WACHEZAJI 23 wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars wameondoka leo alfajiri kwenda Abidjan, Ivory Coast tayari kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa Ligi za Ndani, CHAN.
Tanzania ni kati ya timu zinazoshiriki fainali hizo ikiwa Kundi A pamoja na wenyeji Ivory Coast, Zambia na Senegal. Tanzania itaanza kucheza Jumatatu dhidi ya Senegal. Kundi B lina timu za Congo, Zimbabwe, Libya na Ghana.
Kikosi hicho kitakachoongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Muungano, Muhammed Seif Khatibu.
Wachezaji wa Stars waliagwa juzi usiku kwenye Hoteli ya New Africa walipoandaliwa chakula cha usiku na wadhamini wa timu hiyo, Kampuni ya Bia ya Serengeti na Benki ya NMB.
Akizungumza baada ya kutaja kikosi hicho juzi wakati timu hiyo ilipokuwa ikikabidhiwa bendera ya taifa , kocha mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo alisema mafanikio waliyoyapata wachezaji wa timu ya taifa yanasaidia kujenga kizazi kijacho cha wachezaji mpira wa miguu nchini.
Maximo alisema ili timu hiyo iweze kufanya vizuri inahitaji ushirikiano mkubwa nje na ndani ya uwanja kwani yeye ameijenga timu kushirikiana ndani ya uwanja.
Alisema wachezaji ambao amewachagua kwenye timu ya taifa lakini hataenda nao Ivory Coast alifanya hivyo ili kuwapa motisha na kwamba anajua atakuja kuwatumia au wanafaa kutumika katika timu ya Taifa kwa hiyo wasikate tamaa bali waendelee na mazoezi kwani mafanikio ya Stars ni mwanzo wa kukua na kujulikana soka la Tanzania kimataifa.
Wachezaji walioachwa ni Omary Pazi, Jabir Aziz, Salvatory Ntebe na Uhuru Suleiman.
Maximo alisema timu yake haiendi Ivory Coast kushiriki tu, bali wanakwenda kushindana na Watanzania wategemee kuona kandanda safi na yenye matokeo mazuri kwani TFF na wadhamini wanaoisaidia timu wameshirikiana vya kutosha.
Naye Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Joel Bendera akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi bendera alisema wachezaji wanatakiwa wajenge imani ya ushindi na kuwa timu yao ni nzuri na wanategemewa na wanawakilisha Watanzania zaidi ya milioni 36.
Bendera alisema katika timu hiyo ya taifa kuna wachezaji wazembe ambao wanacheza mpira kwa asilimia 60 tu, wengine asilimia 90 wakati wanatakiwa wasakate kabumbu kwa asilimia 100.
Waziri Bendera alisema wachezaji lazima wajenge ari wawe timamu kisaikolojia na morali ya hali ya juu ili kupata ushindi katika mashindano hayo ya CHAN.
Wachezaji watakaokwenda Ivory Coast ni makipa: Farouk Ramadhan, Shaaban Dihile, na Deogratius 'Dida' Boneventure wakati mabeki ni Shadrack Nsajigwa (nahodha), Salum Sued, Nadir 'Canavaro' Haroub, Juma Jabu, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, na Amir Maftah.
Viungo ni Henry Joseph, Godfrey Bonny, Nurdin Bakari, Shaaban Nditi, Athuman Idd, na Mwinyi Kazimoto wakati washambuliaji ni Mrisho Ngassa, Jerry Tegete, Kigi Makasy, Abdi Kassim, Haruna Moshi, Mussa Mgosi na Nizar Khalfan.
Katika hatua nyingine Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars walichangishana zaidi ya kiasi cha dola za Marekani 95,000 kwa ajili ya shughuli maalum za kuisaidia timu ya Taifa.
Mwenyekiti wa kamati ya ushindi ya Stars, Mohamed Dewji alitoa dola za Marekani 20,000, Dosa na Tanil Somai dola 15,000, Kobil 15,000, Fayaz 15,000, Abji 10,000, NMB 10,000, SBL 10,000, Sanjai 10,000, Azim Dewji 5,000 na Kassim Dewji ambaye naye alitoa dola 5,000.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Leodegar Tenga alisema mbali na fedha hizo zilizochangwa, kamati hiyo imeshatumia kiasi cha milioni 250 katika kuisaidia huduma mbalimbali za timu ya taifa.
Tenga alisema Stars imekaa kambini kwa wiki 61 tangu Machi 2006 na imecheza mechi 41 chini ya Maximo, kushinda 18, sare 13 na imepoteza 10. Alisema Stars katika kipindi hicho imetumia zaidi ya bilioni 1.6 ambazo ilizipata kutoka kwa wadhamini wake ambao ni Serengeti na NMB.
Tenga aliongeza kuwa Taifa Stars katika kipindi cha kocha Maxio Maximo imecheza jumla ya mechi 41 imeshinda 18 imetoka sare mechi 13 na imefunga magoli 48.
Alisisitiza kuwa matarajio ya Watanzania kwa Taifa Stars ni wachezaji na viongozi watakuwa mabalozi wazuri na wataonyesha nidhamu ndani na nje ya uwanja, pili Watanzania wanatarajia kuona mchezo mzuri na wa ushindi na tatu ni timu isiende kushiriki tu bali timu yetu ionekane ikishindana.
Katika hafla hiyo, mdau mmoja wa soka aitwaye, Murtazar Mangungu aliahidi kuwa kila atakayefunga goli kwenye michuano ya CHAN atampa dola 50
Source: Gazeti la Mwananchi