CHADEMA, CUF, NCCR walia faulo
na Nasra Abdallah
[Source Tanzania Daima]
VYAMA vya upinzani vimelalamikia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu, kuwa ni wa wizi mtupu baada ya baadhi ya wagombea wao kuenguliwa, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikitumia mbinu chafu kujipatia ushindi.
Vyama hivyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF).
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya CUF, jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema wagombea wa vijiji 104 wilayani Handeni mkoani Tanga wameenguliwa bila sababu za msingi.
Alisema wagombea kutoka vijiji hivyo, walienguliwa na Mkurugenzi wa wilaya hiyo kwa madai kuwa wamepiga mihuri katika ofisi za chama badala ya kata.
Kutokana na madai hayo, Profesa Lipumba alisema hawajaridhika na hatua hiyo, kwa kuwa sheria ya uchaguzi inamruhusu mgombea kupigiwa muhuri na ofisi za chama ili mradi tu awe ametimiza vigezo vinavyohitajika.
Pia katika mkutano huo, mwenyekiti huyo aliwaonyesha waandishi wa habari baadhi ya karatasi za kupigia kura ambazo alidai tayari CCM inazo, jambo ambalo alisema litavinyima haki vyama vingine vya siasa.
Hebu fikiria, hadi saa hizi, wenzetu tayari wanamiliki karatasi za kupigia kura, kitendo ambacho kinaweza kuwapa nafasi ya kuwapa watu mitaani ili wajaze na inapofika siku ya kupiga kura, wanakwenda tu kutumbikiza karatasi hizo, alisema Profesa Lipumba.
Kutokana na hali hiyo, alisema wanafanya taratibu na wanasheria wao ili kuweza kufungua kesi mahakamani kupinga vitendo hivyo.
Maeneo mengine ambayo CUF inalalamika kuchezewa rafu katika mchakato wa uchaguzi huo, ni pamoja na Wilaya ya Temeke, ambako mgombea wake Omar Lwambo katika Kata ya Tambukareli, alienguliwa kwa madai kuwa hajui kusoma na kuandika.
Lipumba alisema mgombea huyo alijaziwa fomu na mtu mwingine na baadaye aliweka saini, jambo ambalo alidai si kosa kwani hata yeye wakati akijaza fomu za kugombea urais, alijaziwa na mtu mwingine na baadaye aliweka saini yake.
Faulo hizo za uchaguzi, zinadaiwa pia kufanyika mkoani Tabora ambako Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Chemchem, amewapitisha wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wa Serikali za Mitaa Kata ya Chemchem waliodhaminiwa na Ofisi ya Katibu Kata CCM badala ya Katibu wa Tawi.
Lipumba alisema hali hiyo ni kinyume na kanuni za uchaguzi kwani mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa katika mamlaka za miji za mwaka 2009, zinasema mkazi yeyote wa mtaa anaweza kugombea uenyekiti wa mtaa au ujumbe ikiwa ni mwanachama na amedhaminiwa na chama cha siasa.
Malalamiko kama hayo, pia yalitolewa jana na CHADEMA baada ya mgombea wake, Yohana Kabiza kutishiwa kuuawa endapo ataendelea kufanya kampeni.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jijini Dar es Salaam jana, Kabiza anayegombea nafasi hiyo, Mtaa wa Migombani, Segerea, jijini Dar es Salaam, alisema vitisho hivyo vimetolewa na mmoja na wapinzani wenzake kutoka vyama vingine wanaowania kiti hicho.
Alisema kabla ya kupata vitisho hivyo, juzi majira ya saa 12 jioni alikuwa katika kituo cha daladala cha Kona akigawa vipeperushi kwa wananchi waliokuwa wakishuka kwenye daladala na ghafla akatokea mtu asiyemfahamu na kumnyanganya vipeperushi hivyo huku akidai yeye ni polisi.
Kabla hajaninyanganya vipeperushi hivyo, aliniambia nimpe nikakataa
alinitisha nikampa vipeperushi 20, aliendelea kuniambia nitampa vipeperushi nilivyobaki navyo au simpi na kusema yeye ni polisi, ndipo aliponinyanganya vingine 70, alisema Kabiza aliyemaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Nacho chama cha NCCR Mageuzi, kimelalamikia mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya watumishi wa serikali kutaka kuipatia ushindi CCM katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya ya chama hicho jijini Dar es Salaam, jana, Mkuu wa Idara ya Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Sengondo Mvungi, alisema CCM imekuwa ikitumia mtandao wa serikali kwani kuna ushahidi wa barua iliyokamatwa na chama hicho.
Alisema barua hiyo iliyoandikwa na katibu tawala kwenda kwa afisa uchaguzi wa wilaya, inamtuhumu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kasulo wilayani Ngara, Abdu Ngangula kwa kushindwa kumpigia kampeni mgombea wa CCM, hivyo anapaswa kuondolewa.
Kwa kweli inatia shaka na inaonyesha ni jinsi gani CCM ilivyoamua kuendesha demokrasia ya kihuni na hata ikitokea wameshinda uchaguzi, tunaamini ni kutokana na uhuni wanaoufanya, alieleza Dk. Mvungi.
Aidha alieleza kuwa matumizi mabaya ya vyombo vya dola, yamezidi kugubika, huku CCM ikifanya hivyo kwa kuelewa kuwa vyama vya upinzani vinaweza kususia.
CCM imekuwa ikitumia mtandao wa serikali kujua ni maeneo yapi hakuna wagombea, hivyo kujitangazia maeneo hayo kuwa ni washindi, alifafanua Dk. Mvungi.