akipokea vitumbua vyake na kuviweka juu ya meza moja iliyokuwa ndani ya kibanda, akavuta kiti na kukaa.
“Ndiyo.. lakini Leo anaripoti shuleni majira ya saa sita mchana, wanazamu na wenzao ambao hutoka wakati huo..”

“Aha, nilipata wasiwasi kidogo kumuona hapa wakati wenzake wapo shule.” Alisema huku akicheka kidogo, akamtazama tena yule mtoto ambae wakati huo alikuwa amesimama kando ya Mama yake. Kabla mwenyeji wake hajakoleza mada, akawahi kuchomekea swali lililomfanya afike pale na kununua vitumbua.
“Hivi mnafahamu Sheikh Ally?”

“Sheikh Ally... Mh! Hapa wapo Ally wengi sana na wengi wao tunawafahamu.” Mwenyeji alimjibu.
“Yule anaeuza njegere na vitunguu maji hapo sokoni..” Alimsema aliyekuwa amemkusudia.
“Aah! Huyo hakuna asiyemfahamu hapa mtaani na pengine hadi mitaa ya jirani.” Alijibiwa.
“Basi naomba nimtume kijana wako.” Alisema huku akiwa na uhakika ombi lake litakubaliwa, elfu mbili aliyoitoa yote tayari ilitakiwa kulipwa kwa namna hiyo aliyokuwa ameitaka, hata kufika kwake kwenye kile kibanda ni baada ya kumuona huyo mtoto na alitaka kumtumia kufika kwa Ally. Wakati wenyeji wake wakisubiri kuuona mzigo au kusikia maneno ya kuagizwa, Honda Makubi alimpa kipande cha sarafu.
“Nenda na uwahi kurudi.” Alimwambia yule mtoto kisha akainuka na kutoka huku aliyetumwa akijipanga kuianza safari kuelekea sokoni. Honda alipotea usoni mwa muuza vitumbua bila kuaga.

Sheikh Ally alikuwa ni mfanyabiashara maarufu nje na ndani ya soko la Bagamoyo, umaarufu wake ulichagizwa na namna alivyokuwa akihudumia wateja wake hasa wale ambao ingeliwawia ugumu kufika sokoni, aliwapelekea hadi majumbani mwao. Kwa kuwa alikuwa na wateja sehemu mbalimbali, akawa hana budi kuajiri vijana zaidi ya sita ambao kazi yao ilikuwa ni kusambaza majumbani mwa watu, mbali na biashara hiyo alikuwa na kazi nyingine ambayo ilimzidishia umaarufu, alikuwa ni kiongozi kwenye moja ya misikiti iliyokando ya soko na alisifika kwa mada zake nzuri zenye mafundisho na maonyo ndani yake, alipendwa na kila rika. Siku hiyo kwake ilikuwa kama siku zingine za kawaida, aliamka alfajiri kwa ajili ya swala kisha akafanya mazoezi kidogo hadi jua lilipochomoza, akaoga na kuvaa kanzu safi kama ilivyokuwa utaratibu wake kuvaa vazi hilo mara nyingi kwa wiki, kisha akaelekea sokoni kufungua kizimba cha biashara yake ya vitunguu na njegere. Saa tano kasoro alipokea mgeni ambae hakuwa mteja, bahati nzuri wakati huo alikuwa anaagana na mteja wake na hakukuwa na mteja mwingine zaidi ya kijana mdogo ambae hakuonekana kutaka chochote. Kijana alimsalimia kwa heshima kiongozi wake huyo wa kiimani kisha akampa alichotumwa.
“Nani kakupa hii?” Alimuuliza huku akimkazia macho.
“Ni mteja wa Mama.” Kijana alijibu. Sheikh Ally alikitazama kipande cha sarafu kwa namna ya kukihakiki, kisha akakitia kwenye mfuko wa kanzu yake.
“Ahsante sana, uendelee na moyo wako wa utii.” Alisema huku akimpa noti ya shilingi elfu moja, kijana alipokea na kuondoka. Baada ya kubaki peke yake alikitoa tena kipande cha sarafu na kukitazama, kilikuwa sawasawa na kipande alichokuwa nacho nyumbani kwake.
