Daktari: Wanaojaribu kujiua wasishtakiwe

Daktari: Wanaojaribu kujiua wasishtakiwe

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Joined
Feb 7, 2022
Posts
2,780
Reaction score
6,607
Madaktari wanaotibu magonjwa ya afya ya akili, wameiomba serikali kupitia upya sheria inayowafunga watu wanaofanya jaribio la kujiua ili wapatiwe tiba na kuondoa tatizo hilo kwa jamii.

Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Huduma ya Ubora wa Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili Mirembe, Dk. Minael Urio, alitoa rai hiyo juzi baada ya hitimisho la matembezi ya hisani ya kupinga kujiua.

Alisema, waathirika hao wanapaswa kupelekwa hospitalini kupata matibabu ili kubaini tatizo linalowasumbua mpaka kufikia hatua ya kutaka kujiua.

"Wakipata nafasi ya kutibiwa, inaweza kusaidia kumtoa katika hatua aliyofikia badala ya kubaki vivyo hivyo akiwa mahabusu. Tunaomba sheria iangaliwe upya ili kuwanusuru waathirika wa matukio haya nchini," alishauri.

Dk. Urio, alisema wataalamu hao wanaamini wagonjwa wa afya ya akili wakipatiwa matibabu, watapona na kuendelea na majukumu yao vizuri.

“Ulimwenguni takriban watu 800,000 hujiua kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali na kila baada ya sekunde 40 watu hufanya jaribio la kujiua,” alisema.

Pamoja na hayo, aliishukuru serikali kwa kuwapatia bajeti kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo ambayo ni kitovu cha masuala ya magonjwa ya akili nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk. Paul Lawala, alisema matembezi hayo ni moja ya kigezo cha kuamsha hamasa kwa jamii ili kuwafichua wagonjwa wa akili na kuwapeleka kupata matibabu.

"Matembezi ya hisani yamesaidia kwa kiasi kikubwa sana hospitalini hapa, tumefanikiwa kupata mabalozi ambao husaidia kutoa elimu ya kuwapeleka wagonjwa wa afya ya akili kupata matibabu," alisema Dk. Lawala.

Mbunge wa Iringa, Jesca Msambatavangu, aliipongeza hospitali hiyo kwa jitihada inazofanya kuhakikisha wagonjwa wa afya ya akili wanapatiwa matibabu.

Alisema, wabunge watalisemea bungeni suala la uboreshaji miundombinu ya hospitali hiyo ili kuhakikisha linatekelezwa ipasavyo kwa kuwa sehemu hiyo ni muhimu kwa jamii.

Pia, alisema watakwenda kutoa elimu kwa jamii katika maeneo mbalimbali katika majimbo wanayotoka ili jamii iwapeleke hospitali wagonjwa hao.

Chanzo: Nipashe
 
Back
Top Bottom