#COVID19 CUF: Hali ya maambukizi ya Covid-19 nchini Tanzania na hatua za kuchukua

#COVID19 CUF: Hali ya maambukizi ya Covid-19 nchini Tanzania na hatua za kuchukua

CUF Habari

JF-Expert Member
Joined
Dec 12, 2019
Posts
239
Reaction score
234
TAARIFA KWA UMMA
HALI YA MAAMBUKIZI YA COVID- 19 NCHINI TANZANIA NA HATUA ZA KUCHUKUA

Ndugu wanahabari!
Karibuni tena kwenye Ukumbi huu wa Shaaban Khamis Mloo ambapo CUF- Chama Cha Wananchi kinaongea na Umma wa Watanzania kwa mara nyingine kupitia kwenu.

Awali ya yote ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kukutana hapa muda huu. Pia tunawashukuru ninyi wanahabari kwa kuitikia kwenu wito wetu huu na kwa kazi nzuri ambayo daima mmekuwa mkiifanya kwa Maslahi mapana ya Tanzania yetu, kwa kuzingatia Maadili na Miiko ya Tasnia yenu Muhimu.

Ndugu wanahabari!

Mara kadhaa tumekuwa tukitoa Matamko mbalimbali kuelezea hali halisi ya Maambukizi ya COVID- 19 Duniani na kupendekeza hatua za Kuchukua kama nchi ili kukabiliana na janga hili tishio.

Baada ya Kikao chake cha kawaida tarehe 5-6 Machi 2020, Baraza Kuu lilitoa Tamko ambalo nililisoma mbele yenu Waandishi wa Habari kwa minajiri ya kuufikia Umma wa Watanzania. Baraza Kuu lilieleza:-

“Baraza Kuu limepokea taarifa ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona COVID-19 ulitolewa taarifa kwa mara ya kwanza Wuhan, China tarehe 31 Desemba 2019. Mpaka tarehe 5 Machi, siku ambayo Baraza Kuu lilianza kikao chake, Shirika la Afya Duniani WHO lilieleza kuwa wagonjwa waliokuwa wametolewa taarifa ni 95,265 na waliofariki ni 3281. Wengi wa wagonjwa na vifo vimetokea China. Nje ya China kuna taarifa za wagonjwa 2055 katika nchi 33. Inaaminika kuwa idadi ya wagonjwa ni kubwa zaidi kuliko idadi waliotolewa taarifa. Mpaka hivi sasa hakuna taarifa ya maambukizi ya ungojwa huu nchini Tanzania na nchi za jirani. Hata hivyo ni vyema kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu janga hili lisiingie nchini lakini tujiandae kikamilifu kana kwamba wakati wowote nasi tunaweza kukumbwa na janga hili.

Maandalizi hayo ni pamoja na uwezo wa kupima maradhi hayo hasa katika viwanja vya ndege vya kimataifa, hospitali na vituo vya afya, taratibu za kuweka karantini ikiwa ugonjwa utaibuka, wadi za kulaza na kuwatibu wagonjwa wa maradhi haya na kutoa mafunzo ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu.

Serikali kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa hasa WHO iandae mkakati madhubuti wa kukabiliana na mlipuko wa COVID-19. Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Maendeleo ya Afrika limetangaza kuwepo kwa mifuko ya dharura ya kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona. Tunaishauri serikali kuwasilisha maombi ya misaada hii kusaidia kujenga uwezo wa kukabiliana na COVID-19 kabla maradhi haya kuibuka nchini. Kama taifa tutumie tishio la COVID-19 kujenga mfumo imara wa huduma za afya.”

Taarifa hii tumeieleza kwa Waandishi wa habari tarehe 7 Machi 2020. Mwaka mmoja baadaye, hadi kufikia tarehe 6 Machi 2021, takwimu za WHO zinaonyesha maambukizi ya COVID-19 yaliyothibitishwa ni watu 115, 653,459 ikiwa ni pamoja na watu 2,571,823 waliofariki.