“Kumekucha..” Alisema huku akikirejesha kwenye mfuko, akachukua simu yake na kumpigia mmoja wa wasaidizi wake ambae hakuwa mbali, alimtaka kufika haraka ili amkabidhi ofisi kwa muda usiojulikana. Baada ya kuwasiliana na msaidizi wake hakuiweka simu chini, akazitafuta namba za mmoja wa viongozi wa msikiti aliokuwa akihudumu, akaomba ruhusa ya kuwa mbali na huduma kwa muda wa wiki kadhaa ili apate muda wa kushugulikia matatizo ya familia yake ambayo hakuna aliyewahi kujua ilipokuwa, wala wakati huo hakusema familia yake ipo wapi. Akapewa ruhusa na akatajiwa jina la mtu atakaekaimu nafasi yake kwa wakati wote atakaokuwa hayupo, akakata simu na kumsubiri msaidizi wake ambae mara kadhaa alikuwa akimuachia biashara na kuikuta salama. Dakika chache baadae alikuwa anatoa maagizo ya msingi kwa msaidizi wake kisha akaaga na kuondoka kuelekea nyumbani kwake, kilomita mbili kutoka sokoni. Saa saba kasoro Sheikh Ally alikuwa kwenye gari akiwa ni miongoni mwa abiria waliokuwa wakitoka Bagamoyo kuelekea Dar es laam, begi dogo likiwa juu ya miguu yake. Muonekano wake wakati huo ulikuwa ni wakijana mtanashati ambae usingelimdhania kama ni kiongozi wa dini, alikuwa amevaa raba nyeupe, suruali ya jinzi na fulana nyeupe, kichwani alivaa kofia nyeusi, mkononi alivaa saa ya bei ghali ambayo hakuwahi kuivaa nyakati zote alizokuwa Bagamoyo na aliyekuwa karibu yake alifurahia harufu nzuri ya uturi usioumiza pua zake. Rasmi alikuwa analiacha jina la Sheikh Ally na kubaki na jina lake kamili ambalo ni wachache walilifahamu, aliitwa Obimbo Mtei mzaliwa wa Chakechake, Pemba, huku akiwa amekulia na kusomea Dodoma.
 
Majira ya saa kumi jioni yalimkuta akiwa tayari ndani ya jiji la Dar es laam, begi lake mgongoni na alikuwa akitembea kwenye mitaa ya Posta huku kila mara akiitazama saa yake, hakuonekana kuwa na haraka yoyote ni kama alikuwa akizurura karibu na mitaa ya nyumbani kwake. Wakati wote alikuwa makini na watu aliokuwa akipishana nao, alihakikisha hakuna aliyekuwa akihangaika na hatua zake, alijihakikishia usalama kabla ya kuelekea makao makuu ya jeshi la polisi nchini Tanzania, alijitambulisha kwa askari waliokuwa kwenye kibanda cha mapokezi na alisema anashida ya kuonana na Kamishina Zenge wa Zenge, alihitaji kuonana nae kwa shida binafsi. Aliruhusiwa kuelekea kwenye ofisi namba tisa iliyokuwa ghorofa ya pili, hakuhitaji kusindikizwa kwa kuwa alikuwa anaifahamu. Muda mfupi baadae alikuwa anausukuma mlango pasipo kugonga, akaingia ndani na kupokelewa na macho ya watu wawili waliokuwa wamekaa wakitazama mlangoni, hakuwasalimia, akavuta kiti na kukaa akielekeana na mmoja wao huku wakitenganishwa kwa meza na kiti alichokuwa amekalia Mzee mmoja aliyekuwa kapendeza kwenye mavazi yake ya kipolisi yaliyojaa tepe za vyeo mabegani mwake. Alikuwa ni Honda Makubi na Obimbo Mtei kwenye ofisi ya Kamishina Zenge wa Zenge.
“Ni kawaida kwa Kinyonga na Mwewe kutosalimiana..” Kamishina Zenge wa Zenge aliongea huku akiangusha tabasamu adimu kuonekana usoni mwake, hakuwatazama wageni wake na badala yake akainama chini ya meza yake.
“Nilipoona hii nikajua Mwewe yuko salama.” Obimbo alimjibu Kamishina huku akitoa kipande cha sarafu ya kale na kumpa Honda Makubi.
“Ni vizuri..” Kamishina alisema huku akiweka simu mbili mezani kwake, zilikuwa ni simu tofauti na simu zingine za kawaida; kwanza zilikuwa ni ndogo sana kiasi kwamba ukiifumbata kiganjani haiwezi kuonekana, pia ilikuwa na mfuniko ulioungwa na kitu mfano wa kipande kidogo cha karatasi, kipande hicho chenye rangi ya shaba kilikuwa ni maalumu kwa kupokea mionzi ya jua kwa ajili ya kuchaji simu hiyo, pia kipande hicho kilikuwa na kazi ya kupokea mawimbi ya mawasiliano kutoka kwenye setilaiti.
