JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 685
- 1,124
Anga la Tanzania limefunguliwa takribani wiki 2 zilizopita na nchi kuruhusu Watalii kuingia nchini.
Utaratibu wa watalii kuingia nchini utahusisha upimaji wa joto wakiwa Uwanja wa Ndege na kisha kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao za kitalii. Njia hii ya upimaji wa joto pekee ndiyo iliyosababisha CoronaVirus kusambaa duniani. Ikumbukwe pia kuwa watalii wengi hutokea nchi za Ulaya, Amerika na Asia ambazo hadi wakati huu bado zina viwango vya juu vya maambukizi ya COVID19.
Wakati suluhu salama zaidi ikiwa kuwazuia, kama nchi tumeshavuka huko na sasa suala la msingi ni kuangalia namna salama ya kuendelea na shughuli za utalii bila ya kuhatarisha afya na Maisha ya wanaotoa huduma.
Watalii waingiapo nchini wanahitaji huduma kama malazi, chakula, usafiri, uongozwaji, starehe, kuingia kwenye vivutio na maeneo ya kumbukumbu mbalimbali na kununua bidhaa mbalimbali za kitamaduni kwa ajili ya matumizi yao na kubeba kama zawadi. Ni muhimu watu wa sehemu hizi kujilinda sana ili kuepuka maambukizi.
Hatua za kuchukuliwa ni pamoja na
Uvaaji wa barakoa muda wote kwa wahudumu wa viwanja vya ndege, watoa huduma za usafiri binafsi na hata makampuni, wahudumu wa hoteli, migahawa na maeneo yote yanayotembelewa na watalii.
Wahudumu na wafanyabiashara waepuke ukaribu wa aina yoyote ikiwemo kupeana mikono na kukumbatiana na watalii. Umbali wa mita 2 uzingatiwe.
Ni muhimu kwa wasafirishaji kuhakikisha vyombo vitumikavyo vinazingatia “social distancing”
Sheria kali za unawaji wa mikono ziwekwe kwenye maduka ya bidhaa yanayohudumia watalii, maeneo ya vivutio, migahawa, sehemu za starehe n.k.
Waongozaji wa watalii wanapaswa kuwa na namba za mamlaka zinazohusika na suala zima la COVID19 endapo dharura itatokea ya mtalii kuonesha dalili
Waongozaji wa watalii wawasihi watalii kutojihusisha kingono na wazawa na wawaonye pia wazawa ambao hutumia suala la ngono kama fursa ya kupata manufaa kingono
Mamlaka ziwashauri watalii kutotumia usafiri wa umma ili kuepusha usambazaji endapo kwa bahati mbaya wakiwa wameathirika
Malipo ni vyema yakafanyika kwa njia ya mtandao au kadi za kibenki inapowezekana ili kuepusha usambaaji kupitia pesa
Ni vyema kwa wazawa kuepuka kwenda maeneo ya vivutio vya kitalii kwa wakati huu ambao dunia bado inapambana kutokomeza COVID19 ili kuepuka kujichanganya na watalii ambao wanatokea maeneo hatarishi.
Ikumbukwe kuwa baadhi ya hatua zinaweza kuonekana kama unyanyapaa lakini aina ya uambukizaji wa ugonjwa huu inalazimu hali kuwa hivyo.