Ndugu Wanahabari,
Tarehe 13 Machi 2020, Rais Magufuli alizungumza na Umma wa Tanzania alipokuwa akizindua karakana kuu ya Jeshi la Wananchi Tanzania jijini Dar Es Salaam. Akizungumzia suala la Corona Rais alinukuliwa akisema, “'Ugonjwa upo na umekumba nchi nyingi kwa takwimu zilizopo ni kwamba zaidi ya watu 100,000 wameambukizwa na watu 4,500 wamepoteza maisha. ...Tunatambua kuwa Tanzania mpaka sasa hatuna mgonjwa wa corona lakini hatuwezi kujiweka pembeni bila kuchukua hatua, na hatua zimeanza kuchukuliwa Waziri wa wizara ya afya ameshatoa tahadhari tunazopaswa kuchukua. ...Ugonjwa huu unaua na unaua kwa haraka sana, niwaombe tusipuuze, tusipuuze hata kidogo ni lazima kuchukua hatua za kujikinga na tatizo hili.” Huu ulikuwa mwongozo sahihi

Ndugu Wanahabari,
Tarehe 19 Machi nilizungumza na Vyombo vya Habari kuhusu janga la Corona. Nilieleza “Serikali imetangaza kuwa mpaka siku ya Jumatano kuna wagonjwa watatu waliothibitika kuwa na virusi vya korona. Serikali imetoa amri ya kufunga shule na vyuo kuzuia maambukizi shuleni na vyuoni.

Ndugu Wanahabari, CUF-Chama Cha Wananchi kinatoa Pongezi kwa Juhudi ambazo Serikali imechukua katika kupambana na Maambukizi ikiwa ni pamoja na kutangaza Mara kwa mara njia za kudhibiti Maambukizi na hatua za dharura za kuchukua pindi dalili zinapodhihiri, na Maamuzi ya Kufunga Shule na Vyuo ili kupunguza Mazingira ya mikusanyiko.
Pamoja na Pongezi hizi, CUF-Chama Cha Wananchi kinaamini Serikali ilipaswa kufanya zaidi ya ilivyofanya katika kukabiliana na Maambukizi haya. Kwa ukubwa wa nchi yetu na kwa kuzingatia madhara makubwa na ya haraka, ni muhimu kuwa na maabara nyingi zenye uwezo wa kupima maradhi haya. Kama tunavyokumbuka, mtu wa Kwanza kujulikana kwamba ana vimelea vya COVID-19 aliyepatikana Uwanja wa Ndege wa KIA ilishindikana kubaini kwamba alikuwa na tatizo hilo mpaka sampuli zilipopelekwa Muhimbili kwa Vipimo zaidi.”

Pia tulieleza “Tumepokea kwa faraja taarifa ya msaada uliotolewa na Jack Ma, bilionea wa China na muasisi wa kampuni ya Alibaba ya kusaidia kila nchi katika bara la Afrika maski za kinga 100,000, kiti za vipimo vya virusi vya korona 20,000 na suti za kinga 1000. Tunaishauri serikali ichangamkie msaada huu ufike nchini haraka iwezekanavyo. Msaada huu usaidie kuongeza vituo vya kupima maradhi haya. Uwezo wa kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu kunategemea kujua uwepo wa ugonjwa. Bila kupima huwezi ukajua kama ugonjwa umeanza kusambaa nchini.”

Hata hivyo Tovuti ya Africa CDC inaonyesha kuwa mpaka tarehe 21 Mei, 2020; Tanzania imepima vipimo vya Corona 652 na kubaini wagonjwa 509 wakati Kenya imepima vipimo 52507 na kubaini maambukizi 1109. Uganda imepima vipimo 77072 na kubaini maambukizi 274 na Rwanda wamepima mara 53317 na kubaini maambukizi 314. Kiti 20,000 za kupima corona zilizotolewa na Jack Ma ziko wapi?

