DIRA YA TAIFA YA KUHAMIA KATIKA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KUZINDULIWA MWEZI JUNI
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ameeleza kuwa, mwezi Juni mwaka huu utafanyika uzinduzi wa kitaifa wa Dira ya Taifa ya kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia na Mpango Mkakati wa utekelezaji wa Dira hiyo ambayo itaainisha masuala mbalimbali ikiwemo hatua ambazo Serikali itachukua ili kuwezesha asilimia 80 ya watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.
Waziri Makamba ameyasema hayo tarehe 21 Machi, 2023 jijini Dodoma wakati akitoa elimu ya nishati safi ya kupikia kwa Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) pamoja na Wenyeviti na Makatibu wa UWT wa Mikoa na Wilaya ambao watasadia kulipa msukumo suala hilo na kusambaza elimu husika katika ngazi ya Kata na Matawi nchi nzima.
“Takwimu zinaonesha kuwa, asilimia Nane tu ya watanzania ndio wanatumia nishati safi ya kupikia hivyo, Mhe.Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo kuwa ndani ya miaka 10 asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, ameshatuelekeza tutengeneze Dira, Mkakati na Mwelekeo na pia kuanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi, hii ni kazi kubwa lakini inawezekana na kazi inaendelea.” Amesema Makamba
Ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kulivalia njuga suala la nishati safi ya kupikia ikiwa ni moja ya jitihada zake za kuboresha maisha ya watanzania hasa kinamama.
Makamba amesema kuwa, ustawi wa mwanamke wa Tanzania unahatarishwa na namna anavyotafuta nishati na aina ya nishati anayopikia, “Wataalam wanasema lisaa limoja jikoni ni sawa na sigara 300 sasa hapa unategemea ustawi utatoka wapi?, bahati nzuri Mhe.Rais ameliona hili na kwa Wizara ya Nishati, suala Nishati ya kupikia ni jambo namba moja la kutekeleza ili kuleta ustawi ulio bora nchini.”
Amewaeleza Wajumbe hao pia athari zinazotokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia kama vile kuni ambapo alitaja athari hizo kuwa ni pamoja na magonjwa katika mfumo wa upumuaji, mazingira hatarishi wakati wa kutafuta kuni, wanyama hatarishi na athari katika masomo kwa watoto wa kike.
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.