SoC02 Changamoto, fursa, teknolojia na umuhimu kurasimisha sekta isiyo rasmi kukuza ajira, kuongeza mapato na kuondoa umaskini Tanzania

SoC02 Changamoto, fursa, teknolojia na umuhimu kurasimisha sekta isiyo rasmi kukuza ajira, kuongeza mapato na kuondoa umaskini Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

TKAI

New Member
Joined
Sep 10, 2022
Posts
1
Reaction score
0
MUHTASARI
1. Marekebisho ya sera za uchumi (SAPs) yaliyoanzishwa na Shirika la Fedha (IMF) na Benki ya Dunia (WB) kwa nchi maskini, na hasa Afrika katika miaka ya 80 na 90, kutokana na matatizo ya uchumi yalipendekeza kupunguza ushiriki wa sekta ya umma kwenye shughuli za uchumi ili kuiachia sekta binafsi kuendesha uchumi. Ni kutokana na maelekezo haya pamoja na ugumu wa sheria na viwango vikubwa vya kodi tofauti na mapato halisi; iliibuka sekta mpya, SEKTA ISIYO RASMI. Katika Makala ya Shadow Economies, Profesa Schneider anasema, athari hasi za sekta isiyo rasmi ni kubwa kiuchumi na kisiasa zikiwemo mapato ya serikali kuwa kidogo, huduma za jamii zisizokidhi mahitaji na serikali kupoteza imani kwa watu wake. Hivyo, ni muhimu sekta hii kutambuliwa, kuthaminiwa na kurasimishwa ili ichangie kukuza uchumi. Ubunifu unahitajika katika urasimishaji ili kuondoa kero kwa sekta isiyo rasmi kunyanyaswa kwa kigezo cha kuvunja sheria za jiji, miji au Kijiji.

2. Sekta isiyo rasmi ni Wananchi wanaofanya kazi za biashara ili kujikimu nje ya mfumo wa kodi na usimamizi wa serikali, kama wakulima, wafanya biashara ndogo ndogo mijini na vijijini, Mama Lishe, Machinga, boda boda; n.k.
UTANGULIZI
3. Hapa Nchini, asilimia 53.7 (Jedwali Na. 1) ya pato la Taifa inatokana na sekta isiyo rasmi. Kwa maana hiyo pato letu la ndani, kwa sehemu kubwa linachangiwa na sekta isiyo rasmi. Hivyo basi, sekta hii ina mchango mkubwa kushinda sekta za umma na sekta binafsi tofauti na matarajio ya IMF na WB. Kwa hali hii, suala la kurasimisha sekta isiyo rasmi si tu kipaumbele ni suala la lazima na halikwepeki. Urasimishaji ukifanikiwa, unapanua wigo wa kodi na kuwezesha kushusha viwango vya kodi.​

Jedwali 1.._page-0001.jpg


4. Taarifa za kila mwaka kutoka Global Competitiveness, taasisi ya Jukwaa la kiuchumi la Dunia (WEF) zinaeleza kuwa, ukuwaji imara wa uchumi kwa nchi za dunia ya tatu ikiwemo Tanzania unategemea sana uwezo wa kutumia rasilimali zilizopo hasa ardhi kwa kiwango cha juu ili kufikia uchumi imara na shirikishi. Kwa ukweli huu, ili tufaidike na rasilimali zetu kwa kiwango kinachotakiwa, kurasimisha sekta isiyo rasmi ni jambo muhimu, na ili urasimishaji ufanikiwe ni kurasimisha kilimo ili kituwezeshe kutumia ardhi na nguvu kazi kwa kiwango kinachostahili. Hii ni kwa sababu kilimo kinaweza kutengeneza nafasi nyingi za ajira, kuongeza mapato ya serikali na kuharakisha juhudi za kuondoa umaskini.​

HALI HALISI
5. Ufumbuzi kurasimisha sekta isiyo rasmi bado ni kizungumkuti, kila kinachoanzishwa ili sekta hii iingie kwenye mkondo rasmi wa uchumi hakileti matokeo tarajiwa. Mfano, sote tunakumbuka habari za vitambulisho vya machinga na kilichotokea. Ni vema kujua sekta hii ni tishio kwa wanasiasa, pia ni ngazi yao kupanda juu kwa gharama ya kufanya mambo machache hata kama hayaleti badiliko lolote na wakipata wanachotaka sekta inatelekezwa hadi kipindi tishio linaonekana kukwamisha matarajio yao, yanaibuka mazingaombwe mapya. Hatuna budi kutoka huko, zimamoto hazitatusaidia, vyema tupate ufumbuzi wa kudumu kwa tatizo hili.

