CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Kanda ya Serengeti kimelaani vikali matukio ya utekaji kuendelea hapa nchini yakihusisha viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, kwamba vitendo hivyo vinaleta hofu kubwa kwa jamii.
Hayo yamebainishwa jana na Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti Jacksoni Mnyawami, inayounganisha Mkoa wa Shinyanga,Mara na Simiyu, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Kanda hiyo Mjini Shinyanga.
Amesema matukio ya utekaji ambayo yanaendelea hapa nchini siyo afya njema kwa taifa letu,huku akiwataja watu ambao wanadaiwa kutekwa, kuwa ni kiongozi wa hamasa wa Chadema jimbo la Tarime vijijini, Mussa Juma, na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Daniel Chonchorio, ambaye pia ni mtia nia wa Ubunge jimbo la Tarime Mjini.