Ndugu Waandishi wa Habari,
Tarehe 14 Juni 2020, nilizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu hotuba ya bajeti ya serikali ya mwaka 2020/21. Kuhusu hatua za serikali kupambana na Corona nilieleza “Hatua za kibajeti zilizochukuliwa na serikali ni kidogo sana. “Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 19.5 hadi mwezi Mei 2020 kwa ajili ya kukabiliana na COVID-19. Kati ya hizo, shilingi milioni 500 zilizokuwa zitumike katika sherehe za Muungano zilielekezwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na shilingi bilioni 14.3 ni fedha zilizotokana na Global Fund ambazo awali zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya mradi wa Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI.”

Pia nilifafanua “Utafiti wa CDC Africa unaonesha idadi ya Watanzania ambao wanakadiriwa kuwa watafariki katika mwaka mmoja ikiwa hakuna tahadhari yeyote ni 6,180. Watu zaidi ya 450,000 wanafariki kila mwaka. Mkakati sahihi wa kukabiliana na COVID-19 ilikuwa kuchukua tahadhari hasa kwa wale ambao wana maradhi, na Corona inaweza kutishia maisha yao na siyo kuwafungia wananchi wa Dar es Salaam wasitoke majumbani.

Uamuzi wa kukataa lockdown ni sahihi lakini hauna maana tuache kupima ugonjwa huo na kuendelea kushirikiana na WHO.
Tovuti la Shirika la Afya la Dunia linaonyesha idadi ya maambukizi ya Corona hayajabadilika tangu tarehe 8 Mei mpaka hivi sasa. Maambukizi ya Corona ni 509 na watu waliokufa kwa sababu ya Corona ni 21.”

Kwenye Taarifa yetu kwa Umma tuliyoitoa Januari 23 mwaka huu kupitia Kurugenzi yetu ya habari, tulielezea wasiwasi juu ya kuongezeka kwa Maambukizi ya CORONA nchini na uwezekano wa kuingia nchini kwa kimelea hatari zaidi cha CORONA cha Mutated Corona Virus cha Afrika Kusini. Tuliongelea pia ubaya na hatari ya kutopima na kuweka bayana takwimu halisi za Maambukizi ya CORONA. Aidha tulisisitiza pia umuhimu wa kufuata Maelekezo ya Shirika la Afya Duniani ( WHO) na pia kuzifanyia Utafiti Chanjo mbalimbali dhidi ya CORONA ambazo tungeweza kuzipata kupitia Africa CDC na Taasisi ya Kimataifa ya COVAX inayosimamia ugawaji wa Chanjo kwa nchi maskini.

Ndugu wanahabari!
Tangu tumetoa tahadhari mfululizo na kutoa wito kwa Serikali juu ya hatua mbalimbali za kuchukua katika kupambana na Maambukizi ya COVID-19, yafuatayo ni miongoni mwa yaliyojitokeza:-

1. Kuwekewa vikwazo kwa wasafiri wanaotoka Tanzania au wanaopitia Tanzania kukanyaga katika ardhi za nchi mbalimbali, hususan Uingereza;

2. Kutolewa taarifa na Serikali ya Oman kuwa asilimia 18 ya wasafiri wanaotoka Tanzania na kuingia Oman wana virusi vya Covid vikiwemo vya Afrika ya Kusini. Hivi sasa Tanzania haimo katika orodha ya nchi ambazo wasafiri wake wanaruhusiwa kuingia Oman.

3. Nchini Denmark wasafiri wawili kutoka Tanzania wamebainika wana virusi vya Corona vya Afrika ya Kusini

4. Nchini India alau msafiri mmoja kutoka Tanzania amebainika ana virusi vya Corona vya Afrika ya Kusini

5. Tarehe 27 Januari Rais Magufuli wakati anafungua shamba la miti Chato alisema “kuna Watanzania wameenda nje ya nchi wakachanjwa huko wametuletea Corona ya ajabu ajabu. Chanjo hazifai.” “Mungu wetu yuko hai anaendelea kutulinda.”

6. Tarehe 5 Februari 2021, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Mabula Mchembe akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza alieleza msimamo wa Serikali wa kutoomba wala kupokea chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 unao sababishwa na virusi vya corona. Sababu ya msimamo huo wa Serikali ni kuwa “Hadi sasa hakuna utafiti wa kitabibu uliofanyika kubaini ni chanjo ipi inafaa kutumika kwa Watanzania.” Pia haijulikani chanjo inadumu kwa muda gani.

