Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, Naitapwaki Tukai amekutana na Viongozi wa makundi mbalimbali ya Viongozi wa Dini, Mila, Wafanyabiashara akiwaomba watumie nafasi zao kuwahamasisha Wananchi kushiriki uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, kwa amani na utulivu.
Naitapwaki, amesema hayo wakati wa kikao maalumu na viongozi wa makundi hayo, kilichofanyika ofisini kwake, akibainisha kuwa serikali haitamvumilia mtu yeyote mwenye nia ovu, ya kutumia uchaguzi huo kusababisha machafuko hivyo watumie nafasi kuchagua viongozi kwa mustakabali wa maendeleo ya maeneo yao.
"Tukawaeleze watu wote siku hiyo sio siku ya vurugu na kila mtu akapige kura akimaliza aende nyumbani, asitokee mtu yoyote anaenda barabarani kuandamana, akienda inamaana anaichikonoa Serikali na Mimi kama Mkuu wa Wilaya sitakubaliana na chokochoko ya mtu yoyote” alisema Naitapwaki
Kwa upande wao, Viongozi wa dini wamesema kuwa watanzania hususani wakazi wa Wilaya ya Nzega hawana budi kuendelea kulinda amani ya nchi, na kwamba kuchagua kiongozi kwa kupiga kura ni takwa la kidini pia.