SoC02 Deni halipaswi kukimbiwa bali kulipwa

SoC02 Deni halipaswi kukimbiwa bali kulipwa

Stories of Change - 2022 Competition

Salum Makamba

Member
Joined
Feb 26, 2018
Posts
7
Reaction score
6
Ndugu zangu,

Nadhani neno ‘deni’ si geni machoni mwetu. Ni moja ya kitu mashuhuri katika jamii zetu. Wingi wa neno deni ni ‘madeni.’ Binafsi mtu akiniuliza deni ni nini, nitamweleza kuwa; Deni ni shurti (jambo la lazima kufanya) analovikwa au kujivika kiumbe awe hai au mfu.

Ili twende sawa yanibidi kutoa mifano kadhaa. Nikianza na sehemu ya kwanza ya maana yangu, inayohusiana na madeni ya kuvikwa haya yapo aina nyingi ila nitaeleza mawili. Mosi, ni deni ambalo wenye kuamini Mungu tumevikwa hapa duniani. Tunaambiwa kuwa tumeumbwa ili tumuabudu Mungu. Hatukuchagua tuumbwe lakini tumejikuta tushaumbwa na tumevikwa deni hilo. Pili, ni wale waaminio katika mizimu. Wanamwomba kiumbe ambaye hawajawahi kumwona au walishamwona ila akatoweka na wanataka awasaidie mambo yao yaende. Hata kama mtu huyo hataki atajua mwenyewe lakini kuna watu wanaamini ana uwezo na anaweza kufanya jambo kwa ajili yao.

Ndugu zangu,

Ama katika sehemu ya pili ya maana yangu, inahusiana na deni la kujivika. Hili ni deni ambalo mtu, kikundi, taasisi na kadhalika wanalitengeneza wenyewe kwa utashi wao kutokana na sababu mbalimbali. Miongoni mwa njia za kulitengeneza ni mikopo, ahadi na viapo.

Ni jambo la kawaida pale tunapokwama kwenda kwa ndugu, jamaa au taasisi kukopa ili kuweka sawa mambo yetu. Tunapokopa kwa ajili ya biashara, kodi, ada na sababu nyingine mbalimbali tunakuwa tumeamua wenyewe kujivika (ma)deni .Lakini wakati mwingine tunajivika kupitia ahadi. Kwa mfano, mzazi unaweza kumwambia mwanao akifanya vyema darasani utamnunulia mwanasesere au baiskeli. Hapa tayari unakuwa umejivika deni. Halafu kupitia viapo. Mfano mwepesi katika hili unaweza kupatikana katika masuala ya soka. Sina shaka tushawahi kuwaona na kuwasikia watu wenye kujinasibu kutembea utupu, kutaliki wenza wao na kufanya mambo mbalimbali ikiwa timu wazipendazo zitafungwa. Hapo wanakuwa wanajivika deni.

Ndugu zangu,

Kwa aliyefuatilia utangulizi huo kwa makini atakuwa amegundua kuwa, deni si lazima iwe PESA. Baada ya kutambua jambo hilo muhimu, niwakumbushe jambo lingine kuwa, deni ni dhamana. Ni lazima lipatiwe haki yake vyovyote iwavyo. Ndo maana, watu wa imani tofauti huamini kuwa usipotekeleza deni kuna namna ya kuadabishwa. Wapo wenye kuamini watu kutiwa motoni na wengine kutiwa toharani ili kusafishwa kwa kushindwa kutekeleza haki ya deni. Mbali na masuala ya kiimani, katika jamii zetu tumeona watu wakifungwa, kuuana na kufanyiana mambo mbalimbali baada ya upande mmoja kushindwa kutekeleza haki ya deni.

Ndugu zangu,

Wazee wetu walisema, “Dawa ya deni ni kulipa.” Na huu ndiyo ukweli. Baadhi hupenda kujivika madeni lakini huwa wagumu sana kwenye kulipa. Huu si mwendo mzuri. Unaposhindwa kulipa deni unajitengenezea mazingira ya kutokopesheka na mitafaruku na wanajamii wenzako. Haifai kumkimbia, kum-block, kumkwepa njia au kuacha kuwasiliana na anayekudai. Kama imefika wakati mliokubaliana wa wewe kurejesha amana ya watu na mambo hayajakaa sawa ni vyema kumweleza mhusika. Na uwe ni mkweli wa nafsi yako. Usidanganye kwa kuona kuwa unamkomoa kuchelewa kumlipa au kupanga kutomlipa. Tena wapo baadhi yetu ambao hujitapa kabisa kwa kusema, “Kama serikali inadaiwa mimi ni nani.” Ili tu asilipe deni lake kwa wakati. Usipolipa deni duniani utalilipa huko uendako.

