The Watchman
JF-Expert Member
- Nov 7, 2023
- 896
- 1,427
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas James Lyimo amesema wamefanikiwa kukamata Kilogramu 1066.105 za dawa za kulevya,mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, kuteketeza hekari 157.4 za mashamba ya bangi.
Akizungumza na wanahabari Jumanne Novemba 12, 2024, Dar es Salaam na kueleza kuwa kati ya mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu zimekamatwa kilogramu 687.2 za skanka na kilogramu moja ya hashishi eneo la Goba jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema kumekuwa na ongezeko la watumiaji wakubwa wa dawa za kulevya aina ya skanka ikiwa wanaoongoza ni wanawake, huku sababu ya ongezeko hilo ikitajwa kuwa kupambana na msongo wa mawazo ambao umekuwa ukiwasumbua haswa ukitokana na udanganyifu wanaokutana nao kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema sambamba na kukamata dawa hizo, wamemkamata muuzaji maarufu wa dawa hizo kutokea mkoani Dodoma ajulikanaye kama Suleiman Mbaruku Suleiman maarufu kama Nyada(52) pamoja na Kimwaga Msobi Lazaro (37), ambapo Nyanda alikuwa ni kinara wa uuzaji wa dawa hizo, na kwamba hatua za kisheria zinaendelea dhidi yake.
Aidha Kamishna Jeneral Lyimo ametoa wito kwa Watanzania kuachana na utumiaji, pamoja na uuzaji wa dawa za kulevya kwani serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeongeza umakini wa kufuatilia na kudhibiti dawa hizo.
Soma pia: DCEA yakamata kilo 767.2 za dawa za kulevya katika operesheni maalum, 21 mbaroni