Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
SHAJARA YA MWANAMZIZIMA:
DK BUSHIRI TAMIM NIMJUAYE
Na Alhaji Abdallah Tambaza
ALHAJI Dkt. Bushiri Salum Tamim (74), aliyefariki Ijumaa Mei 18, mwaka huu, kwenye Hospitali ya Taifa, Muhimbili, alikuwa si tu daktari wa kawaida aliyestaafu kazi hospitalini hapo; lakini pia alikuwa mmoja wa madaktari wachache wa Kitanzania, waliobobea katika Tasnia ya Tiba za Watoto Wachanga (padeatrics) hapa nchini.
Wodi 38 ya Jengo la Wazazi, ndimo alimokuwa akifanyia kazi ya kuwahudumia watoto ‘njiti’ (premature), na wale wenye matatizo mbalimbali yaliyohitaji uangalizi baada ya kuzaliwa. Magonjwa hayo hujulikana kama ‘post natal syndromes’.
Ikumbukwe kwamba, wakati wa ukoloni nchi haikuwa na madaktari wa namna yake, sasa, marehemu aliyeajiriwa kwenye miaka ya 70s, anakuwa miongoni mwa madaktari wa mwanzo kabisa walioijenga tasnia ya tiba hapa nchini hata leo tukafikia tulipo.
Alizikwa makaburini Kisutu, Jumamosi, Mei 19, mwaka huu, katika mazishi yaliyohudhuriwa na maelfu ya waombolezaji kutoka sehemu mbalimbali yaliyoongozwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete.
Wengine mashuhuri waliohudhuria ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mussa Azzan Zungu; Mkurugenzi wa Hospitali ya MNH, Professa Mohammed Janabi; na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata Sheikh Khamis Mataka.
Sheikh Khamis Mattaka, akiandika rambirambi zake kwenye ukurasa wa ‘whatsapp’ wa Klabu ya Saigon ya Dar es Salaam amesema:
“Si kwa udaktari wake, bali ni kwa ule utu, ucheshi na upole wake… alijipambanua akawa miongoni mwa watu wema nchini.”
Makaburini pale, alikuwapo pia, Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni nchini (Hayyatul L’Ullamaa) Sheikh Abdallah Ndauga; Mwenyekiti wa Shura ya Maimamu nchini Sheikh Mussa Kundecha na Katibu wa Baraza hilo, Sheikh Issa Ponda.
CAG mstaafu, Professa Mussa Assad, ambaye ni mdau wa masuala ya Hijja nchini alionekana pia maziarani pale akisalimiana na kupeana mikono na watu mbalimbali, katika kumsindikiza katika safari yake ya mwisho daktari wa mwanzo nchini kutoa huduma kwa mahujaji pale BAKWATA walipoanzisha safari za Hijja miongo mitano iliyopita.
Habari za msiba huu mzito nilizipata mapema Ijumaa Mei 18, asubuhi, kulipopambazuka kutoka kwa ndugu wa karibu wa Dk Tamim, Alhaji Adam Haidar:
“Niko hapa hospitalini Muhimbili; ambako Dk Tamim amefariki muda mfupi uliopita… nasaidiana na mkewe kufanikisha upatikanaji wa maiti haraka, tafadhali waarifu ndugu na jamaa,”aliniambia.
Nilimshukuru kwa taarifa, nikaagana naye kwa huzuni, kusubiria tangazo la ratiba ya mazishi.
Kutwa nzima siku ile, habari za mjini, hasa kwenye mitandao ya kijamii, ilikuwa ni kuhusiana na msiba ule mzito ambao haukuwa umetarajiwa kutokea namna ile.
Kabla ya kuelekea ‘Malaloni Kisutu’ shughuli za mazishi zilifanyika Masjid Shadhily kwa kumwombea dua pamoja na wasifu na risala kutoka kwa masheikh waandamizi wa Jiji la Dar es Salaam.
Msikiti ulifurika watu kama wote, ndani na nje, ikawa hapana hata pa kutia mguu. Waombolezaji waliojawa na huzuni walishindwa kuonyesha tabasamu na bashasha kutokana na wingu la simanzi lilokuwapo mitaa hiyo ya Twiga na Sikukuu, Kariakoo.