Ndugu zangu,

Deni si jambo jema. Linakosesha amani, utulivu na kusababisha Msongo wa Mawazo. Lakini mambo haya huwa makali zaidi kwa yule asiye na uelewa mzuri wa madeni yake kuliko yule mwenye kuyafahamu madeni yake. Mwingine unakuta mpaka anasahau anadaiwa wapi na wapi. Mambo haya huongeza hofu na mashaka zaidi na zaidi.

Wakili wa Kitanzania, Madam Mariam Mbano amependekeza njia zifuatazo kwa mtu aliye na madeni ili yasiweze kumchanganya na kumkosesha amani. Njia hizi zinamfaa kila mmoja wetu kwa sababu kwa namna moja au nyingine tunaweza kujikuta tukiingia katika madeni. Njia zenyewe ni:-

  • Orodhesha madeni yako yote, kiasi chake na watu ama taasisi zinazokudai.
  • Angalia kila deni na muda wake. Ni muda gani sasa unadaiwa deni hili au lile.
  • Kama ni madeni yanayohusisha riba basi angalia kila deni na kiasi chake cha riba kisha yapange kuanzia yenye riba kubwa hadi ndogo.
  • Tambua wadeni ambao ni wasumbufu na wadeni ambao wanaweza kuvumilia.
  • Tambua madeni ambayo yanaweza kukuletea madhara makubwa kama vile kuuzwa kwa mali zako au kudhalilishwa.
  • Weka utaratibu wa jinsi gani utalipa madeni hayo kwa kiwango gani na kwa muda gani.
  • Kuwa mwaminifu juu ya utaratibu uliojiwekea.
  • Wasiliana na wadeni wako, waambie unatambua deni, elezea changamoto iliyokupata au zilizokupata, wajuze utaratibu wa namna ulivyojipanga kuwalipa na uzingatie ili kutunza uaminifu.
  • Omba kulipa deni kidogokidogo na kwa mfumo mpya ambao mtakubaliana.
  • Usikimbie deni kwani kukimbia deni hakumalizi matatizo bali kunayaongeza zaidi.
  • Usiendelee kukusanya madeni bali tafuta utaratibu mzuri wa kulipa uliyonayo.

Ni vyema kila mmoja wetu akazisoma njia hizi na kuzielewa vyema. Ikibidi hata kuchukua karatasi na kuzinakili pembeni ili kuweza kukabiliana na madeni bila presha kubwa.

Ndugu zangu,

Wapo watu ambao hupenda kufanya yaliyoelezwa katika njia namba 11. Wanatengeneza madeni ili kulipa madeni bila kutambua ikiwa jambo hilo ni miongoni mwa utaratibu mzuri au la. Kwa baadhi ya watu hufaa lakini kwa wengi husababisha majuto na fedheha.

Kabla ya kutengeneza deni ili kulipa deni jaribu kutafuta kwanza msaada. Mwombe tahafifu anayekudai, kaombe usaidiwe ulipaji wa deni katika nyumba za ibada au tazama namna unavyoweza kucheza na kipato chako hata kama ni kidogo namna gani ili kulipa deni ulilonalo. Ikiwa yote haya yatashindikana basi ndo uingie katika hilo la kutengeneza deni ili kulipa deni.

Ndugu zangu,

Natambua wapo wenzetu wanaopitia hali ngumu wakati huu katika kukabiliana na madeni yao. Nawaombea kwa Mola awape nafuu na awafungulie namna nyepesi zitakazoweza kuwafanya walipe madeni yao kwa haraka ili wabaki na utulivu wa nafsi.

Yaonekanayo magumu kwetu wanadamu kwa Mola ni mepesi.

Mwanagenzi!
 
Upvote 1
Back
Top Bottom