Chanzo cha anguko la elimu katika shule za msingi ni walimu kufanya kazi ya bodaboda?

Chanzo cha anguko la elimu katika shule za msingi ni walimu kufanya kazi ya bodaboda?

HOBBIES

Senior Member
Joined
Dec 29, 2011
Posts
145
Reaction score
17
Waalimu wa shule za msingi wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza wamekuwa chanzo cha kufanya vibaya kwa wanafunzi wao kutokana na kujihusisha zaidi na kazi ya kuendesha pikipiki za kubeba abiria maarufu kama bodaboda wakati wa saa za kazi.

Taarifa hiyo iliyoripotiwa na gazeti hili jana ilidai kuwa walimu wanaojihusisha na biashara ya bodaboda wamechangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa ufaulu mbaya wa wanafunzi wao wa darasa la saba waliohitimu mwaka 2013.

Walioibua malalamiko hayo ni baadhi ya wananchi wa Sengerema ambao walijitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Ikoni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo mbunge wa jimbo la Sengerema.

Ilielezwa zaidi kuwa wananchi wamekuwa wakilalamikia tabia ya walimu hao kupitia kwa viongozi mbalimbali lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kusitisha tabia hiyo na kwamba, chanzo cha kuendelea kuwapo kwa hali hiyo ni matokeo ya kulindana.

Afisa Elimu wa Wilaya ya Sengerema alikiri kuwahi kupokea malalamiko hayo. Hata hivyo, baadhi ya walimu, akiwamo mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Bazirasoga wamekuwa wakipinga kwamba hujihusisha na kazi ya kubeba abiria nyakati za kazi.

Walikiri kwamba ni kweli wapo walimu wanaomiliki bodaboda lakini huzitumia kwa biashara wakati wa siku za mapumziko na siyo saa za kazi.

Siyo nia yetu kutaka kujua kwa undani kuwa ni nani mkweli baina ya wananchi wa Sengerema waliotoa malalamiko mbele ya mbunge wao au walimu. Bali, tunachoamini ni kwamba kweli, wapo walimu wanaoendesha bodaboda ili kujiingizia kipato. Kinachobishaniwa ni muda tu wa saa za kufanya kazi hiyo ya ziada; wananchi wakiwatuhumu walimu kuwa huacha kufundisha na kwenda kutafuta abiria wa kuwabeba huku walimu wakijitetea kwamba hufanya kazi hiyo katika saa zisizokuwa za kazi.

NIPASHE tunaamini kwamba mambo yote mawili hayako sawa. Hatuamini hata kidogo kwamba ni sahihi kwa walimu wa shule kujihusisha moja kwa moja na kazi ya kuendesha bodaboda.

Hii ni kutokana na hofu yetu kuwa misingi ya haiba ya ualimu haitoi mwanya huo. Hatuamini hata kidogo kuwa, mwalimu anayejihusisha moja kwa moja na kazi ya kuendesha bodaboda anaweza kutekeleza vyema majukumu yake ya kufundisha na kueleweka mbele ya wanafunzi wake darasani.

Kwa mfano, hatuamini kuwa mwalimu aliyeonekana na wanafunzi wake akiwa mahala kugombea abiria ataeleweka darasani wakati akiwa darasani. Ni kwa sababu kisaikolojia, wanafunzi wanaweza kupungukiwa na imani dhidi ya mwalimu wa namna hii kutokana na asili ya kazi ya ziada anayojihusisha nayo.

Ieleweke vizuri kwamba, kwa kukumbushia hili, hatumaanishi kuwa kazi ya kuendesha bodaboda ni mbaya na haifai kabisa kufanywa na walimu. La hasha. Sote tunajua umuhimu wa bodaboda kwa jamii.

Tunajua vilevile kuwa, vyombo hivi vya usafiri ni chanzo kizuri cha kipato na hivyo kila Mtanzania ana haki ya kutumia fursa hii kwenye eneo alilopo pindi akiona inafaa na kwamba, hakiuki sheria za nchi.

