BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
Chenge alipuliwa upyaa...!
2009-03-18 00:07:10
Na Emmanuel Lengwa, Jijini
2009-03-18 00:07:10
Na Emmanuel Lengwa, Jijini
Wakati uchunguzi dhidi yake kuhusiana na tuhuma za kuhusishwa na rushwa itokanayo na manunuzi ya rada ya bei mbaya wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ukiendelea, Mbunge wa Bariadi Mashariki, Bw. Andrew Chenge amejikuta akilipuliwa tena upya.
Mheshimiwa Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa Serikali ya awamu ya tatu iliyokuwa ikiongozwa na Rais Benjamin Mkapa, hivi sasa anadaiwa kuwa ndiye aliyeshiriki kuianzisha kampuni inayodaiwa kuwa ya kifisadi ya Meremeta Gold.
Aliyemlipua Mheshimiwa Chenge, ni Mbunge wa Jimbo la Karatu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa.
Akizungumza na Alasiri leo asubuhi, Dk. Slaa amedai kuwa Chenge ndiye aliyeisajili kampuni inayokabiliwa na tuhuma za kifisadi ya Meremeta Gold.
Akadai kuwa Chenge, akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alishiriki kuianzisha kampuni hiyo ya Meremeta, kwa kwenda kuisajili katika kisiwa kilekile cha New Jersey nchini Uingereza, ambacho anadaiwa vilevile kuwa ndiko alikoficha mapesa anayotuhumiwa kuyapata kupitia dili la rada yanayofikia kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni moja. Hata hivyo, Chenge aliwahi kuziita pesa hizo kuwa ni vijisenti.
Katika madai hayo mapya yaliyotolewa na Dk. Slaa, ni kwamba licha ya kuwa mwanzilishi, Chenge ndiye Mkurugenzi wa kwanza wa Kampuni hilo la Meremeta, linalodaiwa kuitia losi Serikali ya Tanzania ya zaidi ya shilingi bilioni 155.
Dk. Slaa amesema sasa, yeye na wenzie CHADEMA ambao wako kwenye `Operesheni Sangara` mkoani Kilimanjaro, wanaitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kuichunguza Meremeta na kuwachukulia hatua za kisheria Chenge na wale wote wanaotuhumiwa kujihusisha na kampuni hiyo iliyowezesha kuchotwa isivyo halali kwa fedha za walipakodi wa Tanzania.
Aidha, Dk. Slaa akasema kuwa yeye na wenzie wanafahamu kuwa tayari Rais Kikwete alishaunda Kamati ya Bomani kuchunguza sakata hilo, na kwamba kamati hiyo imeshawasilisha ripoti yake kuhusiana na suala hilo, hivyo kinachotakiwa ni kuchukuliwa kwa hatua zilizopendekezwa.
``Rais Kikwete aliunda Kamati ya Bomani kuchunguza. Kamati hiyo nayo ikatumia Shilingi Bilioni 1.5 kufuatilia suala hilo na mengine.
Mwishowe ikaja na sentensi moja tu, kwamba Meremeta ichunguzwe... lakini hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na Serikali.
Tunaitaka iamke na kuchukua hatua hiyo ya kuichunguza,`` akadai Dk. Slaa.
Kutokana na suala hilo, Dk. Slaa akadai kuwa CHADEMA itaendelea na Operesheni Sangara nchi nzima ili kuwahamasisha wananchi wachukie vitendo vya ufisadi wa aina ya Meremeta, ambavyo kwa bahati mbaya bado Serikali inachelewa kuvichukulia hatua stahili.
``Hatuwezi kuiacha Serikali inaachia mambo haya... tutapita kila kijiji cha nchi hii ili kuhamasisha wananchi wachukie vitendo vya aina hii,`` akadaiDk. Slaa.
Kufuatia madai hayo ya Dk. Slaa, mwandishi alimsaka Mheshimiwa Chenge kwa simu yake ya mkononi leo asubuhi, mishale ya saa 4:05 ili aelezee juu ya tuhuma za kuhusishwa na Meremeta. Lakini alikataa kata kata kuzungumzia suala hilo na badala yake akajibu kwa ufupi, akisema `asante`.
``Asante sana... na kila la heri,`` akasema Bw. Chenge baada ya kuelezwa kila kitu kuhusiana na madai ya Dk. Slaa, kisha akakata simu.
SOURCE: Alasiri