BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
Chenge aandaliwa mashitaka ya rada
Mwandishi Wetu Aprili 1, 2009
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
Adokezwa aandae wadhamini wake
Lengo ni kumuepusha asiende lupango
Mwandishi Wetu Aprili 1, 2009
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
Adokezwa aandae wadhamini wake
Lengo ni kumuepusha asiende lupango
BAADA ya kupandishwa kizimbani kwa kesi ya kusababisha ajali iliyoua watu wawili, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa serikali Andrew Chenge, sasa anatarajiwa kufunguliwa mashitaka kuhusiana na tuhuma za rushwa katika ununuzi wa rada ya kijeshi yenye thamani Sh bilioni 40 inayomkabili na vigogo wenzake kadhaa, imefahamika.
Habari za uhakika zimeeleza kwamba, pamoja na kuwapo juhudi kubwa za kuzuia mashitaka dhidi ya wahusika wakuu wa sakata hilo linaloigusa kwa karibu serikali ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kesi hiyo itafunguliwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kutokana na msukumo mkubwa wa kisiasa.
Rada hiyo ya kijeshi iliyonunuliwa kwa Pauni za Uingereza milioni 28 , iliibua utata mkubwa lakini kasi kubwa iliongezeka baada ya makachero wa uingereza wa kitengo cha Serious Fraud Office (SFO) kubaini kuwapo kwa rushwa kubwa iliyohusisha kampuni ya Uingereza ya BAE System na wanasiasa, watendaji na wafanyabiashara wa Tanzania.
"Hakuna kitakachozuia kushitakiwa kwa watuhumiwa wa sakata la rada akiwamo Chenge kwa kuwa kuna kila aina ya ushahidi, pamoja na kuwapo kwa vikwazo kadhaa. Wenzetu wa SFO wanafanya kazi kwa maslahi yao zaidi na hapa nyumbani kuna wanaojaribu kuwasaidia watuhumiwa, lakini ni suala la wakati tu kwa sasa," kinaeleza chanzo chetu karibu na serikali.
Chanzo hicho kiligusia kuwapo kwa ukabila katika kulindana kutokana na kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Elieza Feleshi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea kutoka sehemu moja na Chenge, lakini wote wamekwisha kukanusha kupitia gazeti moja la kila wiki (si Raia Mwema) kufanya kazi kwa ukabila.
Awali ilielezwa kwamba mwishoni mwa wiki, Chenge alijulishwa kuhusiana na maandalizi ya kesi dhidi yake, akihusishwa na rushwa ili aweze kuandaa wadhamini, lakini taarifa hizo zimekanushwa vikali na pande zote zinazohusika wakiwamo watu walio karibu na mwanasiasa huyo ambaye amekuwa gumzo kwa muda mrefu sasa kutokana na kuhusishwa kwake na sakata hilo.
Tayari imethibitishwa pasi shaka kwamba Watanzania wane wazito wametajwa kuwa watuhumiwa wakuu wa sakata la rada, huku nyuma yao kukiwa na watendaji kadhaa wa idara na asasi nyingine za serikali walioshiriki katika mchakato huo kabla na wakati wa ununuzi wake.
Waliotajwa moja kwa moja na nyaraka rasmi pamoja na Chenge yumo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Idriss Rashidi, ambaye wakati wa mchakato huo alikuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kabla ya kustaafu na kuingia katika sekta binafsi.
Baada ya kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Mkapa kwa miaka kumi, mwaka 2005 Chenge aliwania ubunge jimbo la Bariadi Magharibi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuteuliwa kuwa Waziri wa Afrika Mashariki kabla ya kuhamishiwa wizara ya Miundombinu, ambako alilazimika kujiuzulu kutokana na kashfa ya rada.
Chenge alilazimika kujiuzulu nafasi yake baada ya kutajwa hadharani kuhusika kwake na ununuzi wa rada na kubainika kumiliki akaunti nje ya nchi yenye kiasi kikubwa cha fedha ambazo yeye aliziita kuwa ni ‘vijisenti.'
Kwa upande wake, Dk. Rashidi, baada ya kuondoka BoT mwaka 1998, aliingia katika sekta binafsi ikiwamo benki ya Akiba Commercial, Vodacom Tanzania na benki ya NMB kabla ya kuteuliwa tena kuongoza Tanesco aliko hadi sasa.