Sheikh Mohammed Nassor, Rais wa Wasomaji wa Tajwiid Nchini, ambaye makazi yake kule Kijitonyama, yapo jirani kabisa na nyumba ya hayati Dk Tamim, ndiye aliyesoma Qur’aan kwa ufundi na ustadi mkubwa, akitumia njia (sauti) ya ‘bayyat, sikka, razdi na nakhwandi’.
Dk Tamim alikuwa mpenzi mkubwa wa Quraan, ikisomwa kwa njia ya Tajwiid, kama ambavyo walivyo wazawa na wakazi wengi wa Bagamoyo, ambako Dk Tamim ndiko alikozaliwa na kukulia.
Nasaba yake ama ‘Silsila’, inakwenda mbali sana mpaka kwa Diwani (Chifu) Mwinyimadi Mwinchuguuni ‘wa Mwambao’, kiongozi wa kwanza wa kijadi wa Bagamoyo ya kale.
Dk Tamim, alipata kuniambia: “Mamangu akiniambia kwamba mimi ni kirembwe ama kitukuu cha Chifu Mwinchuguuni ‘wa Mwambao’, aliyepigana na kuwafurusha wapiganaji wa kabila la Wakamba kutoka Kenya kwenye karne ya 1700 kukiwa hakuna nchi inayoitwa Tanganyika,”akisema hayati Tamim kujinasibisha
Sasa, pale nilipokuwa nimekaa msikitini; kuliani kwangu alikuwapo Mwanahistoria mashuhuri nchini Sheikh Mohammed Said; na kushotoni alijiinamia kwa huzuni na mawazo, Balozi Ramadhani Dau. Wote hao walikuwa wamefiwa kikweli kwelI.
Masheikh kwenye safu ya mbele waliwaona. Ghafla, walimtuma mtu aje amwambie Dk Dau kwamba anatakiwa pale mbele ili akatoe wasifu wa marehemu.
Dau alikataa katakata kutokana na kule kuhuzunika kwake; akisema kwamba hiyo itakuwa ni zamu ya Mohammed Said, kwani yeye tayari ‘amepokea jukumu jengine kubwa na zito la kuingia kaburini kuzika.’
Kwa upande wake, Mohammed naye, aliuona ugumu wa kazi hiyo yenye kukutaka umwelezee mtu unayempenda maishani mwako (kama alivyo Dk Tamim kwake), kwa heshima na ufasaha ulionyooka. Aliendelea kukataa, akiomba mtu mwengine apewe jukumu hilo.
Lisobudi hutendwa.
Alinasihiwa tena na tena, ndipo akakubali kwa ‘shingo upande’ kujaribu kuzungumza kitu Allah atakachomwezesha.
Alipokea kipaza sauti, lakini kabla hajasema chochote, alijishika kichwa na kuinama chini akalia sana; hali iliyosababisha watu wengi kulengwalengwa na machozi pale msikitini.
Aliponyamaza kulia aliwatazama watu na kusema:
“…Nilimfahamu hayati Dk Tamim miaka ya 70s, nilipotambulishwa na Daktari Bingwa mwenzake wa watoto Professa Charles Mgone, ambaye ni kakaangu niliyekuwa naishi nyumbani kwake pale hospitalini…
“Sasa kutokana na uungwana wake haikuchukua muda akawa swahiba wangu mpaka leo. “Kwa wasiojua huyu ni daktari pekee aliyekataa kugoma pale madaktari wa Muhimbili walipoamua kugoma wakidai kuboreshewa maslahi yao wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, akisema …hawezi kugoma kwa sababu watu wa hali ya chini wangepata shida kutafuta huduma hiyo kwa malipo, na kama ingetokea mtu angekuja kliniki na kufariki kwa kukosa huduma, angekwenda kujibuje mbele ya Allah, ”amesema.
Uzalendo ule aliouonyesha ulimpatia sifa nyingi ambazo zitabakia milele zikihadithiwa.