“Bila shaka kila mmoja alikotoka ni salama..” Kamishina alisema huku akiangusha macho yake kwa kila mmoja, nyuso zao zilitoa jibu bila sauti lakini zilioonesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichokuwa kimewaweka pale. Hakutaka kupoteza muda, alisema nia ya wito wake.
“Kwa miaka yote tuliyowahi kuwa pamoja na kufanya kazi kwa mafanikio makubwa, iwe ndani ama nje ya nchi lakini sikuwahi kuwaweka muda mrefu wa mapumziko kama ilivyotokea sasa, ila kubwa zaidi ni namna ya kupata taarifa za kikao hiki, hamjawahi kuuona utaratibu huu hapo kabla.” Alimeza mate na kuendelea..
“Kitengo changu kimekaa likizo kwa muda mrefu kuliko kawaida, halikuwa takwa langu bali ni hitaji la kiongozi mkuu, yule ambae mara zote tunawasilisha kwake, namaanisha Rais. Sikujua kwa nini aliamua kutupa likizo na alinambia akinitaji atanipata wakati wowote na hapo ndipo tutarudi rasmi kazini na sasa tupo kazini.” Alinyamaza kidogo na kuyaacha maneno yake yaingie vema vichwani mwa vijana wake wanaofanya kazi fiche chini ya kikosi maalumu kisichoingiliana na idara yoyote ya usalama, kikosi hiki kiongozi wake ni Kamishina Zenge wa Zenge ambae hakuna aliyewahi kujua anakazi ya ziada na anaripoti kwa rais moja kwa moja. Kazi ya kikosi maalumu ni kuhakikisha inaondosha hatari zote zenye muingiliano wa kidiplomasia, kupambana na hatari zilizoshindwa kutatuliwa haraka na vyombo vya usalama, kuhakikisha rais anakuwa salama popote anapoenda, kiufupi kilikuwa ni kikosi kisicholala kuhakikisha nchi inakuwa salama usiku na mchana. Kikosi hiki kilikuwa na watu zaidi ya ishirini nchi nzima, watu kumi nje ya nchi na wengi wakiwa nchi za hapa Afrika huku watu watano wakiwa nchi za Marekani na Uingereza, watu wote hao walikuwa wakiripoti kwa Kamishina Zenge wa Zenge. Wakati wa likizo kutoka kwa rais si kama kweli kitengo chote kilipumzika bali kwa ombi la rais, wale wanaoaminika na Kamishina wapewe likizo isiyo na muda rasmi, nae akawachagua aliowaamini kuliko wengine wote.
“Siku mbili hizi nadhani kwa nyakati tofauti mlipata habari za kifo cha ghafla cha aliyekuwa naibu mkurugenzi wa usalama wa taifa bwana Kankono Malundi, alikufa kwa ajali ya gari.” Akanyamaza kidogo, akakohoa na kukwangua koo.
“Ukweli ni kwamba hakufa kwa ajali bali alitekwa na watu wasiojulikana, alitekwa muda mfupi baada ya kutoka kuonana na rais ambae hadi muda huu amelazwa kwenye hospital maalumu nje ya Ikulu. Kwa muda wote wanausalama wakihangaika kumtafuta bila mafanikio hadi mwili wake ulipookotwa kando ya nyumba yake ukiwa na majeraha mengi, simu na mkoba wake vyote havijapitakana hadi sasa. Kwa mujibu wa rais mwenyewe ni kwamba, alikuwa na taarifa muhimu aliyotakiwa kunifikishia na pengine taarifa hiyo ndiyo iliyochukua uhai wake.” Akameza mate na kuendelea.
“Mbali na taarifa hiyo lakini nyote mtakuwa mmeshitushwa na rais kutangaza kutaka kujiongezea muda wa kutawala, hili kila mmoja analipinga hata mimi nililipinga lakini hili ndilo chanzo cha kifo cha Kankono.” Alinyamaza baada ya kuona Honda anataka kusema kitu.
“Ni kweli rais anania hiyo?” Honda aliuliza.
