Katika juhudi za kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu katika Mkoa wa Dar es Salaam, uongozi wa mkoa huo umeamua kuanza rasmi ujenzi wa shule za ghorofa na kuachana na ujenzi wa shule za majengo ya kawaida ya chini.
Kauli hiyo imetolewa, Septemba 16, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa shule mbili za sekondari za ghorofa zinazojengwa katika Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Chalamila amesema kuwa ujenzi wa shule hizo ni mwanzo wa mwelekeo mpya wa miundombinu ya elimu, na kwamba utaratibu huo utaendelea hadi kwenye sekta nyingine kama afya, ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi hata katika maeneo yenye ufinyu wa ardhi.
Aidha, Chalamila ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imejipanga kutekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 70, fedha ambazo zinatokana na mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mara wanapoona miradi ya serikali imekwama, ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watumishi wachache wanaohujumu fedha za umma. Amesisitiza kuwa ni bora kuwawajibisha wachache wanaozuia maendeleo, badala ya kuwaacha waendelee kuchelewesha utekelezaji wa miradi muhimu ya wananchi.