Wanaopotosha ni wa CCM kwa sababu Mwenyekiti wao haelewi kitu na anapotosha kila kitu lakini nchi kubwa kama Tanzania wananchi wenye akili wanaelewa maana ya Utawala wa Majimbo na umuhimu wake. CCM walivyo wajinga wanachukulia neno Majimbo kuwa na maana ya kugawa nchi vipandevipande matokeo yake kuwagawa Watanzania vipandevipande kumbe Majimbo ni jina tu CHADEMA wangeweza kutumia Mikoa kama ilivyo sasa, Province ilivyokuwa kabla ya Uhuru, County ilivyo Kenya hata State ilivyo USA, maana ikawa hiyohiyo. Hata siku moja CHADEMA hawajasema watagawa nchi katika Majimbo wao wanasema wataleta Utawala wa Majimbo wala siyo wa kwanza kupendekeza mfumo huu wa Utawala nchini mwetu. Mwalimu Nyerere alikuwa wa kwanza kuona umuhimu wa Utawala wa Majimbo kuleta maendeleo sawa nchi nzima bila kupendelea maeneo fulanifulani kwa sababu yoyote ile ikiwa ni pamoja na wanakotoka viongozi. Nyerere, Mwenyekiti wa CCM,aliita Madaraka Mikoani (Decentralization, wasio wa CCM wanaelewa maana yake) lakini, kama ilivyo sasa, Wanachama wenzake ambao pia walikuwa Serikalini hawakuuelewa mfumo huu wa Utawala kwa hiyo utekelezaji wake ulishindikana. Kosa kubwa kabisa lilikuwa la kwake mwenyewe Rais na Mwenyekiti kwa kutoa hata hayo Madaraka nusunusu na kubakiza mengine kwake bila kupeleka Mikoani Madaraka na Mamlaka yote muhimu ili waweze kuamua mambo yao wenyewe. Rais akawa anaajiri na kuteua wafanyakazi wote muhimu na bajeti za Mikoa za matumizi tu, mapato yalikusanywa na Serikali Kuu, zilitayarishwa Mikoani na kuletwa Serikalini, zikipita baada ya kupunguzwa zilipelekwa Bungeni kupunguzwa zaidi. Rasimu ya Waryoba ya Katiba Mpya, kwa kutambua hali ya nchi yetu na kujali matakwa ya Wananchi, nayo ilipendekeza mfumo huu wa Utawala kilichotokea ni haohao CCM kwa kutoelewa walipinga kwa nguvu zote ndo maana hata Katiba yenyewe hatunayo hadi leo. Utawala wa Majimbo wanaopendekeza CHADEMA na wengine ina maana Majimbo, ndani ya maeneo yao, yatakuwa na Serikali zao kamili zikiongozwa na Watumishi ambao watachaguliwa na kufukuzwa au kuteuliwa na kutenguliwa au kuajiriwa na kutumbuliwa hukohuko bila Serikali Kuu kuhusika na watakusanya mapato yao na kupanga matumizi hukohuko. Serikali Kuu itakuwa ndogo kwa saizi lakini itakuwa juu ya Serikali zote za Majimbo kwa Madaraka na Mamlaka na ndo itatambulika Kimataifa na itaongozwa na Rais atakayechaguliwa na wananchi wote wanaokubalika kisheria akisaidiwa katika utendaji kazi zake na Mawairi na Watendaji Wakuu wengine. Ile Mihimili miwili mingine ya Mahakama na Bunge nayo itakuwepo na itapatikana kwa taratibu zitakazopangwa na kukubalika. Inaposemwa kuwa kutakuwa na Mabunge ya Majimbo, CCM wanafikiri yatakuwa makubwa kama Bunge la Ndugai la ndiyoooo na kupiga meza lakini yatakuwa na Wabunge 20 au 30 kutegemea ukubwa wa Jimbo ambayo yatatuwa jumla Majimbo labda 10 au 15 tu. Umuhimu na kuhitajika kwa Utawala wa Majimbo
umeonekana sana Awamu hii ambapo mtu mmoja tu amekuwa anaamua kutumia fedha za walipakodi wa huku kutekeleza miradi isiyo kipaumbele ya kule. Uwanja wa Chato usingejengwa kama Serikali yao ya Jimbo ingewataka wananchi wa Chato wagharamie huo ujenzi huku wao wanashida kubwa ya maji ingawa Ziwa lipo karibu.