Mzee Mwanakijiji,
Sidhani hatua kama hiyo, itasaidia kulimaliza tatizo la uchakachuaji wa kura unaodaiwa kufanyika wakati wa uchaguzi mkuu uliopita. Kama unavyofahamu, kisheria, 'he who asserts must prove' (tuseme anaye hakikisha, athibitishe).
Kwa hiyo, chini ya principle hii, utakuta kwamba CHADEMA (na wale wote wanaoamini uchakachuaji wa kura ulifanyika), wanaweza kutakiwa na Mahakama kuthibitisha kwamba, kweli CCM ilifanya hivyo i.e. ilichakachua kura; lakini hailekei CCM yenyewe, inaweza kutakiwa na Mahakama ithibitishe 'ushindi' wake, kwa kuwa haiupingi.
Lakini pamoja na hayo, ukweli ni kwamba kura zilihesabiwa na Tume ya Uchaguzi ambayo iliteuliwa na CCM, na wala hakuna hata mjumbe yeyote kutoka kambi ya upinzani (achilia mbali CHADEMA), aliyekuwepo wakati wa zoezi hilo.
Hii ina maana kwamba ni CCM, pamoja na taasisi zake, zinazohifadhi kumbukumbu muhimu ambazo CHADEMA ingelizihitaji kuthibitisha Mahakamani, uchakachuaji wa kura unaodaiwa.
Aidha, itakuwa ni juu ya CHADEMA kuiomba Mahakama iilazimishe serikali ya CCM kuzitoa takwimu hizo, ili CHADEMA iweze kuthibitisha kesi yake mbele ya Mahakama.
CHADEMA inaweza kuiomba Mahakama kuitaka serikali kufanya hivyo, kwa kuonyesha kwamba, swala zima, ni muhimu kufahamika vyema na kupata suluhu, kwa manufaa ya Taifa (public interest).
Vinginevyo, CCM inaweza kwenda mahakamani kudai CHADEMA, na wafuasi wake, wamtambue Rais aliyetangazwa na Tume ya Uchaguzi kuwa ni mshindi halali.
Lakini, amri kama hiyo, haiwezi peke yake kubadili hisia zilizokwisha jengeka katika mioyo ya baadhi ya wananchi kwamba kweli uchakachuaji wa kura ulitokea.
Kwa kukazia, hazipo nguvu za dola zinazoweza kubadili kilichomo mioyoni mwa baadhi ya wananchi wake, bali kujenga misingi mizuri, ya pande-husika kuaminiana.
Ni dhahiri kwamba msingi wa tatizo lenyewe, ni katiba ya Jamhuri ya Muungano. Katiba hii, haiwahami vya kutosha wanasiasa kutoka kambi ya upinzani. Isitoshe, ilitungwa muda mrefu, enzi za chama kimoja; na ina viraka vingi mno, vinavyokipa Chama-tawala upendeleo, kwa gharama za siasa za wakati huu i.e. za ushindani.
Nje ya hayo, katiba hii haitilii maanani mabadiliko ya kisiasa, na ya kijamii, yaliyotokea (na yanayoendelea kutokea) katika jamii yetu. La zaidi, ni katiba isiyotilia maanani kutokuwepo usawa (kikatiba) kati ya wananchi na Taifa lao (unequal power relationship between the State and its citizens). Bila ya kulishughulikia tatizo la katiba hii, serikali itaendelea kukumbana na matatizo (au malalamiko) ya namna hii, kila wakati.
Kwa upande mwingine, kama serikali itaendelea kupuuza malalamiko ya wananchi; malalamiko ambayo yanayotokona na dosari za katiba hii; inaweza kutafsiriwa na baadhi ya wananchi kwamba, serikali inafanya hivyo, maksudi, ili iendelee kuyahami maslahi ya wateule wachache, miongoni mwake.
Pamoja na kuwepo ushahidi unaoonyesha kwamba serikali ya Rais Kikwete, huko nyuma, ilishindwa kuzichukulia hatua nguvu zilizolihujumu, kiuchumi, Taifa analoliongoza, sidhani kwamba (Rais Kikwete) angelipenda kujenga, kuimarisha, na, au kuendeleza hisia hizi, miongoni mwa wananchi wake.