Wakuu kuna ukweli hapa?
- Tunachokijua
- Julai 18, 2023, Ukurasa wa Instagram unaofahamika kwa jina la DW 24 Swahili uliandika madai ya Kampuni ya DP World kuonesha nia ya kusitisha Mkataba wake na Serikali ya Tanzania unaohusu uwekezaji wa Bandari nchini.
Madai haya yanasema;
“Baada ya maandamano na wanaharakati kukemea mkataba, DP WORLD waomba kuvunja mkataba na kurejeshewa pesa walizotoa hongo $ Million 100, viongozi wakuu watatu, ambao majina yao tutayaifadhi, walipokea pesa hizo Kama hongo, Taarifa zaidi zitakujia hapahapa.”
Tangu taarifa za Tanzania kuingia mkataba na Kampuni ya Dubai ya DP World kuanza kuenea mnamo Juni 5, 2023 mwaka huu na Azimio la mkataba huo lilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Junii 10, 2023, kumekuwa na hoja nyingi zimeibuliwa miongoni mwa Wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi ya Tanzania.
Sehemu za hoja hizo zimejigawa katika makundi mawili ikiwamo wanaopinga kusainiwa kwa mkataba huo wakidai una mapungufu mengi na upande mwingine wanaunga mkono wakiona kwamba mkataba huo una maslahi kwa taifa.
Madai ya DPW kusitisha Mkataba wa uwekezaji nchini
Madai ya DPW kuonesha nia ya kusitisha mkataba wake na Tanzania yameshika kasi siku za hivi karibuni.
Julai 17, 2023, kupitia mjadala wa sauti wa mtandao wa Twitter (Twitter Spaces) unaoongozwa na Maria Sarungi Tsehai, Katibu wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), Catherine Ruge alizungumza suala hili.
Alisema;
"Mimi kuna taarifa nimepata kutoka huko huko Serikalini. Unajua sio kila mtu anafurahia hiki kinachoendelea. Kabla NEC haijafanyika, a week ago, kabla ya NEC, nasikia watu wa DP World wali reach out wakasema sisi hatuwezi kuendelea na mkataba, kuna vurugu huko kwenu, makelele, maandamano, kuna wanaharakati wanapiga kelele, sisi hatuwezi kuendelea na mkataba. Tunataka mrudishe hela zetu tulizowapa"
"Walipewa rushwa, kuna rushwa ilitolewa na dola milioni 100 ambayo ni kama bilioni 250"
Ruge aliendelea kufafanua kuwa rushwa hiyo ilikuwa imetolewa kwa watu watatu ambao kwenye mkataba huu wao ndio masterminds.
"Sasa wakaambiwa turudishieni hela zetu, kwa hiyo ikabidi faster iitwe NEC ili kuweza ku endorse hicho kitu. Ili ionekane kwamba chama kinasapoti, ndio maana ikaitwa NEC faster. Kwa hiyo huu mkataba unahusishwa na rushwa kubwa kwelikweli"
Catherine Ruge alienda mbali zaidi kwa kudai Waandishi na wahariri wamehongwa pia ili kutokuandika taarifa za wapinzani. Alisema haya akirejea mkutano wa Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe aliofanya Julai 14, 2023 kuelezea maazimio ya kamati Kuu ambao JamiiForums ilisaisha mkutano huo kwa andiko lenye Kichwa cha habari "Freeman Mbowe: Tunazindua "Operation +255 Katiba Mpya Okoa Bandari Zetu" kuwaambia watanzania ubaya wa Mkataba wa DP World" ambao kwa maelezo yake haukuripotiwa na vyombo vingi vya habari na magazeti.
JamiiForums imebaini kuwa, madai yaliyotolewa na DW 24 Swahili kwenye Mtandao wa Instagram yanafanana kwa kiasi kikubwa na kauli zilizotolewa na Catherine Ruge. Pia, DW 24 Swahili alichapisha madai haya Julai 18, siku moja baada ya Ruge kuzungumza kwenye Maria Spaces.
Vyanzo vingine vya Madai haya
Ukiondoa vyanzo hivi viwili vilivyo jadiliwa hapa ambavyo muktadha wa maudhui yake unafanana, JamiiForums haijapata uthibitisho mwingine kutoka upande wowote, ikiwemo Serikali, kampuni yenyewe ya DP World au vyanzo vingine vya kuaminika vinavyoweza kutumiwa kama rejea ya kufikia hitimisho.
Hata hivyo, Julai 13, 2023, mtumiaji wa JamiiForums alichapisha taarifa zinazodai kuwa Kampuni ya DP World ilikuwa imesikia malalamiko ya wananchi kuhusiana na Sakata hilo. Alisema;
"Hatimaye, malalamiko ya watanzania kuhusu uhalali na vipengele vya Mkataba kati ya Tanzania na Emirati ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World yamewafikia na kuwashtua wahusika. Taarifa za uhakika nilizozipata zinaonesha kuwa DP World wamesikia hoja za wazalendo wa kitanzania na wameguswa nazo.
Katika kutaka kujiridhisha ili kutoa uamuzi juu ya nini cha kufanya, DP World imewatuma nchini Maafisa wake watatu ili kupata undani wa jambo hilo. DP World imewatuma Maafisa wake hao ambao wamewasili nchini jana na wanatarajiwa kuzungumza sirini na makundi tofautitofauti.
Maafisa hao watazungumza na viongozi wa kiserikali na kichama-CCM; viongozi wa TPA; viongozi wastaafu mbalimbali wenye 'kuukubali' na wale 'wa kuupinga' Mkataba huo; wanasheria mbalimbali wenye mtazamo tofauti; wasomi wenye mtazamo tofauti, wanasiasa na wananchi wa kawaida.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa DP World kufanya jambo kama hili ili kuamua cha kufanya kabla ya muda wa kuingia Mikataba Mahsusi kufika. Kwangu mimi, hii ni hatua muhimu na adhimu kwakuwa DP World watayasikia yale yanayofurahisha na kukatisha tamaa kuhusu Mkataba wao."
Pamoja na uwepo wa tetesi hizi za kusikiliza mapendekezo na malalamiko ya makundi tofauti kabla ya kuingia mikataba mahsusi, JamiiForums haijapata uthibitisho unaoweka bayana lengo la kampuni hiyo katika kusitisha Mkataba wake na Tanzania.