USAID ni shirika la Marekani kwa ajili ya maendeleo ya kimataifa, shirika hili linakadiriwa kuwa na budget ya dola Billion 40 za Kimarekani sawa na Shilingi zaidi ya Trilioni 100 za Kitanzania (101,151,160,000,000 Tsh)
Baada ya utawala mpya wa
Donald Trump kuanza kazi January, 2025 nchini Marekani kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika nyanya mbalimbali ikiwemo kusitishwa kwa muda huduma za USAID. Jambo ambalo limekuwa limeibua taarifa nyingi hususan kwa bara la Afrika ikiwa ni miongoni mwa waliokuwa wanufaika wa misaada kutoka kwenye shirika hilo.
Madai
Kumekuwapo na kipande cha video kinachomuonesha Rais wa Marekani Donald Trump akisema kuwa;
“Tumelifunga shirika la USAID, kwani misaada hii ya kimataifa imeifanya nchi za Afrika kuwa wavivu. Tunahitaji kuona nchi hizi zinaendeleza utamaduni wa kujitegemea wenyewe”. Tazama
hapa
Uhalisia wa madai hayo na video hiyo
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck umebaini kuwa Trump hakusema maneno hayo hivyo madai hayo
si ya kweli. Ufuatiliaji wa kimtandao kwa kutumia Google reverse image search umebaini kuwa video hiyo imehaririwa sauti kutoka kwenye maswali na majibu aliyokuwa akifanya Trump na waandishi wa habari Januari 30, 2025.
Kipande hiko cha video kinaonesha tarehe upande wa juu kushoto kuwa ni Januari 30, 2025, ambapo kiuhalisia siku hiyo Trump alitia saini ya baadhi ya mabadilliko ya sheria nchini humo Kisha waandishi wa habari wakamuuliza maswali mbalimbali ikiwemo kuhusiana na ajali ya ndege iliyotokea muda mchache uliopita kabla hajafanya mazungumzo hayo.
Tukio la utiaji saini na maojiano ya waandishi wa habari yamewekwa katika chaneli ya
Youtube ya Ikulu ya Marekani ambapo hakutamka lolote ama kuulizwa kuhusiana na USAID na nchi za Afrika.
Aidha JamiiCheck imebaini utofauti wa sauti iliyopo katika video hiyo na sauti halisi ya Trump, vilevile sauti inayoonekana kwenye video potoshi imeambatana na kelele ama mikwaruzo kila Trump anapozungumza. Kipande cha video potoshi kinafanana na kipande cha video halisi kinachomuonesha Trump akijibu swali la mwandishi wa habari aliyemuuliza kama atakwenda kwenye eneo ambalo ndege imeanguka. Tazama
hapa
Ufuatiliaji kwa kutumia nyenzo ya deepfake total imeonesha
asilimia 99.4 ya sauti inayosikika katika video hiyo si halisi.