Kero ya Usafiri
Kumekuwa na tabia ya baadhi ya madereva wa daladala kupaki na kupakia abiria nje ya vituo rasmi, hususan katika vituo vya Keko Bora (maarufu Tameco), Maduka Mawili na Serengeti kwa daladala zinazotoka katikati ya jiji kuelekea Temeke kupitia Chang’ombe.
Utaratibu huu umekuwa ukisababisha msongamano mkubwa wa magari na kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara, hasa wanaotokea Barabara ya Kilwa kuelekea Keko na maeneo mengine ya jiji.
Ni muhimu mamlaka husika zichukue hatua za haraka kukomesha tabia hii ya baadhi ya madereva kupakia na kupaki nje ya vituo vilivyotengwa kwa ajili hiyo.
Cha kushangaza ni kwamba vituo hivyo vina uwezo wa kuhudumia zaidi ya daladala tano kwa wakati mmoja, lakini havitumiki ipasavyo. Hivyo, usimamizi madhubuti unahitajika ili kuhakikisha vituo vinatumika kama ilivyokusudiwa na kuondoa usumbufu unaowakabili watumiaji wa barabara.