Katika juhudi za kuimarisha usalama na kupambana na uhalifu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (SACP) George Katabazi ameungana na wananchi wa Kata ya Ihumwa kwa kuchangia vifaa vya ujenzi wa kituo kipya cha polisi jijini Dodoma. Hatua hii imeungwa mkono pia na wadau mbalimbali, ambao wamejitolea pesa na rasilimali zingine kusaidia ujenzi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Katabazi amepongeza ushirikiano wa wananchi katika kufanikisha mradi huo, akisisitiza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutakuwa chachu ya kuimarisha ulinzi wa wananchi na mali zao.
"Ujenzi wa kituo hiki utarahisisha utoaji wa huduma za usalama kwa wananchi na kurahisisha upatikanaji wa msaada wa haraka tofauti na ilivyokuwa hapo awali," alisema Kamanda Katabazi.
Aidha, aliwataka wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu, kukemea vitendo vya kihalifu, na kushiriki katika juhudi za kudumisha amani.