Helikopta ya Jeshi la Wananchi Tanzania yaua sita Arusha
*Ni ile iliyokuwa ikifanya doria wakati wa Sullivan
*Iliwaka moto na kutetea angani
Na Mussa Juma, Arusha
HELKOPTA ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), iliyokuwa inafanya doria wakati wa Mkutano wa Leon H Sullivan katika maeneo mbalimbali ya Arusha imeanguka jana mchana na kuua watu sita, wanne miongoni mwao wakiwa wanajeshi.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Matei Basilio alithitibisha jana kutokea kwa ajali hiyo katika eneo la Matevesi Wilayani Arumeru jirani kidogo na Uwanja Mdogo wa Ndege wa Arusha na kueleza kuwa watu wote sita waliokuwemo kwenye helikopta hiyo wamekufa.
''Ninachoweza kusema sasa ni kweli ajali hiyo imetokea na wote sita wamefariki baada ya helikopta hiyo kuwaka moto baada ya kuanguka,'' alisema Basilio.
Kamanda Basilio alisema kuwa helikopta hiyo ilianguka ikiwa safarini kwenda Dodoma jana baada ya kumaliza kazi maalum ya kuimarisha ulinzi wakati wa mkutano wa Leon H Sullivan.
Hata hivyo, Kamanda Basilio alisema majina ya wanajeshi ni kanali Makele, Meja Sinda, Luteni Kirunga na PT Mambe. Wengine ni mtoto mdogo Diana Mzirai na Irine Jitenga. Miili yote imehifadhiwa chumba cha maiti cha Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha.
Baadaye taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari Makao Makuu ya Jeshi ilisema helkopita hiyo ya JWTZ yenye namba 9507 iliyokuwa inarejea Dar es Salaam, ilianguka saa 6.40 mchana katika eneo la Oljoro nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Taarifa hiyo ilitaja waliofariki katika ajali hiyo ni marubani wawili, mafundi ndege wawili na abiria wawili. Ndege hiyo ilikuwa kati ya ndege mbili zilizokuwa zikitumika kwa shughuli za ulinzi, wakati wa mkutano wa Sullivan.
''Uchunguzi kuhusu ajali hiyo umeanza kufanyika kwa ushirikiano kati ya JWTZ na vyombo vingine,'' ilisema taarifa hiyo.
Umati wa wakazi wa Arusha jana walikuwa wakihaha kupata taarifa za tukio hilo na kupiga simu mara kwa mara kwa waandishi wa habari hasa kutokana na kutotolewa mapema taarifa kamili za tukio hilo.
Tukio hili limekuja wakati bado wakazi wa Arusha, hawajasahau heka heka za ndege hiyo iliyokuwa ikiranda juu ya anga wakati wote wa mkutano wa Leon H Sullivan.
Juni 3 mwaka jana, watu 13 walijeruhiwa katika ajali ya ndege ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yenye namba JW 9036 iliyoanguka eneo la Kizota mjini Dodoma baada ya kupata dhoruba angani.
Ndege hiyo aina ya SD33 Sherpa, yenye uwezo wa kubeba abiria 40 ilianguka saa 7:20 mchana katika eneo hilo baada ya injini zake mbili kushindwa kufanya kazi.