TANZANIA inaongoza kwa kuwa utawala wa kidemokrasia katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwa mujibu wa ripoti ya matokeo ya utafiti.
Licha ya kuongoza Afrika Mashariki, Tanzania inashika nafasi ya 12 katika ya nchi 50 za barani Afrika na nafasi 97 duniani kati ya mataifa 167.
Utafiti huo umetolewa hivi karibuni na Wataalamu wa Taasisi ya Kimataifa wa Utafiti na Ushauri wa Kiintelijensia (EIU) uliochunguza mienendo ya tawala zote zilizochaguliwa kidemokrasia duniani hadi kufikia mwaka 2008.
Nchi nyingine zinazoifuatia Tanzania katika ukanda wa Afrka Mashariki pamoja na nafasi inazoshikilia Afrika na dunia ni Uganda (Afrika 16, dunia 101), Kenya (Afrika 17, dunia 103), Burundi (Afrika 19, dunia 106) na ya mwisho ni Rwanda (Afrika 26, dunia 121).
EIU, ambayo makao yake makuu yapo jijini London, Uingereza inaeleza katika utafiti huo kwamba nchi 10 kumi bora kwa demokrasia barani Afrika ni Mauritus, ambayo inaongoza na kufuatiwa na Afrika Kusini, Botswana, Guinea, Namibia, Lesotho, Benin, Mali, Madagascar, Msumbiji wakati Ghana ni ya 11.
Tawala zilizoonyesha demokrasia hafifu zaidi barani Afrika ni Chad, ikifuatiwa na Jamhuri ya Afrika Kati, Guinea-Bissau, Libya, Guinea, Guinea ya Ikweta, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Eritrea, Djibuti na Togo.
Ripoti hiyo inaonyesha nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na demokrasia ni Sweeden ambayo inafuatiwa na Norway, Iceland, Uholanzi, Denmark, Finland, New Zealand, Uswisi, Luxembourg, Australia na Canada.
Licha ya mataifa makubwa kama Marekani, Uingereza, Ujerumani na Ufaranza kuonekana kuwa vimbelembele wa kuhimiza demokrasia duniani, hayamo kwenye kumi bora ya orodha hiyo.
Ujerumani inashika nafasi ya 1), Marekani (18), Uingereza (21) na Ufaransa (24).
Tawala zinazoshika mkia duniani kwa demokrasia hafifu ni Korea ya Kaskazini, Chad, Turkmenistan, Uzbekistan, Myanmar, Jamhuri ya Afrika Kati, Saudi Arabia, Guinea Bissau, Libya, Laos, Syria, Guinea ya Ikweta na DRC.
Kwenye ripoti hiyo, EIU imegawanya demokrasia katika makundi makuu manne; demokrasia iliyokomaa; demokrasia inayokua; demokrasia ya mchanganyiko inayotokana na matakwa ya watu lakini inayoaandamana na vitendo vya kutumia dola katika kujiimarisha; na kundi la mwisho ni la demokrasia inayotokana na utawala wa mabavu.
Ukiachia kundi la kwanza la demokrasia iliyokomaa, kundi la pili na la tatu linaelezewa na EIU kuwa tawala zake zinaendeshwa kiubabaishaji kwa maana kwamba hazizingatii misingi ya demokrasia. Ingawa kundi la nne lipo katika tawala za mabavu, kuna aina fulani ya utekelezaji wa demokrasia.
Katika mchanganuo huo, EIU inaeleza kwamba ni asilimia 14 tu ya watu duniani wanaoishi katika demokrasia iliyokomaa wakati asilimia 50 wanaishi katika demokrasia ya kiubabaishaji.
Tanzania kwenye mchanganua huo ipo katika kundi la tatu la demokrasia mchanganyiko ambayo ni ya utawala ambao licha ya kutumia demokrasia ina kiasi fulani cha kutumia dola katika kujiimarisha madarakani.
Nchi nyingine za Afrika Mashariki zilizo kwenye kundi hilo ni Uganda, Kenya na Burundi. Rwanda ipo kwenye kundi la nne, ambalo ni la utawala unaotumia nguvu katika kujiimarisha.
Katika Afrika ni Mauritus pekee iliyopo kwenye kundi la demokrasia iliyokomaa.
Afrika Kusini Botswana, Namibia, Lesotho na Benin zimewekwa katika kundi la demokrasia inayokua.
Mataifa makubwa kama vile Ujerumani, Marekani, Uingereza, Ufaransa, Japan, Italia na Canada hazipo kwenye nchi kumi bora katika kundi la demokrasia iliyokomaa.
Utafiti huo unaweka wazi kwamba karibu nusu ya nchi zote duniani zinaendeshwa kwa demokrasia, lakini tawala nyingi hazizingatii mfumo huo kwa umakini.
Kwenye mchanganua huo, Iran na Sudan zipo katika kundi la tawala za serikali zinazoongozwa kimabavu, Iraq na Palestina ziko katika kundi la tatu la demokrasia ya mchanganyiko wakati Israeli imo kwenye kundi la demokrasia inayokua. Somalia haikuwekwa kwenye kundi lolote kutokana na kutokuwa na serikali inayoeleweka.
http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=18711