Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Utangulizi
Nami nasubiri patulie In Shaa Allah nataka niandike jinsi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyochaguliwa kuongoza harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika katika kikao cha watu watatu Nansio, Ukerewe nyumbani kwa Hamza Kibwana Mwapachu mwaka wa 1953 na moja ya sifa kubwa iliyotajwa ni dini yake. Wazalendo hao wote watatu waliokubaliana kumkabidhi Baba wa Taifa uongozi walikuwa Waislam, mmojawapo akiwa Katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika).
Kisha nitaeleza vikao vyote vya dua alivyoshiriki Baba wa Taifa pamoja na Waislam katika kumlilia Allah awape msaada Watanganyika washinde dhulma zote za Waingereza na Allah alikubali dua ya wenye kudhulumiwa.
***
Mwaka wa 1950 uongozi wa TAA ulikuwa chini ya Dr. Vedasto Kyaruzi kama Rais na Abdulwahid Sykes akiwa Katibu na ikaundwa TAA Political Subcommittee (Kamati ya Siasa ya TAA) iliyokuwa na pamoja na Rais na Katibu, wajumbe hawa wafuatao: Sheikh Hassan bin Ameir aliyekuwa Mufti wa Tanganyika, Sheikh Said Chaurembo, Hamza Mwapachu, Steven Mhando na John Rupia,
Katika kipindi hiki cha mwaka wa 1950 Abdul Sykes alikuwa katika majadiliano na Chief David Kidaha Makwaia akimtaka aingie TAA wamchague kuwa rais kisha waunde TANU yeye akiwa rais wadai uhuru wa Tanganyika.
Kwa kuwa hapa tunazungumza nafasi ya dini katika historia ya uhuru wa Tanganyika napenda kueleza kuwa Chief David Kidaha Makwaia hakuwa Muislam ingawa alikuwa mtoto wa Chief Makwaia Mohamed Mwandu.
Wakati huu Abdul Sykes alikuwa mmoja wa viongozi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) lakini hili halikuingia katika fikra zake katika kumtaka Chief Kidaha Makwaia kuongoza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na uhuru ukipatikana awe Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika.
Juhudi hizi hazikufanikiwa.
Mwaka wa 1951 Waingereza walimpa uhamisho Dr. Kyaruzi na kumpeleka Jela ya Kingolwira, Morogoro kisha wakamuhamishia Nzega.
Hamza Mwapachu yeye akahamishiwa Nansio, Ukerewe na yote hii nia ya Waingereza ilikuwa kuivunja nguvu TAA Makao Makuu, New Street kudhoofisha juhudi za kuunda chama cha siasa.
Mwaka wa 1952 Mwalimu Julius Nyerere alipelekwa kwa Abdul Sykes na Joseph Kasella Bantu.
Wakati huu Abdul Sykes alikuwa Kaimu Rais wa TAA na Katibu.
Picha hizo hapo chini aliyevaa kitenge ni Chief David Kidaha Makwaia, Hamza Kibwana Mwapachu, Abdulawahid Kleist Sykes, Mufti Sheikh Hassan bin Ameir na aliyefunga kilemba cha Ki-Omani ni Chief Makwaia Mohamed Mwandu wa Siha.
Itaendelea...