“Ni yeye pekee anaeujua ukweli, lakini amenihakikishia huo ni mtego wake kwa watu waliowahi kumtega. Muda wa miaka miwili uliosalia ili aondoke madarakani anataka kuutumia kusafisha alichokichafua, hataki rais ajae awe ni aina ya rais kama yeye.” Alijibu.
“Umesema aliyetakiwa kukufikishia ujumbe aliuawa kabla hajafika kwako, yeye ni mgonjwa, amewezaje kukupa yote hayo?” Obimbo alimuuliza.
“Mengine alipata kunidokeza huko nyuma, mengine alinambia kupitia simu aliyowahi kunipa miaka minne iliyopita, simu kama hii, alinipigia usiku wa jana muda mfupi baada ya kutangazwa kifo cha Kankono.Ni mgonjwa ila si mgonjwa wa kushindwa kuongea.” Alijibu huku akinyooshea vidole simu mbili zilizokuwa mezani kwake.
“Kwa nini ametangaza kitu ambacho hana nia nacho?” Honda aliuliza.
“Unamuua vipi nyoka aliyeshimoni?” Kamishina nae akatupa swali kwa vijana wake.
“Unaweza kuwasha moto juu ya shimo ili apaliwe na moshi, kisha achague kufa kwa kukosa hewa safi au atoke umpige kichwa.” Honda alijibu.
“Hivyo ndivyo anavyotaka, anawachokoza waliolala ili waamke, awajue kwa rangi zao kisha awapige na kitu kizito.”
“Uhusika wetu ni upi kwenye mzozo huo?” Obimbo aliuliza.
“Anataka kusaidiwa na watu anaowaamini sana, kati ya watu hao alikuwemo Kankono lakini sasa nimebaki mimi na nyinyi tu, hamwamini hata mke wake.” Alijibu na kutulia kidogo ili kuwapa nafasi wenzake waelewe alikokuwa anataka kuelekea, alipohakikisha hakuna swali lingine akaendelea.
“Hii inaweza kuwa ni moja ya kazi ngumu sana kuliko zote tulizowahi kuzifanya, tunaenda kupambana na watu wenye nguvu kubwa kiasi kwamba wanamaamuzi juu ya rais, si watu wa mchezo hata kidogo. Wapo vitani na walishajiandaa kabla yetu, wapo kila mahali hadi kwenye ulinzi wa rais na sasa wametutangulia hatua moja kwa kumuua Kankono na hatujui watakuwa wamevuna mangapi kwake.” Alimeza mate na kuendelea.
“Vita yetu itafanikiwa endapo tutampata mtu mmoja aliyepotea miaka sita iliyopita, mtu huyo anaemfahamu ni rais pekee lakini amenipa ramani ya kumfikia..” Alisema huku akiiweka karatasi nyeupe mezani kwake, karatasi ile haikuwa imeandikwa kitu chochote kile, lakini waliokuwa kwenye ile ofisi hawakushangaa karatasi ya namna ile kuwa na ujumbe.
“Huyo mtu ni yeye pekee mwenye silaha za maangamizi kwa adui, akipotea huyo rais atakuwa hana namna zaidi ya kujiongezea muda wa kutawala, hivyo ili asiongeze inabidi huyo mtu apatikane akiwa hai. Nadhani mnaona rais kajiweka mtegoni pengine kwa kujua ama kutokujua na kwa kuwa sisi hapa wote hatuhitaji kumuona mtu akiifinyanga katiba yetu, lazima tumpate mtu huyo ili tuone rais atatengua kauli yake au ataiacha iishi, katega na sisi tunamtega.” Alisema huku akichukua kalamu ya mkaa na kuanza kuisugua juu ya karatasi iliyokuwa juu ya meza yake, akaendelea kufanya hivyo taratibu huku maneno yakimtoka kwenda kwa vijana wake wa kazi.
“Hatuombei huyo mtu kutopatikana, ila asipopatikana ina maana tutakuwa na kazi ya ziada na hatari zaidi pengine kuliko hii.” Alinyamaza lakini mikono yake iliendelea kuchorachora kwenye karatasi.
“Kumuondoa rais madarakani itakuwa ni zoezi gumu sana lakini itatulazimu. Kikubwa tusiwaze huko kabla hatujampata huyo kiumbe anaetembea na siri nzito zilizobeba uhai wa taifa.” Alinyamaza na kuiweka pembeni penseli kisha akaishika karatasi kwa mikono miwili na kuinua juu, akatabasamu kwa ushindi, karatasi ilikuwa imeonesha kile kilichofichwa.
