BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 525
- 1,257
Naomba nitumie jukwaa hili kuwasilisha dukuduku yangu nikiwa naamini ujumbe utawafikia wahusika kama ambavyo tumekuwa tukiona kwenye baadhi ya kero ambazo zimekuwa ziibuliwa hapa jukwaani.
Ni kwa mara kadhaa nimekuwa nikienda Stendi ya Mbezi Magufuli (Magufuli Bus terminal) nikiwa nasafiri au kupokea ndugu na jamaa zangu, lakini kuna jambo sio rafiki kabisa linafanywa na baadhi ya wahudumu wanaotoa kadi kwa ajili ya kuingia ndani ya stendi hiyo linatakiwa kukemewa.
Kwa kawaida utaratibu uliopo unamtaka Mwananchi kulipia kiasi cha Tsh. 300 kuingia ndani, lakini baadhi ya wahudumu hawarejeshi chenji hasa ya Tsh.200 wanataka wakate Shilingi 500, wanapoulizwa wanasema hawana chenji wakati mwingine wanachagua Mtu gani wamrejeshee cheji yote kwa kumuangalia jinsi alivyo.
Ikitokea Mtu amewakazia wanamrejeshea hela yake wanamwambia kama anataka akatwe Shilingi 300 basi atafute chenji awapelekee kiasi kamili, wanafanya hivyo huku wakiwa wanatoa majibu na lugha zisizo rafiki kwa wapokea huduma jambo ambalo wakati mwingine linaibua mizozo.
Mazingira hayo nimeyashuhudia mwenyewe mara kwa mara watu wakikatwa shilingi 500 huku wengine wakisimamishwa pembeni kwa muda mrefu na kuambiwa kwamba wangojee chenji hata kama wanayo, lakini wanatumia mbinu hiyo ili kuwakatisha tamaa baadhi ya watu waweze kuacha chenji hiyo kwa kuwa wanajua wengi wanakuwa na haraka.
Nitoe wito wangu kwa mamlaka zinazosimamia stendi hiyo kufuatilia na kuwachukulia hatua wahudumu wanaobainika kukosa uadilifu na kama kuna upungufu wa cheji suala hilo lishughuliwe ipasavyo ili kuondoa kero na usumbufu.