Wanachama upatu wa Deci wataka kukutanishwa na tume ya serikali
Mmoja wa mamia ya wanachama wa upatu uitwao Deci waliokutanika Dar es Salaam ii kushinikiza kukutana na kamati ya serikali inayofuatilia kisa cha ushirika wa kupanda na kuvuna mbegu (fedha), ambao shughuli zake zimesitishwa na serikali.
Fidelis Butahe na Simon Simalenga
WASHIRIKI wa mchezo wa upatu unaoendeshwa na taasisi ya Development of Entrepreneurship for Community Initiative (Deci), jana walicharuka na kuzingira ofisi za makao makuu ya kampuni hiyo wakishinikiza wakutanishwe na tume iliyoundwa na serikali kuichunguza taasisi hiyo.
Serikali ilitangaza kusitisha shughuli zote za Deci, ikiwa ni pamoja na kuzuia akaunti zote na kuitaka iorodheshe upya majina ya washiriki wake kwa ajili ya kuwarejeshea fedha walizowekeza.
Lakini subira imeonekana haivuti heri kwa washiriki wa mchezo huo, maarufu kama "Kupanda na Kuvuna Mbegu" na tangu wiki iliyopita wamekuwa wakipanga kukutana kwenye ofisi za taasisi hiyo zilizo Mabibo jijini Dar es salaam kwa lengo la kushinikiza kuharakishwa kwa malipo yao.
Jana washiriki hao walijazana nje ya jengo la ofisi hiyo ambalo walidai kuwa limeshakabidhiwa kwa mmiliki wake kwa kile walichoeleza kuwa Deci imeshindwa kulipa fedha ya pango.
Mkusanyiko huo ulisababisha baadhi ya viongozi wa taasisi hiyo kuamua kuzungumza na washiriki hao ili kuwatuliza.
Akizungumza kwa upole, mmoja wa wakurugenzi wa Deci, Dominick Kigendi alisema kuwa zoezi la kuichunguza taasisi hiyo ni zito kwa sababu taasisi hiyo ina washiriki 700,000 hivyo aliwataka washiriki kuwa wavumilivu mpaka hapo uchunguzi utakapokamilika.
Wiki iliyopita walikuja washiriki na kuomba kujua hatima ya fedha zao, niliwaambia waandike majina na niliwaambia waje leo (jana) ili kupata majibu," alisema Kigendi.
"Sasa nawajibu kama ifuatavyo; uchunguzi bado unaendelea na si rahisi kutoa majibu kwa sasa.
Serikali imewaomba muwe watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati uchunguzi unaendelea. Deci ipo karibu sana na tume iliyoundwa kwa ajili ya kufanya uchunguzi hivyo mambo yakikamilika taarifa mtazipata. Nawatakieni kila la kheri katika uvumilivu wenu.
Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Timoth ole Loitingye aliwaambia washiriki hao kuwa fedha zao zipo, lakini wataitaarifu serikali ifanye haraka katika uchunguzi huo ili kuondoa usumbufu kwa kuwa inaonekana wazi washiriki wamechoka kusubiri.
Hata hivyo, kauli ya Kigendi ilionekana kuwakera washiriki hao na kujaa jazba. Washiriki wawili waliopewa nafasi ya kuuliza maswali, walisema hivi sasa uvumilivu umewashinda na kusisitiza kuwa lolote linaweza kutokea.
Tunachokitaka ni kukutanishwa na hiyo tume iliyoundwa kwa ajili ya kuichunguza Deci ili itueleze huo uchunguzi utakamilika lini na tutaanza kurejeshewa fedha zetu siku gani, alisema Abdalah Said.
Naye Lucas John alisema kuwa serikali ilitakiwa kutoifungia Deci badala yake ingeiamuru kwanza iwarejeshee fedha washiriki.
Lakini, Kigendi alijibu hoja hizo kwa kueleza kuwa maswali waliyouliza yataandikwa na kusomwa kwenye vyombo vya habari, hivyo wahusika watayaona na kuyafanyia kazi.
Maswali nimeyasikia lakini kuna vyombo vya habari hapa vitayaandika na yatasomwa na wahusika, alisema Kagendi na kuingia ndani huku akiwaacha washiriki hao wakiwa bado hawajajua hatima yao.
Akizungumza na Mwananchi, mwenyekiti wa kamati iliyoundwa na washiriki hao Deci kwa ajili ya kufuatilia kwa ukaribu urejeshwaji wa fedha zao, Mchungaji Isaack Kalenge alisema kuna siri nzito kati ya viongozi wa Deci na serikali.
Kalenge, ambaye aliwahi kukamatwa na polisi na baadaye kuachiwa kwa kile kilichoelezwa kuwa alikuwa akichochea vurugu, alisema kuwa viongozi wa Deci si wakweli akidai kuwa hawawaelezi ukweli washiriki.
Unajua sisi tunazungumza karibu kila wiki na viongozi wa Deci, lakini tunachozungumza nao sio wanachokisema wanapokuwa wakizungumza na washiriki. Hilo linatupa wasiwasi sana, tukiamua kusema tunachozungumza nao, hapa patakuwa hapatoshi, alisema Kalenge.
Nadhani kuna kitu kinaendelea kati ya Deci na serikali... kuna mchezo unachezwa hapa, kulikuwa hakuna sababu ya kuzuia fedha za wananchi, kwanza hata hiyo tume iliyoundwa kuchunguza Deci hatuna imani nayo. Kinachofanyika hapa ni kupoteza muda tu.
Alisema kuwa walikuwa wamepanga kuishitaki Deci, lakini uongozi wa taasisi hiyo uliwaomba kutolipeleka suala hilo mahakamani na badala yake wakae na kuzungumza ili kuweza kupata ufumbuzi wa suala lao.
Nafiriki hawa jamaa hivi sasa wanaleta usanii, tutakaa na kujadili suala hili kwa pamoja kama kamati. Tukiafikiana tutakwenda mahakamani. Wanaonekana wanataka kupoteza muda tu kwa kujifanya wanazungumza na sisi kumbe kuna mipango wanayoipanga, alisema Karenge.
Wiki iliyopita Waziri wa Fedha na Uchumi aliliambia Mwananchi kuwa kinachosubiriwa hivi sasa ni ripoti ya tume iliyoundwa kuichunguza taasisi hiyo ambayo inaongozwa na mkurugenzi wa makosa ya jinai, Robert Manumba.