Mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika 2024 (FOCAC) ulimalizika hivi karibuni hapa mjini Beijing. Mkutano huo safari hii umekuja na habari njema ambayo imeleta faraja kubwa kwa nchi za Afrika mashariki, hasa baada ya kuonesha moyo wa dhati wa kuwaenzi waasisi wao yaani Mwenyekiti Mao Zedong na Mwalimu Julius Nyerere.
Hii inakuja baada ya hatua ya kihistoria kupigwa wakati Rais Xi Jinping wa China, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema waliposhuhudia utiaji saini mkataba wa makubaliano (MoU) wa kufufua Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Mkataba huu wa kihistoria uliotangazwa tarehe 4 Septemba, wakati wa Mkutano wa FOCAC, unasisitiza uhusiano wa kudumu kati ya China na Afrika na dhamira ya maendeleo ya pamoja. TAZARA, reli yenye urefu wa kilomita 1,860 inayounganisha Zambia isiyo na bandari hadi jiji la pwani la Tanzania la Dar es Salaam, imekuwa alama ya urafiki kati ya China na Afrika kwa miongo kadhaa.
Ikiwa imejengwa na wafanyakazi wa China wakisaidiwa na wenyeji wao Waafrika katika mwaka 1970 hadi 1975 kwa mkopo usio na riba kutoka China, reli hii ilitoa njia muhimu ya maisha kwa mauzo ya shaba ya Zambia kwa kusafirisha mizigo kutoka migodi ya shaba na kobalti ya Zambia hadi baharini kwenye pwani ya Tanzania. Pia ilileta changamoto kwa utawala wa kikoloni na kukuza uhuru wa kiuchumi. Shughuli za kibiashara za njia hiyo ya reli zilianza mwaka 1976, licha ya kupuuzwa na baadhi ya serikali za Magharibi wakati huo kama “reli ya mianzi”.
Mapema mwezi Februari mwaka huu, China ilipendekeza kutumia dola za Marekani bilioni 1 (kama Sh trilioni 2.72/-) kukarabati reli hiyo kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Hivyo kwa sasa, ufufuaji wa TAZARA ni muhimu zaidi kuliko hapo awali. Rais Xi Jinping, kupitia vyombo vya habari vya serikali, amenukukuliwa akisisitiza kwamba China iko tayari kuchukua fursa ya mkutano huu kufanya maendeleo mapya katika ufufuaji wa reli ya Tanzania na Zambia.
"China inapenda kuuchukulia mkutano huu kama fursa ya kufanya maendeleo mapya katika ufufuaji wa reli ya Tanzania na Zambia, kushirikiana kuboresha mtandao wa usafiri kati ya reli na bahari katika Afrika Mashariki, na kuijenga Tanzania kuwa eneo la mfano wa ushirikiano wa kina wenye bora wa juu wa “Ukanda Mmoja Njia Moja” kati ya China na Afrika," Rais Xi alisema.
Wakati uchumi wa Afrika unakua kwa kasi na biashara ya kimataifa inapanuka, miundombinu bora ya uchukuzi ni muhimu sana. China na Afrika zinaifanya reli hiyo kuwa ya kisasa na inayokwenda na wakati zaidi, ili kuimarisha mawasiliano ya kikanda, kurahisisha biashara, na kukuza maendeleo ya kiuchumi.
Uchakavu wa miundombinu na matatizo mengine ya kimtaji ni miongoni mwa masuala yaliyopunguza ufanisi wa TAZARA kiasi cha kuathiri ratiba za safari za treni za abiria na mizigo. Kwa maana hiyo mradi huo hautanufaisha Tanzania na Zambia pekee bali pia mataifa mengine ya Afrika yasiyo na bahari yanayotaka kupata masoko ya kimataifa. TAZARA iliyofufuliwa inaweza kutumika kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi, kutoa nafasi za ajira na kupunguza umaskini katika eneo la Afrika Mashariki.
Ufufuaji wa TAZARA unaendana na dhamira ya China ya maendeleo endelevu. Kwa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa na rafiki kwa mazingira, mradi huu unaweza kusaidia kupunguza utoaji wa kaboni, kuboresha ufanisi wa nishati, na kukuza ukuaji wa kijani. Makubaliano hayo yanaashiria hatua kubwa ya maendeleo katika kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika. Pia yanaonesha uungaji mkono usioyumba wa China kwa maendeleo ya Afrika na nia yake ya kuwekeza katika miradi ambayo ina umuhimu wa kihistoria na wa kimkakati.
TAZARA inapoingia katika enzi mpya, inatoa mwanga wa matumaini kwa mustakabali mzuri. Ufufuaji wa reli sio tu kwamba unahusu miundombinu, bali pia unahusu kuimarisha uhusiano, kukuza ustawi, na kujenga dunia iliyounganishwa zaidi na endelevu.