Watuhumiwa wengine wawili wakuu waliotajwa ni pamoja na mtuhumiwa mkuu ambaye kwa sasa amekimbilia nje ya nchi Shailesh Pragji Vithlani na mshirika wake mkuu kibiashara Tanil Somaiya.
Chenge, Dk. Rashidi, Vithlani na Somaiya wote wametajwa kuwa washiriki wakuu waliowaongozwa wengine katika kufanikisha biashara hiyo tata kwa upande wa Tanzania kila mmoja kwa sasa amekwisha kuchunguzwa kuhusiana na suala hilo.
Wakati Chenge alishiriki kwa kiasi kikubwa kama Mtaalamu wa sheria, Dk. Rashidi ametajwa kushiriki kama mtaalamu na mhusika mkuu wa mambo ya fedha akiwa Gavana wa BoT.
Taarifa zinaonesha kwamba Vithlani na Somaiya walikuwa na hati za kiapo zenye kuwapa mamlaka ya kisheria kuwakilisha kampuni iitwayo Envers Trading Corporation.
Uchunguzi unaonyesha kwamba Envers Trading ililipwa dola za Marekani milioni 12 na kampuni nyingine iitwayo Red Diamond Trading, iliyofunguliwa mwaka 1998 katika visiwa vya Virgin ambavyo ni sehemu ya dola ya Uingereza.
Red Diamond Trading ilikuwa na uhusiano mkubwa na kampuni iitwayo BAE Systems, ambayo ilitengeneza na kuuza rada iliyouziwa serikali ya Mkapa mwaka 2002.
Imedaiwa kwamba Red Diamond iliweza kujinufaisha kwa kutumia mianya ya kisheria katika visiwa vidogo vya Caribbean ambako kampuni kama hiyo zinaweza kuficha taswira ya akaunti zake benki ikiwa ni pamoja na majina ya wamiliki wake.
Akihojiwa na wapelelezi wa Uingereza, Somaiya, ambaye anamiliki kampuni ya Shivacom ya mjini Dar es Salaam, alikiri kuwa na hati zao za kiapo zenye kuwapa mamlaka ya kisheria kuwakilisha kampuni iitwayo Envers Trading Corporation kwa miezi 11.
Somaiya alikiri katika mahojiano hayo kwamba yeye na "rafiki yake mkubwa" Vithlani wanamiliki kwa pamoja kampuni iitwayo Merlin International.
Hata hivyo, nyaraka za SFO zinaonyesha kwamba Somaiya kupitia kwa wakili wake aliiambia Takukuru kwamba aliacha kuwa mwenye hisa na mkurugenzi wa Merlin International kipindi ambacho tayari biashara ya rada ilikuwa imekwisha kamilika.
Kwa sasa Vithlani pekee ndiye anayetafutwa na ameshitakiwa kwa kutoa taarifa za uongo kuwa sio mmiliki wa Envers Trading na kuhusu kupokea dola 390,000 kwa biashara ya rada wakati ukweli ni kwamba alilipwa kitita cha dola milioni 12.
Tayari makachero wa Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Mazito ya Uingereza (Serious Fraud Office-SFO) wamekwisha kuomba ushirikiano wa wenzao wa Tanzania katika kuwahoji na kuwapekua watuhumiwa wakuu wa sakata hilo.
Tayari SFO kwa kushirikiana na vyombo vya dola vya Tanzania, Uswisi na Ufaransa wamebaini kuwapo kwa Dola za Marekani milioni 12 (Sh. bilioni 13.8), ambazo zililipwa kwa siri kwa maofisa wa juu wa serikali kupitia Vithlani kama kamisheni, fedha zilizolipwa kupitia benki ya Uswisi.
Imefahamika kwamba umepatikana ushahidi mzito wa kuthibitisha malipo yaliyofanywa na British Aerospace Engineering (BAE) kuwa ni hongo kwa wale waliopitisha ununuzi huo, malipo yaliyofanywa wakati wa utawala wa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.
BAE ilifanya mipango miwili tofauti na Vithlani ambapo kwanza, makubaliano ilikuwa ni kusaini malipo ya kamisheni ya asilimia moja, baada ya kupitishwa kwa ununuzi wa rada wa Dola za Marekani milioni 40.
Mwezi mmoja baada ya kupitishwa kwa ununuzi huo na serikali, BAE iliilipa kampuni ya Merlin International Ltd hapa nchini, jumla ya Dola za Marekani 400,000.