Changamoto nyingi binafsi za walimu zinaweza kusaidiwa kwa kiasi kikubwa na vyombo hivi pindi wenyewe wakiamua kuwa wajasiriamali waliojiingiza katika shughuli hii. Hilo halina shida.

Bali, tunachoamini kwamba hakiko sawa ni kwa walimu wenyewe kufanya shughuli hiyo badala ya kuwapa vijana na wao kama wamiliki kubaki kuwa wasimamizi wa biashara hiyo. Kama tulivyogusia, ualimu ni kazi tofauti kidogo. Inahitaji sana kuzingatia weledi na moja ya sifa muhimu ni kulinda haiba ya mwalimu. Namna ya kuvaa, nguo za kuvaa, miondoko, kauli na hata kazi za ziada za mwalimu zinapaswa kulinda haiba yake.

Sisi tunaamini kuwa kinyume chake, kama mwalimu atapuuzia haiba ya ualimu, anaweza kujikuta akiwa miongoni mwa wale wanaotenda dhambi mbaya ya kuzika kiwango cha elimu.

Kuendesha bodaboda ni miongoni mwa kazi za ziada ambazo tunadhani kwamba hazilindi haiba ya mwalimu. Biashara hii ya bodaboda inaweza kuwa chanzo kizuri cha mapato ya walimu.

Hata hivyo, inaweza kuwa chanzo cha kushuka kwa kiwango cha elimu, na hasa inapobainika kwamba ni kweli kuna baadhi ya walimu hutelekeza wanafunzi wao ili wakagombee abiria kwenye vituo vya mabasi.

Shime, mamlaka za elimu nchini zichukue hatua sahihi za kuzuia walimu wa Sengerema na maeneo mengine nchini kujihusisha moja kwa moja na kazi ya udereva wa bodaboda kwani kuruhusu jambo hilo ni kubariki kifo cha elimu.


CHANZO: NIPASHE
 
Mkitaka tuache ongezeni mishahara sio pesa zote mnapeleka Dodoma na sie tunapenda bata,mtapiga kelele sana ila nikipata kichwa nakula mda usio wa kazi na haiba bongo haipo,Haiba iko Ulaya
 
Pesa za kula na kuvaa tunazo. tunataka pesa za maendeleo. Mtu kama mimi nnavipindi 52 kwa wiki, na mshahara ni ule ule, zaidi zaidi sipati motisha ya aina yeyote, nnajitahidi kufundisha kadri ya uwezo wangu lakini wakati mwingine nnachoka, na nnatiwa uvivu nnapoona wenzangu ( walimu wengine) wana vipindi chini ya 6 kwa wiki, so mda mwingi wanapiga stori tu na kuniachia shule peke yangu.

Any way this is Tz for Tz, ninalazimika kuangalia kazi mbadala ya kufanya ili niongeze kipato zaidi.
 
Posho mjiongezee nyie! mishahara mizuri nyie! sitting allowance na bajet za chai kwny ofc zenu!
Mitaala mibovu mnatengeneza nyie! vitabu vyenye matango pori mnaptisha nyie!! watoto wanafeli mnaleta kigezo hafifu eti tunaendesha bodaboda!!. Mnahtaj maombi
 
Na sio walimu wote wanaondesha boda,ni wachache sana
 
Mm nina jamaa yangu ambaye ni Mwalimu alikaa mwaka mzima hajaingia darasani anafanya mambo yake mengine ya kiuchumi.Si bora hao ambao hata japo wanaripoti kazini.Walimu wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la tatu.
 
Posho mjiongezee nyie! mishahara mizuri nyie! sitting allowance na bajet za chai kwny ofc zenu!
Mitaala mibovu mnatengeneza nyie! vitabu vyenye matango pori mnaptisha nyie!! watoto wanafeli mnaleta kigezo hafifu eti tunaendesha bodaboda!!. Mnahtaj maombi
Waambie wamezidi
 
Back
Top Bottom