SoC02 Chuo sio bata

Stories of Change - 2022 Competition

Ceo_crypto

Member
Joined
Aug 27, 2022
Posts
6
Reaction score
3
Katika karne hii ya sayansi na teknolojia imekuwa karne ya mapinduzi mengi ya kimaendeleo na maisha ya binadamu vijana mojawapo ya kundi tegemewa sana kwenye karne hii, kwa wakati huu pia ndio tumeshuhudia mapinduzi makubwa ya kielimu hasa katika nchi zetu zinazoendelea ikiwemo Tanzania mapinduzi haya yamefanikisha kuongeza idadi kubwa ya vyuo kwenye nchi yetu, malengo ya taifa ni kumwezesha elimu kijana kupata elimu sahihi na bora.

Hata hivyo vijana wengi kabla kufikia elimu ya chuo hujenga mawazo ya chuo maisha ni mazuri, chuo elimu ni rahisi, chuo hakuna kufeli na wanafikia hatua ya kuiita elimu ya chuo kwa lugha ya mtaani na kusema “Chuo Bata” wakimaanisha elimu ya chuo ni rahisi na ndio elimu unayoweza kupata huku ukistarehe.

Dhahania hii ambayo vijana wengi ambao hawajafika chuo huijenga sio sahihi hata kidogo na kwa kutumia dhahania hii ya “chuo ni bata” vijana wengi hupata madhara yafuatayo chuoni ambazo mara nyingi huwa yanawaongoza kwenye kupoteza dira sahihi ya malengo yao kimasomo.

Matumizi mabaya ya fedha, kwasababu vijana hujenga mawazo kuwa ukiwa chuo ni wakati wa kufanya starehe matumizi yao ya fedha huwa tofauti na kile wanachokiingiza, wanafunzi wa vyuo vikuu serikali huwa inawapatia mikopo ya fedha za kujikimu kwa vijana wengi wa chuo fedha hizi hutumika vibaya na wengi wao kujikuta wanaishiwa fedha ndani ya muda mfupi.

Kufeli chuoni,
wanafunzi wengi kwenye vyuo vyetu huwa hawasomi, sio watafiti wa vile wanavyovisomea kwasababu ya dhahania inayokuwa vichwani mwao kuwa chuo ni bata mara nyingi wanafunzi hawasomi kwa undani vitu wanavyosomea hii wengi wao huwaongoza kwenye kufeli masomo yao chuoni na kupoteza dira ya malengo vile vile hupelekea kupata wahitimu wasio na ujuzi sahihi wa kile walichosomea.

Tabia ya umalaya na ushoga, dhahania ya chuo ni bata huwaongoza wanafunzi wengi kuwa na tabia ambazo zisizo za kimaadili ambazo kwa kiasi kikubwa huchangiwa na tamaa za wanafunzi kutaka fedha hivyo vijana wa kike uingia kwenye biashara ya kuuza miili yao na vijana wa Kiume kuingia kwenye tabia za ushoga ili tu wapate fedha ambazo zitawasaidia kula hilo bata la chuo.

Kupata msongo wa mawazo pale ambapo unafika chuoni na kuona wenzako wanastarehe na wewe ukiwa labda umetoka familia isiyo na uwezo mkubwa na huna hela za kutosha za kufanya starehe huku kichwani ukiongozwa na ile dhahania ya chuo ni bata, ikiwa wewe unajiona huwezi kula bata kama wenzako unaanza kupata mawazo ambayo wakati mwingine husababisha mwanafunzi kufeli na kuwa na tabia za hovyo.

Ndoa zisizo na malengo,
dhahania ya chuo ni bata pia imesababisha kuundwa kwa ndoa nyingi zisizo na malengo ambapo mwisho wa siku huleta mimba na kutelekezwa kwa mwanamke, wanafunzi wengi kike vyuoni wakiingia mwaka wa kwanza huwa kama almasi inavyotafutwa wanarubuniwa na wanafunzi miaka ya juu ya masomo vilevile walimu wao, wanakuwa na mahusiano ambayo kwa wengine hufikia hatua ya kuishi pamoja kama mume na mke, lakini endapo mwanamke atashika mimba mahusiano huwa machungu na kuvunjika huku mwanamke akitelekezwa na mimba ambazo husababisha kuvurugika kwa malengo.