Ama angehatarisha maisha yake mbele ya madaktari wenzake ambao wangemwona kama ni kibaraka na msaliti kwao.
Akiendelea, ndugu yangu Mohammed Said aligusia tukio alilosikia kwenye audio likimuhusisha Ustadh Masuud Adam, (msomaji Quraan ambaye sasa anaisha London) alipozungumza kwa simu na babake hapa nchini, wakikumbushana namna hayati Dk Tamim alivyomshughulikia kitabibu wakati zilipotokea changamoto wakati alipozaliwa.
Ndani ya video ile, “Ustaadh Masuud, anaeleza imekuwa kawaida kila alipokutana na Dk Tamim, humtania na kumwambia, ‘We, Mas’uud hebu njoo unisomee Qur’aani nyingi sana ufidie namna nilivyokushughulikia ulipokuwa mdogo…. teh! …teh! …teh! (Tamim alicheka kwa kimaskhara lakini kweli akipenda kusikiliza Quraan ikisomwa kwa mtindo wa tajwiid).”
Aidha, katika umati ule uliokuwa umejazana makaburini Kisutu, walikuwamo watoto (watu wazima sasa), ambao Dk Tamim aliwatibia wakiwa na matatizo mbalimbali pale wodi 38, Jengo la Wazazi, Muhimbili.
Daima Daktari huyu makini, akiwakumbuka na kutaka kujua maendeleo ya watoto hawa ambao aliwashughulikia kwa namna moja ama nyengine siku za nyuma.
Mimi ni shuhuda wa hilo, kwani kila tukikutana naye kusalimiana; kamwe hakusahau kuniuliza habari za mwanangu Yahya; ambaye yeye, kwenye kliniki yake miaka 23 iliyopita, aliligundua tatizo la ‘Utindio wa Ubongo’ (Celebral Palsy) ambalo Yahya anaishinalo hadi leo.
Ugonjwa huo ulilotokana na uzembe uliofanywa na madaktari kwenye hospitali binafsi za malipo:
“Vipi ndugu yangu, mwanangu Yahya na mamake wanaendeleaje!” ni maneno ambayo lazima yatoke kinywani mwake, iwe kwa simu au ana kwa ana tukionana popote.
Sasa ukiyaangalia maneno yake hayo; utaona kwamba hakutumia neno mwanetu wala mwanao; daima akitumia neno ‘mwanangu Yahya’, akiimaanisha mtoto yule ni wake yeye pia.
Sasa, msomaji, angalia utu huo uliojaa mapenzi ya dhati.
Kwa kweli, ni lazima niseme hapa, kwamba watu wa Mzizima na Dar es Salaam yake kwa ujumla, daima tumekuwa tukizawadiwa madaktari wa aina hiyo, ambao walikuwa wakijitoa sana kwetu, katika kutusaidia kupata huduma kwa urahisi kwenye hospitali za umma.
Hapa namkumbuka Dk Hamza Maunda wa Taasisi ya Saratani Ocean Rd. Huyu ni kama Dk. Tamim na wala sijui nani anamshinda mwenziwe.
Wawili hawa walijijengea udugu na urafiki mwingi katika maisha yao ya nje pia.
Ni mwaka jana tu nilikuwa kwenye harusi ya kufana ambapo binti wa Dk. Tamim alikuwa akifunga ndoa na mtoto wa Dk Maunda.
Ni ndoa ya kukumbukwa sana.
Ndani ya orodha ya waja wema hao katika tiba, yumo pia hayati Dk. Buyuni Jahazi, Dk. Ishaak Madjapa, Dk. Ali Salamba, Dk. Magombeka, Dk. Kapesa, Dk. Mlawa, Dk. Chande, Professa Idrissa Mtulia; Dk. Amani Malima wa Kibaha, Pwani; na Dk. Juma Mambo wa Hospitali binafsi ya Mangesani pale Kariakoo.
Madaktari hao niliowaorodhesha hapo juu, utamaduni wao ni uleule kama alivyoudumisha hayati Dk. Tamim. Wakati wowote wako tayari, kukufanyia chochote, bila faida yoyote isipokuwa ahsante yako tu ingetosha.