7. Tanzania imeandikwa sana kwenye vyombo vya habari vya kimataifa kwa msimamo wake kuhusu COVID-19. Mfano Tovuti ya BBC tarehe 6 Februari 2021 “Coronavirus in Tanzania: The country that's rejecting the vaccine.” Washington Post la tarehe 17 Februari 2021 “Tanzania’s leader says his country is ‘covid-free.’ The facts are proving him wrong.” Shirika la Habari la Reuters tarehe 17 Februari 2021 “Covid-skeptical Tanzania is experiencing a spike in pneumonia”

8. Tarehe 10 Februari 2021 Ubalozi wa Marekani umetoa Tahadhari ya Kiafya inayoeleza “Ubalozi wa Marekani unafahamu kuwa pamekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya visa vya COVID-19 toka mwezi Januari 2021. Aidha, hatua za kuondosha na kuzuia maambukizi ya COVID-19 bado zimeendelea kuwa za kiwango cha chini. ... Aidha, Taasisi ya Kudhibiti na Kuzuia Maradhi ya Marekani (CDC) inasema kuwa wasafiri waepuke kusafiri kwenda Tanzania.”

9. Tarehe 20 Februari, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Dr Tedros Adhanom Ghebreyesus alitoa taarifa inayoeleza kuwa mwishoni mwa mwezi Januari, “yeye na Dr Matshidiso Moeti Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika waliishauri serikali ya Tanzania waongeza juhudi za kinga dhidi ya COVID-19 na wafanye maandalizi ya chanjo dhidi ya COVID-19. Pia waliisihi serikali ya Tanzania kutoa takwimu ya maambukizi ya COVID-19 baada ya kupata taarifa ya Watanzania wengi wanaosafiri nje ya nchi wanabainaka wana maambukizi ya Corona. Mpaka sasa Shirika la Afya Duniani halijapata taarifa zozote toka Tanzania kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali kupambana na COVID-19. Hali ya Tanzania ni ya mashaka makubwa. Natoa wito kwa Tanzania kuanza kutoa Taarifa za COVID-19. Pia ninatoa wito kwa Tanzania kuanza kutekeleza hatua za kuzuia maambukizi ya Corona na kujiandaa kwa Chanjo. Ni muhimu Tanzania kuchukua hatua kuzuia maambukizi ya corona kuwalinda Watanzania na wananchi wa nchi jirani na dunia kwa ujumla.”

10. Kuzuiwa kwa Timu yetu inayowakilisha Taifa katika Mashindano ya Kombe la Shirikisho , Namungo FC ya Lindi kucheza mechi yake huko Angola wiki mbili zilizopita. Imekuwa ni bahati tu kwamba Maamuzi ya Shirikisho la Soka Afrika ( CAF) yalielekeza mechi hiyo ihamishiwe Tanzania na hivyo kuiwezesha Timu yetu kufuzu kuingia hatua ya Makundi baada ya kushinda mechi zake;

11. Taifa limepata msiba mkubwa wa kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad, Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Maalim Seif alikuwa jasiri. Alieleza wazi kuwa anaumwa COVID-19. Ujumbe wake wa simu ulieleza “Naomba kuwajulisha kuwa Jumatatu niliomba nipimwe Covid 19 mimi na mama yenu baada ya kupata nimonia kali. Jumanne tukapimwa.Rapid test ilionesha viashiria kwa kuwepo kwa covid 19. Nikashauriwa mimi na Bi Aweina tuji- self isolate tukianza kupata madawa. Test halisi leo zimethibitisha kuwa tunayo. Baadhi ya walinzi wangu 3, Hassan na Alii na Mayasa wameonekana na viashiria kwa rapid rest. Baada ya saa 72 ndio watapata confirmation.

