Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Doris Mollel , Doris Mollel amesema jengo la kuhudumia Watoto waliozaliwa kabla ya wakati (Watoto njiti) lililojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza, ni jengo lenye ubunifu na viwango vya Kimataifa ikiwemo uwepo wa wodi ya kwanza ya mfano nchini ambayo haimtengi Mtoto njiti na Mama yake (zero separation).
Doris Mollel ameelezea kuhusu maeneo mbalimbali ya jengo hilo nje na ndani akifafanua zaidi kuhusu ubora na upekee wa wodi zilizopo katika jengo na maeneo mengine yenye ubunifu ikiwemo chumba maalum ambacho Familia ikiwemo Baba wa Mtoto watakuwa na fursa ya kumuona Mama akiwa na Mtoto wake kifuani na kumjulia hali, ambapo licha ya uwepo wa jengo hilo mradi huo kwa ujumla unahusisha uwepo wa nyumba mbili za Wauguzi
“Hiki chumba ni sehemu ya akina Mama kuonwa na Ndugu zao hususani Baba mwenye Mtoto, Familia zitatumia eneo hili kuwaona Wapendwa wao ambao wamelazwa wodi hii ya Watoto njiti, hili wazo limetokana na akina Mama wenyewe wakati tumepata mchoro kutoka Wizara ya Afya tukakaa nao chini tukauliza kitu gani haswa kikubwa ambacho mnatamani kukipata ndani ya wodi hii wakasema Wanaume hawaruhusiwi kuingia wodi zile za Kangaroo, tukaona ni wazo muhimu sana Mama anaweza kutoka na Mtoto kjfuani Baba akamuuliza anaendeleaje n.k”
“Eneo lingine ambalo kwangu ni pendwa sana ni chumba maalum ambacho Mimi mwenyewe nilipatiwa huduma miaka ya nyuma wakati nazaliwa Mimi nilizaliwa na gramu 900 pacha wangu alizaliwa na KG 1.2, Mama hapa ana nafasi ya kumuona Mtoto wake akiwa anahudumiwa kwenye mashine, hii ndio maana ya zero separation Mtoto hatengwi na Mama yake, Mama anaona kinachoendelea”
“WHO imehamasisha sana juu ya umuhimu wa kutomtenga Mtoto na Mama yake sisi tumefuata huo mwongozo, wazo hili ni la kibunifu na ni wazo la kwanza kwenye nchi kuwekeza mawazo ambayo yapo katika standard za Kidunia, inaitwa wodi ya kwanza ya mfano”
Your browser is not able to display this video.
Jengo hilo limejengwa na Taasisi ya Doris Mollel kwa ushirikiano na Taasisi ya Msanii maarufu wa Marekani Alicia Keys inayoitwa KEEP A CHILD ALIVE likiwa na thamani ya Tsh. bilioni 2.125.