R.B
JF-Expert Member
- May 10, 2012
- 6,296
- 2,575
Jaji Joseph Warioba
Awamu ya nne, ambayo ni ya mwisho ya kukusanya maoni binafsi ya wananchi kuhusu Katiba Mpya, kunakofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaanza Jumatatu ijayo hadi Desemba 19, mwaka huu, katika mikoa sita, ikiwamo Dar es Salaam.
Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid, alisema jana kuwa mikoa, ambayo maoni hayo yanatarajiwa kukusanywa na tume hiyo katika awamu hiyo, sanjari na Dar es Salaam, ni Arusha, Simiyu, Geita na Mara na Mjini Magharibi.
Alisema taratibu zote za kuanza kazi ya kukusanya maoni katika mikoa zimekamilika, ikiwamo kuandaa ratiba na kuisambaza katika ofisi za mikoa, wilaya na halmashauri za manispaa na wilaya husika.
Wajumbe wa Tume na watumishi wa Sekretarieti wamejigawa katika makundi saba. Kila mkoa utakuwa na kundi moja isipokuwa Dar es Salaam, ambao utakuwa na makundi mawili, alisema Rashid.
Alisema katika mkoa wa Dar es Salaam, tume imejigawa katika makundi mawili na siku hiyo ya Jumatatu itaanza na Wilaya za Temeke na Ilala.
Rashid alisema katika Wilaya ya Temeke, tume itaanza na eneo la Keko wakati katika Wilaya ya Ilala itaanza na eneo la Jangwani kwa mikutano itakayoanza saa 3:00 asubuhi.
Alisema kwa mikutano ya alasiri, wilayani Temeke mkutano huo utafanyika Changombe na ule wa Ilala utafanyika Tabata, wakati kwa upande wa Mkoa wa Arusha, itaanza na Wilaya ya Karatu eneo la Mbulumbulu na mkoani Mara, itaanza katika Wilaya ya Tarime eneo la Bumera.
Kwa Mkoa wa Simiyu, alisema tume itaanza na Wilaya ya Busega eneo la Lamadi na mkoani Geita, itaanza na Wilaya ya Chato eneo la Kachwamba, wakati kwa Mkoa wa Mjini Magharibi, itaanza katika Wilaya ya Magharibi.
Aliwaomba wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na tume na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kwa kuzungumza na kwamba, pale wanapokosa nafasi ya kuzungumza, watumie fursa ya kuwasilisha maoni yao kwa maandishi kwa kutumia fomu maalum zitakazokuwa zinatolewa na tume katika mikutano hiyo.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba amesema tatizo la vyama vya siasa, kuwatumia wananchi kuwasilisha maoni yao badala ya wananchi kutoa maoni yao wenyewe limepungua kwa kiasi kikubwa.
Alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa majaji wa Mahakama ya Tanzania, kwa ajili ya kuzungumzia suala la Katiba na Mahakama, jijini Arusha.
Alisema katika ukusanyaji wa maoni changamoto kubwa waliyonayo ni ya muda wa miezi 18 waliyopewa kuwa ni mchache kwa sababu walitakiwa kuanza Mei 2, mwaka huu, lakini utokana na sababu za maandalizi, walichelewa na kuanza Julai, hivyo wanahitaji muda zaidi wa ukusanyaji maoni hayo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alisema wameamua kupeleka mada hiyo ya katiba na utoaji wa haki, sababu majaji ndiyo wanaosoma katiba kila siku na kuifanyia kazi, hivyo, akawaomba kutumia uzoefu wao kutoa mchango kwenye kuandika Katiba mpya itakayofaa.