Leo nimepata matatizo ya kupumua. Hivyo mnamo saa 11.45 jioni nimelazwa Mnazi Mmoja kwa close supervision. Madaktari wamejitahidi sana. Sasa sijambo na matibabu yanaendelea. Bibi Aweinah hajambo. Yuko self isolation nyumbani. Musiwe na wasi wasi. Zidisheni dua tu. Mungu Ataninyanyua, Amin”

12. Vifo mfululizo vimeripotiwa katika kipindi hiki. Kwa kuwa kiwango cha upimaji si kikubwa, si rahisi kusema kwa uhakika kwamba vifo hivi vimetokana na CORONA. Wapo kadhaa ambao vifo vyao vimeripotiwa kutokana na matatizo katika mfumo wa Upumuaji na pia wapo ambao vifo vyao ama vimetanguliwa au vimefuatiwa na vifo vya watu wao wa karibu sana kwa muda mfupi na kwa maradhi yanayofanana, yanayohusu mfumo wa upumuaji.

13. Tarehe 3 Machi 2021, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima ameeleza kuwa zaidi ya mapadri 25, watawa zaidi ya 60 na wazee wawili wa Baraza la Walei wamefariki dunia ndani ya miezi miwili kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo changamoto ya upumuaji.

14. Kuna taharuki miongoni mwa wahudumu wa afya kuwa hawana kinga ya kutosha dhidi ya maambukizi ya COVID-19

15. Upimaji wa COVID-19 ni ghali siyo chini ya dola 100 sawa na shilingi 230,000/-

16. Serikali ya Saud Arabia imetangaza kuwa ni lazima mahujaji wa mwaka huu wawe na Chanjo dhidi ya Corona. Bila chanjo huwezi kupata viza ya kwenda Hijja.

17. Tanzania haimo katika mgao wa kwanza wa Chanjo uliofanywa na COVAX na utakaotekelezwa kati ya Februari – Mei 2021 unaotarajiwa kugawa dozi milioni 237. Kenya imetengewa dozi 3,564,000. Malawi dozi 1,260,000. Mozambique dozi 2,064,000. Rwanda dozi 846,960. Uganda dozi 3,024,000. Zambia dozi 1,212,000.

Ndugu wanahabari!
Baada ya kuyasema yote yaliyotangulia, tunaomba kumalizia Ujumbe wetu kwa Umma wa watanzania kama ifuatavyo:-

a) Tunarudia kutoa wito kwa Serikali zote mbili kuhimiza na kusimamia Kupima COVID - 19 na kuweka bayana takwimu za Maambukizi;

b) Afya siyo jambo la Muungano. Zanzibar ina haki na wajibu wakujiwekea utaratibu wake wa kupima Covid-19 na kutoa taarifa. Kutathimini chanjo zilizopo na kuiomba Jumuiya ya Kimataifa hususan COVAX ipewe mgao stahiki wa chanjo.

c) Tunarudia kutoa wito kwa Serikali kuzingatia Maelekezo yote ya Shirika la Afya Duniani ( WHO) katika kupambana na Maambukizi dhidi ya CORONA. Ni muhimu kushirikiana na Jumuiya ya kimataifa. Tusipofanya hivyo nchi yetu inaweza kutengwa hasa katika usafiri wa kimataifa na kuathiri utalii, biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi na jamii kwa ujumla.

d) Madaktari na Wanasayansi wote wawe huru kufanya tafiti na kutoa ushauri wao wa kitaalam bila kuogopa kuwa ikiwa taarifa zao zitakinzana na fikra za Rais wataingia matatani

e) Ili kujua hali halisi ya maambukizi ya virusi vya Corona, wataalam wa afya wanaweza kufanya vipimo vya sampuli ya bila utaratibu maalum (random sample) ya watu 5000 mpaka 10000 kujua hali halisi ya corona jijini Dar es Salaam. Kwa mfano unaweza kuchukua sampuli kwenye masoko ya Buguruni, Tandale, Temeke kujua hali ya maambukizi kwa wananchi wa kawaida. Kujua hali ya maambukizi kwa wananchi wa kipato cha juu unaweza ukachukua sampuli Mlimani City, Shoppers Plaza na maeneo mengine. Utaratibu kama huo unaweza kufanywa katika miji mingine.