Leo hii, kama utakaa chini uanze kuwahesabu watoto ambao Dk. Juma Mambo (mwenyewe akijiita Tekelo) amewatahiri hospitalini kwake kwa ada ndogo kabisa; idadi yake hutoweza kuipata.
Ni wengi, wengi, wengi mno, huku akiwa anatoa dawa za ziada pale inapojitokeza tatizo la kuchelewa kupona bila kumbebesha mzigo mzazi wa mtoto.
Huyo ndiyo Dk. Juma Mambo, ambaye mwenyewe amejipachika jina la utani la Tekelo, akijifananisha na yule mganga wa jadi aliyekuwa akitibia kwa kutumia tiba za asili za tunguli.
Hayati Dk. Bushiri Tamim alizaliwa wilayani Bagamoyo mnamo Septemba 23, mwaka 1948. Alipata elimu yake ya Madrassa Zawiani kwa Sheikh Muhammad Ramia hapo hapo Bagamoyo.
Elimu yake ya (msingi), aliipata kwenye Shule ya Sewa Haji Paro mjini Bagamoyo (sasa Shule ya Msingi Mwambao); na baadaye kumalizia kwenye Shule ya Kati ya Miembe Saba, 1965. Sekondari alisomea Mzumbe na H.H. AgaKhan (sasa Tambaza) ya Dar es Salaam.
Kutokana na ufadhili (scholarships) mbalimbali, ikiwamo na ile ya Umoja wa Mataifa (UNDP), Dk. Tamim alipata mafunzo yake ya udaktari nchini Urusi, Malaysia, Norway, Japan na Ulaya New Zealand.
Katika ndoa yake na Bi Maryam, walibahatika kupata watoto 4; wawili wanaume na wawili wanawake wakiwamo na wajukuu 4.
Pamoja na hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hayati Dk. Tamim katika safari yake ndefu ya udaktari, amefanya kazi katika hospitali ya Wilaya kule Mahenge, Morogoro; Hospitali ya Aga Khan na baadaye ile ya binafsi ya Dk. Khalid Khan, zote za jijini Dar es Salaam.
Mwezi mmoja uliopita, akiwa amelazwa pale Sewa Haji 12, Muhimbili hospital, na nikiwa sina habari hizo; Dk. Tamim alinipigia simu na kusema kwa sauti ya kigonjwa:
“Nimelazwa Kibasila 12 ...njoo unione leo, nina jambo zito nataka kuteta na wewe… usiwe na wasiwasi wa kuingia ndani, nitakuwa nimeacha maagizo mtu akusubiri mlangoni; usikose hiyo ni amri!” alimaliza huku akileta na utani kidogo.
Kweli, nilifika na nikapelekwa kitandani kwake, tukazungumza kwa zaidi ya saa 3 mbele ya mkewe na mtoto wake wa kiume, waliokuwa wakimwuguza.
Sasa, ambacho sikufahamu, ni kwamba alikwishajua ana saratani ambayo ingechukua uhai wake wakati wowote, na hivyo kuwaacha wanawe na mkewe wakihangaika na jambo hilo.
Alhamdullilah, na bila kutegemewa; jambo lile kubwa aliloniitia si la kulisema kwa kila mtu likawa jepesi na uvumbuzi ukapatikana ndani ya siku chache tu.
Sikumwona tena.
Na hivyo ndivyo alivyoniambia kwaheri ndugu yangu.
Wengi wakimwiita Tamim Walii wa Mwenyezi Mungu.
Ewe, Mola Mtukufu, Mghufirie madhambi yake kiumbe wako huyu dhaifu; na uifanye pepo ya Firdausi iwe ndio makazi yake.
Ammyn.

Dk. Bushiri Tamim
Picha iliyochapwa ukurasa wa mbele wa Daily News ukimuonyesha akiwa kazini akitibia wagonjwa wakati madaktari wenzake wako katika mgomo mwaka wa 2012
atambaza@yahoo.com; 0715808864