Kuna mambo mengi hutokea kwa vijana chuoni kwa kujenga dhahania ya chuo ni bata mambo ambayo yanapingana na malengo ya serikali juu ya kuboresha elimu ya vyuo na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi, mambo gani ambayo mwanafunzi unatakiwa ufanye ili kuachana na huo usemi wa chuo ni bata,

Chuo si bata, cha kwanza inabidi kila kijana ambaye anaingia chuoni atambue kuwa chuo sio bata, yani elimu ya chuo inahitaji kujitoa kupambana kusoma kwa bidii kuacha starehe na kuwa mbunifu na mdadisi kila kijana akiingia chuoni na dhahania hii elimu ya chuo haiwezi kumvuruga kisaikolojia na atafanikiwa kwa asilimia zote kwenye elimu yake.

Kubali hali ya maisha uliyonayo, kama vijana wa vyuoni wakikubali hali zao za maisha kuna baadhi ya tabia zisingekuwepo kwenye vyuo vyetu hasa kwa wanafunzi wa kike, kuishi nje ya hali yako ya maisha huko ndiko husababisha wanafunzi kuwa na tabia ambazo sio za kimaadili ambazo mara nyingi husababisha matatizo kwao wenyewe.

Weka malengo sahihi kwenye masomo yako, kama mwanafunzi inapaswa uwe na malengo ambayo unatakiwa upambane kuyafikia na kukamilisha ukiwa na malengo nu rahisi kuweza kuendesha maisha yako ya chuoni vizuri malengo hubeba kile unachokihitaji na jinsi ya kukifikia malengo ni muhimu chuoni.

Usiwe limbukeni chuoni hakikisha ukiwa chuoni usiwe na tamaa na vitu vidogo vidogo, kuwa mtu ambaye huna tamaa hakikisha kuwa kitu unachokihitaji basi kiwe na umuhimu kwako sio kwasababu ya kuwaonyesha watu kuwa unacho hiko kitu hii itasaidia kukujenga kuwa imara na muwajibikaji mzuri.

Hakikisha mahusiano unayokuwa nayo chuoni yawe ni mahusiano yenye malengo, kwasababu kama mtu mzima ni muhimu kuanza kuwa na mahusiano lakini hakikisha hayo mahusiano yana umuhimu na yana malengo kwenu wote wawili ili mahusiano yasije yakaja kuharibu malengo yako ya chuoni kabisa.

Kuwa mwanafunzi mwema soma kwa bidii kuwa mdadisi na mbunifu,
jitahidi kusoma ili uondoe ujinga ila usisome kwa kutegemewa utaajiriwa sehemu fulani hii itakusaidia unapomaliza chuo kuwa mtu sahihi na si mzigo kwenye jamii yako na watu wako wanaokuzunguka.

Kwa hakika elimu ya chuo si elimu ya kuchezea au elimu ya kusoma juu juu kwakuwa elimu ya chuo ndio elimu ambayo imebeba malengo sahihi ya kwako vilevile ya taifa, katika elimu ya chuo ndio maana hata wanafunzi hawavai sare kwakuwa mpaka kufika elimu ya chuo inaaminika kuwa tayari wewe umejitambua na hakuna shida ya kukutambua tena kwa sare, kitu kikubwa kinachohitajika kutoka kwako ni maarifa yako na ubunifu wako kwaajili ya malengo ya taifa letu hili, napenda kurudia tena kusema elimu ya chuo ni muhimu kwako na taifa kila kijana aondoe ile dhahania ya chuo ni bata, na kila kijana aweke dhahania hii kuwa “Chuo Si Bata” .

Imeandikwa na David Jerome (ceo_crypto).
 
Upvote 2
Naomba mnipigie kura kwa kubonyeza kialama cha like chini ya makala hii, naomba pia unisaidie kushare hii makala kwa watu wengine ili nao wasome hii, maoni yako pia ni ya thamani kubwa kwangu nayaomba pia
 
karibuni kupata madini ya chuo
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…