6. Sote tunajua, rasilimali pekee inayopatikana kwa wingi sehemu kubwa nchini ni ardhi nzuri kwa kilimo na ufugaji. Hapa ndio pana jibu la CHANGAMOTO ZA SEKTA ISIYO RASMI IKIWEMO KUTOKUWEPO MITAJI KUFANYA BIASHARA. FURSA PIA ZIKO WAZI; UKUBWA WA SEKTA ISIYO RASMI WENGI WAO WAKIWA NI WAKULIMA NA UWEPO WA TEKNOLOJIA NA MTAJI KUFANYA MAPINDUZI YA KILIMO KUFANIKIWA.
7.
Kupitia MAPINDUZI YA KILIMO kunawezesha mazingira muafaka kwa MAPINDUZI YA VIWANDA kufanyika kwa ajili ya usindikaji na utengenezaji bidhaa kutokana na mazao ya kilimo. Mapinduzi haya yanavutia vijana wengi kuingia kwenye kilimo tofauti na sasa ambapo kilimo kimeachiwa wanawake na wazee.

SULUHISHO
8. Suluhisho la kurasimisha kilimo linajengwa kwa kutambua mapinduzi ya kiteknolojia yaliyofikiwa, mfano kwa sasa hapa Tanzania takribani watu 56.2 millioni wanamiliki simu za mkononi. Teknolojia inatoa majibu kwa changamoto nyingi za kimaendeleo ikiwemo kilimo. Urasimishaji utakipa sura mpya kilimo chetu, sambamba na motisha kutoka kwa serikali kutoa vitambulisho vya kazi kwa wakulima na kuwaingiza kwenye mfumo wa bima ya afya na mafao kama watumishi wa umma.

9. Urasimishaji unafanyika Kupitia programu tumishi (mobile app) kwa simu za mkononi kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya kilimo; Serikali, wakulima, wasindikaji, wasafirishaji, wamiliki wa matrekta, watafiti, bodi za mazao, halmashauri za wilaya, wasambazaji mbegu na viuwatilifu, Vyama vya msingi, mabenki, taasisi hali ya hewa, maafisa ughani, mifuko ya jamii na makampuni ya simu.
Jedwali 2_page-0001.jpg


MAPENDEKEZO
10. Mfumo imara wa uwezeshaji wakulima unahitajika, serikali kupitia halmashauri za wilaya ielekeze kuwa zile 10% kwa ajili ya makundi maalum, 8% zitolewe kwa wakulima. Sifa za kijana kuingia kwenye urasimishaji ni, awe anamiliki shamba kuanzia ekari 3 hadi 5 lenye hati ya matokeo ya vipimo vya udongo kutoka kwa afisa ughani aliyethibitishwa. Uwezeshwaji ugharimie kulima kwa kutumia trekta, mbegu, mbolea, madawa, palizi na vifungashio mazao. Kuwepo makadirio halisi ya gharama za uwezeshaji kwa kipimo cha ekari moja na aina ya zao analolima mkulima. Muda wa uwezeshwaji uwe kwa vipindi viwili vya misimu ya kilimo baada ya hapo, mkulima apewe namba ya mlipa kodi, uanachama hifadhi ya jamii na bima ya afya.

11. Wakulima watambuliwe kupitia majina, jinsia, picha, alama za vidole, namba za simu, maeneo wanamoishi (vijiji, vitongoji), vyama vyao vya msingi, aina ya zao na eneo analolima. Kila Mkulima aliyesajiliwa anapewa kadi yenye taarifa zote zinazotumiwa na wadau wengine kumhudumia.

12. Halmashauri ziweke kanuni na masharti rafiki kusimamia urasimishaji huu kwa njia ya uwazi.
Jedwali 3_page-0001.jpg

MATOKEO
Urasimishaji ukifanikiwa utaleta matokeo yafuatayo;

(a) Kupunguza ongezeko la sekta isiyo rasmi na kukuza sekta binafsi.

(b) Kuimarika hali ya usalama wa chakula nchini na Uchumi kukua kwa kasi zaidi

(c) Kuongeza ajira, wigo wa mapato na Kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa

(d) ongezeko thamani ya mazao na bidhaa za nje, ili kupunguza nakisi kati ya thamani ya bidhaa tunazonunua kutoka nje mfano mafuta ya kupikia na thamani ya bidhaa tunazouza nje kupunguza utegemezi.

(e) Kuandaa viongozi na raia wema wanaojua changamoto tulizo nazo na wanashiriki kwa vitendo kuzitatua.

Asanteni!
 
Upvote 0
Back
Top Bottom