KAKA zetu Mna Mambo!
Msema kweli hakika, huyo mpenzi wa Mungu,
Kalamu nimeishika, nilisemalo ni langu
Beti ninaziandika, mzisome kakazangu,
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo.
kaka zetu mwatutega, twategwa tukategeka,
Mikogo mnayomwaga, twajikwaa twaanguka,
Na nyuma mkigeuka, toba! Tunanusurika,
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo.
mkifungua mapochi, wagumu wanayeyuka,
dada kila akiona pochi, kiwewe kinamshika,
tena mbele yake pochi, miguu yatetemeka,
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo.
Hasa mnaponong'ona, mwatupandisha presha,
Tunabakia kuguna, na milio ya kutisha,
Na tukiwa tumenuna, kwq pochi mwatuchekesha,
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo!
Nguo zinavyowapendeza, mwatusukuma dhambini,
na mjuavyo kuchombeza, mwatuingiza majaribuni,
kaka zetu mwatuweza, mwajua mwafanya nini,
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo!
Mara mnatukonyeza, mwapiga jicho kwa vile,
Twabaki twajiuliza, ana nini kaka yule,
Tukija twajibamiza, twalishwa chenga za Pele,
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo!
Mwajua kutuchombeza, kama samaki na chambo,
Magoma tukiyacheza, kama ndege na ulimbo,
Wenzenu mwatumaliza, mkisimamisha ‘mtambo',
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo!
Mwajua kututuliza, mwauma na kupuliza,
Tena mnatuliwaza, twalala twapitiliza,
Kweli mnatushangaza, twabaki twajiuliza
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo!
Mengi tunawakosea, majumbani twawakimbiza,
Maneno twawatolea, na mengine ya kubeza,
Mengi tunawatendea, twatenda bila kuwaza,
kaka zetu mna mambo mambo yenye vijimambo!!
Mwisho mnakimbilia, kwa mwingine kutulia,
Mapenzi kutafutia, mahawara mwajipatia,
Mioyo ikitulia, kimoja mnazamia,
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo!
Wengine mwavumilia, na miaka inapita,
Watoto kutukuzia, kumbe mioyo yajuta,
Na siku ikifikia, na ninyi mbele mwapeta,
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo!
Ukweli nawaambia, bila nyinyi tumekwisha!
Tunakaa twajutia, na mawazo tunakesha,
kwa mawazo twaumia, machungu yanatuzonga,
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo!
kaka zetu twawapenda, Bila ninyi tunakonda,
Kila siku zikienda, twajuta tunayotenda,
Msiache kutupenda, twapenda mnavyopenda,
kaka zetu mna mambo, mambo yenye vijimambo!