f) Tunarudia kutoa wito kwa Serikali kufanya utaratibu wa kuwatumia Wataalamu wa Afya kuzifanyia uchunguzi Chanjo za CORONA na hatimae majibu ya uchunguzi wa wataalam ndiyo yaongoze kuamua juu ya kutumia au kutotumia chanjo hizo. Tunatambua WHO ina utaratibu madhubuti wa kuidhinisha Chanjo za kutumia. Nchi za jirani; Kenya na Rwanda tayari wameanza taratibu za kuwachanja wananchi wao. Kongo DRC wamepokea chanjo. Afrika ya Kusini, Ghana, Cote D’Ivoire na Senegal pia wameanza kuwachanja wananchi wao.

g) Tanzania haijatumia fursa ya kupata mkopo usiokuwa na riba kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa kushughulikia tiba na athari za Corona. Serikali inaweza kukopa hadi dola milioni 569 bila riba yeyote. Ulipaji wa deni hili unaweza kuanza miaka tano na nusu baada ya kukopa na deni lote liwe limelipwa katika miaka 10. Fursa ya mkopo huu ipo mpaka tarehe 30 Juni 2021. Vilevile Serikali inaweza kupata mkopo wenye masharti nafuu toka Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Bado tunaendelea kuunga mkono Msimamo wa Serikali wa kutoifungia nchi ( Lockdown) lakini tunaamini Serikali inapaswa kuweka utaratibu mwepesi wa kupima Corona kushirikiana na WHO katika mapambano dhidi ya Corona.

Mwisho kesho tarehe 8 Machi ni siku ya wanawake ambao pia ni wahanga wakubwa wa Corona na mfumo duni wa huduma za afya. Tuwaenzi kina mama kwa kuongozwa na sayansi katika mapambano yetu dhidi ya Corona.

HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!

Prof. IBRAHIM HARUNA LIPUMBA
Mwenyekiti- Taifa
CUF - Chama Cha Wananchi
Machi 7, 2021
 
Naona watu hawaangalii nini kimesemwa bali nani kasema,ndio maana huwa naona hizi kelele za Korona ni siasa tu wazee wa matukio.
 
Magufuli ni mzalendo kwelikweli angekuwa fisadi hii covid19 ilikua ni fursa rahisi sana kuiba. Ndio maana watanzania wengi tena wengine ni wa vyama pinzani wao wanaangalia mkopo wa riba nafuu bila kujali italipwaje.

Hawajui kama lengo namba moja la Korona duniani ni kuwanufaisha wale waliofadhili kutengenezwa hicho kirusi. TUZIDI KUMUOMBEA RAIS WETU YUPO KWENYE VITA NGUMU SANA LAKINI TUNAMUANI NI JASIRI NA ATASHINDA HAKIKA.

#Mungu akushindie Rais wangu nakupenda sana
 
Ficha ujinga wako kidogo prof. Wenzenu walishatoa msimamo tangu mwaka jana kipindi cha bunge na wakatukanwa na kuambiwa warudishe pesa ya allowance we ulikuwa wapi.
 
Mmechelewa sana,wajanja tulishtuka kitambo
Nalog off
 
Magufuli ni mzalendo kwelikweli angekuwa fisadi hii covid19 ilikua ni fursa rahisi sana kuiba. Ndio maana watanzania wengi tena wengine ni wa vyama pinzani wao wanaangalia mkopo wa riba nafuu bila kujali italipwaje.

Hakuna mzalendo ambaye ni jizi la kura, wanaosema ni mzalendo ni wale aliowapa ulaji, kiasi kwamba imefikia mahali sasa hivi inakuwa vigumu kutofautisha uzalendo na ujinga.

Hao CUF walikubali kutumiwa na shetani kwenye uchaguzi, lakini walichofanyiwa ndio wamejua shetani hana rafiki. Hizi porojo zao saa hii hakuna mtu ana muda wa kuwasikiliza, labda wawapelekee ccm maana ndio mabwana zao.
 
