Hata hivyo, mradi wa kujenga daraja la Kigamboni ni mzuri sana mathalani pale mtu unapofanya tathmini yake kiuchumi na kwa jamii nzima ya watu ambao shughuli zao za kimaendeleo kwa siku hazikamiliki, au ni sawa na ndoto za alinacha wasipopanda feri kuvuka upande mmoja kwenda mwingine. Lakini pamoja na faida zote zinazoambatana na mradi huu, hatuoni kama serikali yetu ina watu makini wa kusimamia ukamilishwaji wa mradi huu. Kama ilivyokuwa miradi mingine, na huu hivyohivyo, umebakia 'mpango mtakatifu' uliolala kwenye mashelfu ya wataalamu wetu! Who cares, and why should you ever care? Kila mtu na hamsini zake! Ugonjwa wa nchi yetu hii isiyokuwa na MPANGO MBIRINGIKO WA MAENDELEO (Strategic Development Plan), ni kwamba watu na hata viongozi wetu wanapigania kufa na kupona mambo ambayo kwa namna moja au nyingine yana manufaa kwao sasa (have immediate effect/returns) lakini sio yale ambao kwa kuyafanya leo, manufaa yake ni kwa vizazi vijavyo (future returns). Hapa, ndipo tunapotofautiana kimipango na wenzetu wa Ulaya. Kwa mfano, wakati nchi zetu za ulimwengu wa tatu wanawekeza asilimia 60% na zaidi kwenye mambo ya leo, mengi yao yakiwa ni ya kulika leoleo; wenzetu wanawekeza nguvu zao na rasilimali zako sawa na zaidi ya kiasi tunachowekeza kwenye ulaji leo hii, kwenye mikakati ya kimaendeleo ya baadaye.
Na kwa hili tusiwalaumu watu wa Magharibi, kwamba wao ndio waliosababisha kudorora kwa maendeleo ya nchi za ulimwengu wa tatu kwa maana kama ni elimu wametufundisha, na kumbuka kupanga ni kuchagua. Sasa kama ndivyo, alaumiwe nani na aliyekuambia uwekeze sehemu kubwa ya pato lako kwenye ulaji na usiwekeze kwenye maendeleo ni nani?