“Ni ramani ya Mkoa wa Mara.” Alisema na kuwapa ile karatasi, Honda akaipitia kwa umakini mkubwa kisha akampa Obimbo ambae nae aliipitia kwa umakini kisha akaiweka juu ya meza.
“Mtu wetu yupo Buhemba, wilaya ya Butiama” Honda alisema.
“Ndivyo ilivyo, lakini si wa kufika na kumbeba kama kuku. Huyo mtu lazima ujitambulishe ili asikupe ugumu wowote, utambulisho wake ni utambulisho wetu sote hata kwa ambao hawapo hapa ila tunatarajia kuwatumia huko mbele ya safari.” Akanyamaza kidogo na kuwatazama namna walivyokuwa wametega masikio yao kwa umakini mkubwa, kitu muhimu kuliko vyote walitarajia kukisikia kutoka kwake.
“Jambo la kwanza mwambie AMKA, akikuuliza wewe ni nani mwambie unaitwa CASABLANCA, atakuuliza unashida gani, mwambie PANGA INATAKA MAKALI. Atakuuliza unaitwa nani kwa mara ya pili, mjibu unaitwa CASABLANCA1. Hili jina la mwisho lililoongezewa namba ni lake yeye kwenye harakati hizi ambazo rais amependekeza ziitwe harakati Casablanca.” Alimaliza kutoa maelekezo muhimu sana na yaliwaingia vema vijana wake wa kazi waliokuwa makini wakimsikiliza.
“Tutamtambuaje?” Honda aliuliza.
“Wanamuita Maneno, ni mchangamfu na mwongeaji sana kwa wenyeji wake. Mwonekano wake hakuna anaeujua zaidi ya rais mwenyewe, mtafuteni Maneno.” Alinyamaza kidogo na kuendelea baada ya kuona amepewa usikivu.
“Kila mmoja fungu lake limeshaingia kwenye akaunti yake, hakikisheni mnaenda leo hii Kwa sababu hatujui Kankono alisema nini na wao walimfanya nini.” Alisema huku akichukua simu mbili zilizokuwa juu ya meza akampa kila mmoja simu yake.
“Iwe kwa sauti au kwa ujumbe mfupi, hakikisha umekutana na maneno Casablanca kisha jina la mjumbe, naitwa Mamba.” Alimaliza huku akipiga meza mara mbili.
“Timamu mkuu!” Waliitikia huku wakiinuka na kusimama kwa heshima tofauti na mwanzo wakati wanaingia.
“Kanuni ni ileile, usimuamini mtu hata kivuli chako usikiamini.” Alisisitiza huku akiwapa ishara ya kuruhusu waondoke.
“Romeo!” Walijibu kwa pamoja kisha wakampa mgongo na kutokomea, walimuacha ofisini akiwa anakusanya karatasi zilizokuwa kando yake na kuziweka kwenye mkoba wake, akainuka na kusimama huku mkoba wake wa ngozi halisi ukiwa mkononi mwake, akajinyoosha kidogo na kupiga hatua kuufuata mlango, akaufungua na kutoka huku kichwani mwake akiwa hana wazo la kuelekea nyumbani kwake kwa jioni hiyo, kuna sehemu muhimu sana alitakiwa kufika kabla ya saa moja jioni. Wakati Kamishina akiiacha ofisi yake, Obimbo Mtei na Honda Makubi nao walikuwa wanagawiana majukumu, mmoja alitakiwa kusalia Dar es laam kufuatilia ni kina nani waliomuua naibu mkurugenzi wa usalama wa taifa huku mwingine akitakiwa kusafiri hadi kanda ya ziwa kumtafuta mtu asiyefahamika kwa sura wala jina lake kamili.
******



Tukutane hapa Ijumaa...
 
Muendelezo baada ya muda gani ama Pidiefu lipo kabisaa???
 
Kudo ww ni mkongwe kwenye izi kazi tafadhali kuwa tofaut na hawa wakuja mauongo kwenye ahadi zao, mi nishaachaga kusoma baadhi ya story za hawa magen z ata sifungui kabisa napita ivi nkaona kamanda kudo nkaja mbiombio nimeskitika mkuu ahadi ilikuwa ijumaa lkn Leo jtatu bado kimya
 
Bakers Mkuu.. we nisubir hapahapa! Nilitingwa kidogo
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…