Upinzani upi? maana kila chama ni pandikizi kasoro Chadema tu,ndio tuseme kwamba Tz tukizungumzia upinzani tuna maanisha Chadema tu?
CHADEMA na ACT Wazalendo ndio vyama vya Upinzani dhidi ya CCM

Trust me wakati niko CCM tulikuwa tunapanga mikakati kila Mbinu ya kupigwa CHADEMA na kuwafilisi Viongozi wake.
 
Chadema na ACTwazalendo ndio vyama vya Upinzani dhidi ya CCM

Trust me wakati niko CCM tulikuwa tunapanga mikakati kila Mbinu ya kupigwa Chadema na kuwafilisi Viongozi wake.
Kuna siku nilikuwa natumia kifaa cha mawasiliano cha mwanausalama mmoja hivi. Nililazimika kutumia kwasababu nilikuwa namsaidia kazi zake. Dah niliyoyaona huko. Ni wapumbavu tu watakaosema CCM inashinda uchaguzi ati kwakuwa inapendwa
 
Lipumba anàtaka kutumia Korona kama mtaji wa kisiasa!

Hakuna mkopo usiokuwa na riba!! wala hakuna mkopo wa riba nafuu!

Hata hiyo chanjo kupita mpango wa covax siyo ya bure kabisa kama inavyozungumzwa! Watakuambia hiyo imeshalipiwa tayari Ila wanakupa fursa ya kujikaanga mwenyewe kuambiwa uchangie sehemu ya gharama kwenye mfuko wa covax!

Kiasi utakachotoa kitaamriwa kwa kukubaliana kwanza na wafadhili waliowezesha gharama za upatikanaji wa chanjo hiyo!! Lazima utoe!
Sisi Tumekataa maana chanjo imepatikana kwa "mwendo kasi" na madhara yake ya muda mrefu hakuna ayajuaye!
 
Meseji ya Maalim ilikuwa inatia matumaini lakini ghafla mambo yakabadilika , inakuwaje alihamishishwa hospital nyingi nyingi?
 
Acheni stori ndeeeeeefu amwambie Mtemi Mwanamalundi aache kuiingilia Tume ya Uchaguzi aiache iwe huru halafu muitishe Uchaguzi mpya muone hichi Chama chenu cha Mtutu wa Bunduki kama kitabakia madarakani
 
Kuna siku nilikuwa natumia kifaa cha mawasiliano cha mwanausalama mmoja hivi. Nililazimika kutumia kwasababu nilikuwa namsaidia kazizake. Dah niliyoyaona huko. Ni wapumbavu tu watakaosema ccm inashinda uchaguzi ati kwakuwa inapendwa
Suala la CCM kuiba kura au kutumia mbinu ambazo si halali ili kushinda hilo linafahamika ila bado kuna wapenzi wengi tu wa CCM.
 
Acheni stori ndeeeeeefu amwambie Mtemi Mwanamalundi aache kuiingilia Tume ya Uchaguzi aiache iwe huru halafu muitishe Uchaguzi mpya muone hichi Chama chenu cha Mtutu wa Bunduki kama kitabakia madarakani
Mimi sina chama kwanza japo nakielewa ADC, tatizo ninyi mnawaza kuitoa CCM tu madarakani na kuishia hapo ila je nani atachukua madaraka baada ya kuitoa CCM madarakani? hapo ndio unakuta vyama vinavyoshoshutumiana kuwa vibaraka wa CCM yani vurugu tupu.
 
Mimi sina chama kwanza japo nakielewa ADC,tatizo ninyi mnawaza kuitoa ccm tu madarakani na kuishia hapo ila je nani atachukua madaraka baada ya kuitoa ccm madarakani? hapo ndio unakuta vyama vinavyoshoshutumiana kuwa vibaraka wa ccm yani vurugu tupu.
CCM ikitoka tunaunda coalition ya vyama makini navyo vinajulikana na vingine vitaundwa ili kuripea demeji ilisababishwa na CCM ya awamu ya tano
 
Back
Top Bottom