Anakuzungusha kila siku, anakupenda kweli?
Nazungumzia juu ya wale ambao wapo katika hatua za mwanzo za kutafuta mahali pa kupata pumziko la moyo! Umeshatoa hisia zako kwa muhusika lakini anakupiga chenga, haeleweki, hajulikani kama anakupenda au lah! Mwingine hazungumzi kitu, mwingine hutoa jibu la moja kwa moja, lakini kuna mwingine anakubali lakini mambo anayokufanyia hayana alama hata moja inayoonesha kweli anakupenda au vinginevyo!
Hili ni tatizo, lakini dawa yake imeshapatikana hapa katika Uwanja wa Huba. Tulianza kwa kuona jinsi ambavyo unatakiwa kumsogeza karibu yako mpenzi wako huyo mtata. Kwamba, ujumbe mfupi katika simu yake, waraka pepe na hata kumpigia simu sana kwa siku za awali za uchunguzi wako, inaweza kukupa msaada mkubwa sana kwako.
Kama kumbukumbu zako zitakuwa zipo sawa, utakumbuka nilisema kwamba, unatakiwa kuiongoza siku nzima ya mpenzi wako huyo huku manjonjo yakichukua nafasi kubwa kuliko kitu kingine chochote...uwe kiongozi wa siku yake!
Ukiwasiliana naye kila wakati, ataona unavyomjali na hata kama alikuwa na mpango wa kukutana na patina mwingine, nafsi humsuta, maana kila baada ya muda mfupi, simu yake huingiza sms kutoka kwako. Meseji ambazo bila shaka zitakuwa na ujumbe wa mapenzi, kutokana na hilo, siyo rahisi kuingiwa na hisia za kufanya kitu kibaya, vinginevyo atakuwa hakupendi!
Inashauriwa umpigie simu mara tano au zaidi kwa siku na kumtumia sms kumi au zaidi kwa siku, bila kusahau kuwa unapaswa kumtupia waraka pepe mara moja au zaidi kwa wiki!
Lengo ni kumfanya awe karibu na wewe kila wakati, apende asipende na hiyo ndiyo shabaha yako. Ninachomaanisha hapa ni kumfanya aone kuwa wewe ni sehemu ya maisha yake, sehemu ya siku yake, bila wewe siku haiwezi kukamilika. Fanya hivi kwa siku tatu mfulilizo.
(iii) Baada ya kuona mambo ya msingi ya kuzingatiwa kwa siku tatu mfululizo, sasa tugeukie katika siku tatu zingine. Katika muda huu wa siku tatu, unapaswa kumwekea mitego! Hapa namaanisha mitego ya kimapenzi. Kumbuka kuwa kwa siku tatu za mwanzo umeshamsogeza karibu yako, hafurukuti kwa lolote, umemfanya aishi unavyotaka wewe, ni kama hawezi kufanya kitu chochote kabla hujampa maelekezo, sasa mtege!
Hapa hutakiwi kufanya kitu chochote kwa nia ya kumwonyesha mapenzi, bali kaa kimya! Katika siku hizi tatu, hutakiwi kumwandikia sms, waraka pepe wala kumpigia simu, acha yeye afanye jambo hilo. Usithubutu kumfanyia kitu chochote, naomba hapo nieleweke vizuri. Hupaswi kufanya mawasiliano ya aina yoyote na yeye.
Bila shaka kimya chako kitamfanya akupigie simu, akuandikie waraka pepe au meseji, usijibu waraka pepe wala meseji zake lakini simu yake pokea. Hata hivyo, hutakiwi kabisa kutumia maneno kama, dear, sweetie, mpenzi na majina mengine yatakayoonesha lugha laini ya mapenzi.
Mshangaze katika hilo, labda kama akiomba umwite jina la kimapenzi ndiyo ufanye hivyo, lakini wewe kama wewe usithubutu kufanya hivyo. Akihitaji mkutane, kubali!
(iv) Hapa ndiyo mwisho wa mchezo, ukweli unajulikana katika kipengele hiki. Kama anakupenda kweli, kimya chako kitamfanya akutafute na wakati mwingine atahitaji mkutane kwa ajili ya mazungumzo ya faragha, hapo sasa ndipo atakapokueleza ukweli wa penzi lake, lakini kama hakupendi, hatashtuka na atakuacha, kwa sababu sms, waraka pepe na simu zako zilikuwa zinampotezea muda wake tu!
Jiulize, kama ulikuwa unamkera, kuna sababu gani ya kuwa na mtu ambaye hana mapenzi ya dhati kwako? Hapo ni mwanzo wa utumwa ambao mwisho wake ni mbaya. Bila shaka mpaka hapa, utaweza kugundua kama mwenzi wako alikuwa anakupenda au vinginevyo!