ISOME KWA UREFU ZAIDI...
Mshambuliaji wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo amesema Ligi Kuu ya Saudi Arabia, Saudia Pro League, "ni bora" kuliko ile ya MLS na kwamba hana mpango wa kucheza Marekani au kurejea kwenye timu yoyote barani Ulaya.
Ronaldo alikuwa akizungumza na vyombo vya habari baada ya kucheza kipindi cha kwanza cha Al Nassr ikichapwa mabao 5-0 na Celta Vigo ya Ligi Kuu ya Hispania, LaLiga, nchini kwao Ureno juzi.
"Ligi ya Saudi ni bora kuliko MLS," nyota huyo wa Ureno alisema alipoulizwa kuhusu kuhamia Marekani kama mpinzani wake wa zamani wa nchini Hispania, Lionel Messi, ambaye alitambulishwa kama mchezaji mpya wa Inter Miami CF Jumapili.
Ronaldo, ambaye alitolewa wakati wa mapumziko wakati matokeo yakiwa 0-0, aliongeza: "Nilifungua njia kwa ligi ya Saudia, na sasa wachezaji wote wanakuja hapa."
Tayari msimu huu wa joto, wachezaji kadhaa wa hadhi ya juu wamemfuata Ronaldo, huku Karim Benzema, Marcelo Brozovic, N'Golo Kante na Roberto Firmino wakisaini mikataba ya kucheza Ligi Kuu ya Saudia.
Mchezaji wa zamani wa Inter Milan, Milan Brozovic alikuwa uwanjani na Ronaldo siku ya Jumatatu baada ya kujiunga na Al Nassr, Julai 3.
"Katika mwaka mmoja, wachezaji wengi wa juu zaidi watakuja Saudi. Katika mwaka mmoja ligi ya Saudi itapita ligi ya Uturuki na ligi ya Uholanzi," aliongeza Ronaldo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alielekea katika msimu wake wa kwanza kamili akiwa na Al Nassr tangu ajiunge na klabu hiyo Januari kufuatia kuondoka kwa ghafla baada ya kuichezea Manchester United kwa mara ya pili.
Ronaldo, mfungaji bora wa muda wote wa Real Madrid, pia alisema siku zake za kucheza Ulaya zimekwisha na anaamini kiwango cha uchezaji huko kimeshuka katika miaka ya hivi karibuni.
"Nina uhakika wa asilimia 100 sitarejea katika klabu yoyote ya Ulaya," aliongeza kusema Ronaldo.
"Nina umri wa miaka 38. Na soka la Ulaya limepoteza ubora mwingi. Lililo halali na ambalo bado linafanya vizuri ni Ligi Kuu ya England. Wako mbele zaidi ya ligi zingine zote."
Mchezo huo pia ulikuwa wa kwanza kwa kocha Rafa Benitez kuinoa Celta Vigo ambapo pia amewahi kuzinoa Valencia na Liverpool.
Al Nassr watacheza mchezo wao wa pili wa kirafiki nchini Ureno siku Alhamisi, wakimenyana na mabingwa wa nyumbani Benfica.